Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Amina Daud Hassan

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MHE. AMINA DAUD HASSAN: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi nichangie katika hoja ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.

Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uwezo wa kuweza kusimama katika Bunge lako hili tukufu ikiwa ni mara yangu ya kwanza nikiwa na afya njema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ambayo anaifanya katika Taifa letu. Vilevile nimpongeze Waziri na Naibu wake pamoja na watendaji wake kwa kazi nzuri wanayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na mimi nichangie kuhusu ukatili wa watoto mitandaoni; tumeona mara nyingi video za utupu zikisambazwa katika mitandao ya kijamii na matukio mbalimbali ya video na ngono za watoto na wanawake zikisambazwa katika mitandao ya kijamii kwa makusudi kabisa. Udhalilishaji huu unaleta madhara ya kisaikolojia na kusababisha hata kifo au kupoteza mwelekeo wa maisha katika jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukatili huu wa wanawake na watoto unaonekana kuathiri makuzi na mila za desturi zetu za jamii ya Kitanzania. Udhalilishaji huu umeonekana ni fimbo ya kuwapigia wanawake pindi wanapoomba ajira au nyadhifa fulani kwa makusudi au kwa wivu au kwa wivu wa mapenzi. Kwa mfano, baadhi ya wasanii, wanamuziki na maigizo wanawake hapa nchini hudhalilishwa katika mitandao yao ya kijamii wao wenyewe, haya ni matukio yasiyo ya kawaida.

Ninaiomba Serikali iangalie vizuri na iweke sheria kali kwa wale ambao wanahusiana na kadhia hii. Natoa wito kwa Serikali na asasi za kiraia kuzungumzia madhara na vitendo kama hivi vya ukatili wa kijinsia na kutoa elimu hasa katika kizazi cha sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie kuhusu wamachinga; naipongeza Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwamba kwa kulitambua kundi hili la wamachinga kwamba ni wafanyabiashara wadogowadogo ambao ndio wanaoleta pato katika Taifa letu. Sambamba na hilo nampongeza sana Rais kwamba wamachinga wawekewe maeneo rafiki ili waweze kufanya biashara zao bila ya kubughudhiwa na mtu yeyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa dhamira yake na makusudi na mapenzi yake kwa Watanzania kwamba ameamua kutoa shilingi milioni 10 kwa kila Mkoa ili waweze kuwaendeleza wamachinga ambao ni wafanyabiashara wadogo wadogo kati yao na wanawake humo wamo, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)