Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi asubuhi ya leo na mimi kuwa miongoni mwa wachangiaji kwenye bajeti ya Wizara hii mpya ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.

Awali ya yote nianze kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan na kumpongeza kwa maono yake ya kuirejesha Wizara hii, kama walivyosema waliotangulia na umuhimu wa Wizara hii tumeuona namna ambavyo Mheshimiwa Waziri nikupongeze Dkt. Gwajima na Naibu Waziri wako na watendaji wote kwa kazi nzuri na mchakamchaka mliouanza mara baada ya kuundwa kwa Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze kwenye mpango kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto ambao unatarajia kukamilika Juni, 2022 na kwa mujibu wa maelezo ya Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake wanatarajia kufanya tathmini ya kina ya mafanikio ya mpango huu. Pamoja na kwamba inaonesha mpango huu umepunguza matukio ya ukatili kwa wanawake na Watoto, lakini ninadhani kuna haja kama Taifa kujipanga kuangalia namna gani ya kushirikiana pamoja na Wizara na Serikali kupunguza matukio ya ukatili. Ukiangalia takwimu zinatisha kwa Januari, 2019 mpaka sasa matukio ya ukatili jumla yake yalikuwa kama 29,000, lakini miongoni mwao matukio ya kubakwa kama 19,000 ni kama asilimia 70 na katika hayo yaliyofikishwa mahakamani ni kama asilimia 75. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo unaona yapo baadhi ya matukio pia hayafikishwi mahakamani, lakini yaliyohukumiwa ni kama asilimia 67. Kwa hiyo naunga mkono kama alivyosema mmoja wa wachangiaji kwamba tatizo hili ni kubwa na katika moja ya changamoto hasa matukio ya kulawiti watoto wa kiume zaidi ya 3,000 kati ya 3,260 asilimia 94. Pamoja na maendeleo yanayofanyika Serikali inafanya vizuri kwenye sekta mbalimbali, lakini sekta hizo maendeleo haya yanaweza yakawa hayana maana, kama tunaandaa kizazi cha watoto wengi wanabakwa kama tunaandaa kizazi cha watoto wa kiume wengi wanalawitiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba sana Serikali nilikuona Mheshimiwa Waziri Gwajima unavyoshirikiana na Wizara zingine mfano Mambo ya Ndani, mfano Wizara ya Katiba na Sheria kama pana mapungufu mbalimbali ya kisheria, kwa sababu adhabu ya miaka 30 ipo, kifungo cha maisha ipo, lakini haipiti wiki haujasikia tukio la kubakwa, kulawitiwa na vipigo na kinachosikitisha zaidi matukio haya sasa yameambukiza ndani ya familia. Unamkuta baba anabaka watoto, wake baba analawiti watoto wake, mjomba, kaka nadhani tumuombe Mwenyezi Mungu atuwezeshe na viongozi wa dini muendelee kukemea haya matukio. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na hayo jamii/wazazi hasa wanawake tumrudie Mwenyezi Mungu tutafakari namna ya malezi ya vijana wetu. Nalisemea hili kwa uzito kwa sababu na kwa hisia kubwa tunaanza kuwa na hofu unapokuwa na watoto wa kike, wa kiume humuamini hata jirani, humuamini mume wako, humuamini ndugu yako, tunakwenda wapi? (Makofi)

Kwa hiyo, naiomba Serikali hata pale tutakapokuwa na tafakuri au tulete adhabu zaidi, tunaanza kufikiria au hawa wanaume tufanyeje au wahasiwe? Nadhani tunahitaji kuangalia haiwezekani kwa hiyo nadhani tunaomba Watanzania, hebu tuangalie hebu tutathmini kwa nini kila siku matukio yanajitokeza? Tuiombe mahakama iende mbele kutenda haki. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, lakini la pili nilikuwa naangalia hotuba pia ya Wizara hii pamoja na mambo mbalimbali, lakini kama alivyosema Mheshimiwa Mama Shally upo upungufu mkubwa wa watumishi. Naiomba Serikali tunaona juhudi za Mheshimiwa Rais hata jana zimetangazwa ajira zaidi ya 1,000 na amekuwa mama ambaye anatoa ajira amevunja rekodi, lakini tunamuomba kwa dhamira yake namna gani anavyoguswa na matukio ya ukatili wa kijinsia aitazame Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii kuweza kuipa kibali mahususi. Kwa ajili ya Maafisa Maendeleo ya Jamii ambako kuna upungufu wa zaidi ya asilimia 43, lakini kwa Maafisa Ustawi wa Jamii ambako kuna upungufu wa asilimia zaidi ya 90. Hawa Maafisa ndio watakaosaidia kuelimisha jamii namna gani katika sekta mbalimbali, lakini kuongoza mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na hilo naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo ameunda kamati ya kumshauri masuala ya kijinsia, lakini sambamba na hilo kuchagua eneo mahususi la haki na uwezeshaji wa wanawake. Tumeona kwenye masuala ya haki hivi karibuni mtandao wa haki umempa Tuzo naona ambavyo alivyoanza. Lakini kwenye masuala ya uwezeshaji wanawake tunamshukuru sana kwa kuendelea kusimamia halmashauri zetu kutoa mikopo ya asilimia 10 lakini kuelekeza kwenye miradi ya kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasimama hapa kuushukuru uongozi wa Mkoa wa Pwani Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wote mkoa wetu umetoa zaidi ya shilingi bilioni tisa, lakini kwa mwaka huu wa fedha zaidi ya shilingi bilioni tatu Mheshimiwa Gwajima ulikuja katika Mkoa wetu umeona namna gani pia tumejipanga kwenye majukwaa ya uwezeshaji. Tunayo majukwaa 1,700 tumeshayasajili, tunaelekea kuunda kiwanda tunaelekea kutoa mchango kwenye jukwaa la uwezeshaji wa wanawake kiuchumi kitaifa; na jitihada zote zimechangiwa na kiongozi wetu mahiri Katibu Tawala wa Mkoa Engineer Mwanaasha. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwapa nafasi wanawake mahiri wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala na Wakurugenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi wawakilishi wa wanawake katika maeneo mbalimbali tunaona kazi zao, tunatembelea miradi, tunaona namna wanavyochakarika. Kwa hiyo, naomba huu mwongozo unaoandaliwa wa namna ya kuzisajili hayo majukwaa uendelee, tuna matumaini makubwa kutokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi na fursa anazozitafuta Mheshimiwa Rais wanawake wamejipanga vizuri kuzisubiri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli kama kuna wakati wamepata ari zaidi ni wakati huu ambapo pia Mheshimiwa Rais mwenyewe Mama Samia anaongoza kwa mfano, na ndio maana amekuwa miongoni mwa watu 100 wenye ushawishi hapa duniani na tumeona kazi yake ambayo imepitia katika ushawishi wake kukubalika katika siasa za Kimataifa, siasa za ndani ya nchi, maridhiano na kazi inayoendelea.

Kwa hiyo, nimalizie kwa kuwashukuru sana Wizara hii tunakuomba Mheshimiwa Gwajima tumekuona unapambana na panya road, Wizara yako ni mtambuka tunakuombea upate watumishi wengi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru Naibu Waziri na Katibu Mkuu lakini pia suala la wamachinga mnavyolisimamia na ujenzi wa masoko mahususi haya. Tunaipongeza Mkoa wa Dodoma na mikoa yote mingine Mwanza, Mbeya, Dar es Salaam namna ambavyo wanawapanga wamachinga, na tunawaomba wamachinga hususani wamachinga wa kike muwe na imani na Serikali hii inajipanga ili muweze kukaa maeneo mazuri.... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele imeshagongwa Mheshimiwa Subira, ahsante sana.

MHE. SUBIRA K. MGALU: ... kutoa mchango wenu.

Mheshimiwa Spika, naomba kushukuru naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)