Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na ninakuomba kwa huruma ya kiti kabla sijaanza mchango wangu, nitoe pole kwa wazazi wa kijana William Manento Elifuraha aliyepoteza maisha hapo UDOM akiwa katika matibabu. Yeye ni kijana aliyekuwa mwaka wa tatu katika ndaki ya elimu na ninapozungumza hapa sasa hivi waliondoka jana kusafirisha. Kwa hiyo, wale ni eneo ninalotokea, nasikitika nao na pia nawapa pole. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo sasa niingie kwenye mchango, awali ya yote namshukuru Mungu kwa kutupa uhai wote na kuweza kuwa hapa kuongelea mambo ya maendeleo. Leo tunaongelea eneo ambalo ni mtambuka. Tunaposema Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ni Wizara ambayo inagusa kila mahali. Lakini nichukue fursa hii kipekee kabisa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuona umuhimu kurejesha Wizara hii. Hii Wizara ni nyeti na inahitajika sana kwa sababu inagusa maeneo yote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze tu na masikitiko kwamba bajeti iliyosomwa hapa ya kiwango hicho cha shilingi bilioni 43.4 kwa Wizara kubwa kama hii na mpya ninaiona kama ni ndogo, lakini basi kwa vile tumeshapita katika mchakato wote na inaonekana, nimpongeze sana Dkt. Dorothy Gwajima kwa wasilisho lake na inaelekea inakwenda kufanya kazi. Lakini nimpongeze pia Naibu Waziri pamoja na timu yao ya Katibu Mkuu na wote ambao anafanya nao kazi. Leo nitazungumzia zaidi kwenye eneo moja tu la maendeleo ya jamii kwa sababu, nikianza kutangatanga huko nitapotea njiani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, waajiriwa hawa wa maendeleo ya jamii katika lugha nyepesi ningeweza nikawaita social engineers. Kuna ma-engineer wa ujenzi (civil engineers), kuna technical engineers, kuna electrical engineers na kadhalika, lakini hawa ni social engineers kwa sababu bila hao hakuna linalofanyika chini kwenye jamii. Lakini nimesikitika tu kwamba katika kwenda sasa kuchukua mafunzo wanakwenda wakipungua na katika wasilisho la Mheshimiwa Waziri amesema wako wachache na hata hawatoshelezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niiombe sasa Serikali itoe kibali maalum kwa wale ambao wamehitimu na wako mitaani wote waajiriwe na sio lazima waajiriwe Serikalini, hawa wanatakiwa wawe katika kila taasisi lazima kuwe na Afisa Maendeleo ya Jamii. Kwa nini nasema hivyo, kwenye maji kama ni kwenye Taasisi za Maji lazima wawepo, waweze kuwafundisha watu utumiaji mzuri wa maji na jinsi ya kutunza maji na pia kutunza vifaa vya maji. Lakini ukienda benki lazima wawepo wawafundishe watu jinsi ya kutunza fedha waende, kuna benki mpaka sasa hivi zina shilingi bilioni tisa za dividend zimekaa tu hakuna wachukuaji kwa sababu hawajaelimishwa kule chini. Wangekuwa na Afisa Maendeleo ya Jamii na hapa nazungumzia CRDB, wangeshatoa elimu watu wao wakaenda kutoa elimu watu wakaja kuchukua dividend zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia hata kwenye elimu na kwingineko tatizo ninaloliona/changamoto kubwa, hawa Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa hawana Idara yao, wao wako wame-hang mahali. Sasa hili ni tatizo kubwa mno wao wako chini ya mtakwimu na wanapokuja sasa kwenye level ya kutoa maamuzi wao wanapelekewa na hao, watanisahihisha watakapokuja kutoa, lakini nina uhakika nalo kwa sababu hata mimi katika kusoma kwangu mambo mengi nilichukua pia Diploma ya Community Development, najua jinsi gani cadre hiyo inanyanyasika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini naomba basi twende mbele zaidi tunapokuja kwenye halmashauri kazi zao ni nyingi mno Maafisa Maendeleo ya Jamii. Tukizungumza marejesho ya ile asilimia kumi inayotolewa na Serikali 4-4-2 tunasema kila siku ni revolving funds, lakini hazirudi lakini wako mbali, utoke mjini au utoke makao makuu mpaka ukafike kijijini kule. Kwa hiyo, siku hizi pia kuna hizi simu wanaingia kwenye simu wanauliza marejesho hawawezi kwenda, labda waombe gari kwa RAS na kama kuna mitihani waombe gari kwa Afisa Elimu, waombe gari kwenye Idara ya Afya, waombe gari ni lini sasa tutawapatia magari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiangalia hii bajeti ya leo ya shilingi bilioni 42 nimechukua Randama mezani, sijaona kwenye maendeleo kama kuna fedha za kununua magari naomba sana hili jambo lifikiriwe. Lakini nimechukua mimi Ilani ya CCM imezungumzia vizuri sana kwenye ule ukurasa wa 279 na hii nataka niseme wazi ni Wizara ya Muungano, ni Wizara kubwa sana, ndani ya TAMISEMI ukiuliza Wizara zote mtasema Elimu, mtasema sijui nini, lakini hii ni kubwa mno. Nawaomba sana yaani naiomba Serikali yangu sikivu iangalie sasa baada ya kutupa Wizara kamili iangalie inakwenda kuiwezesha vipi, lakini pia nataka niombe hata hao wafadhili waiangalie kwa jicho la pekee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inapokuja kwenye NGOs nipongeze NGOs zote Tanzania, zimejitahidi sana kutoa elimu kwenye eneo hili, zimejitahidi sana kuelimisha makundi mbalimbali, lakini inapokuja sasa Ofisa Maendeleo ya Jamii anakwenda kukagua NGO na NGO hiyo haiko karibu, yule mwenye NGO atamuwezesha. Sasa unapowezeshwa na mtu yule ukaenda kukagua wewe unakwenda kufanyaje sasa kusema hii ni hapana. Hapo hakuna rushwa ila kuna huruma, wewe umeniwezesha nimetoka mjini, labda nimetoka Dodoma ninakwenda kukagua kule mbali kabisa yaani sijui ni Kata gani ya mbali kabisa huku Dodoma. Halafu nafika naona mambo hayapo hivi nakujaje mimi kumpa alama za chini! Sio kitu kirahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mimi ninaombi maalum chenji ya zile fedha za Covid-19 kama kwenye maeneo mengine, ikiweko ile ya Maliasili wataona kwamba wanahitaji Ofisa Maendeleo ya Jamii naomba wapatiwe. Kwa nini nikasema ile chenji zile fedha zilishagawiwa kwa maeneo muhimu, lakini kuna hawa Maafisa Maendeleo ya Jamii wangetakiwa sasa watumike, kwa sababu mnavyotuletea viosha mikono mabomba na nini bila Maafisa Maendeleo ya Jamii kupita na kuingia kwenye kaya, kuingia kwenye makanisa, kuingia kwenye misikiti kuelimisha watu nani anakwenda kutoa hiyo elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naongea kwa uchungu nikisema kwamba hata ukija kwenye political issues, economic issues mimi kila siku nasimama hapa naomba vifaranga vya kuku, naomba mitamba ya ng’ombe lakini Maafisa Maendeleo ya Jamii wao ndio watakwenda kule kuwaambia mkifuga…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele ya pili hiyo Mheshimiwa.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naunga hoja mkono asilimia 100 na ninawaomba wenzangu wote tuunge hoja mkono na tuzidi kwenda nao ahsante. (Makofi)