Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Prof. Shukrani Elisha Manya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia katika hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, na cha kwanza kabisa niweze kumpogeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi ambavyo aliona vema kuweza kuunda tena Wizara hii kwa sababu Wizara hii inashughulikia mambo mtambuka, lakini ni kweli kwamba inashughulikia ustawi wa jamii yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ustawi wa jamii yetu una uhusiano mkubwa sana na ustawi wa mama na mtoto; na mimi asubuhi ya leo ningependa kukita mchango wangu juu ya lengo la Wizara ambalo linasema kuendelea kuimarisha huduma za ustawi wa jamii na haki kwa familia na watoto, ikiwemo malezi ya kambo na kuasili, watu, walezi wa kuaminika, malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto, ulinzi na usalama kwa watoto dhidi ya vitendo vya ukatili pamoja na huduma za utengamao katika familia.

Mheshimiwa Spika, na ni kwa nini niulete mchango wangu kuhusiana na hili lengo?

Mheshimiwa Spika, mimi napenda kuamini kwamba changamoto katika jamii tunaweza tukawa tunaangalia ukatili unaokuja kutokea baadae, lakini chanzo cha mambo yote haya tungetambua kwamba yanaanza katika familia. Na kwa jinsi hiyo malezi ya mtoto, elimu ya malezi ya mtoto inapaswa kutolewa katika jamii yetu tangu wazo la kutaka kuwa na mtoto linapotungwa katika mawazo ya wenzi wanaotarajiwa; na ni kwa sababu mapungufu ya elimu hii ndio chanzo cha kupata hata watoto ambao baadae tunakuja kuwaita watoto wanaokaa katika mazingira magumu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Wizara inapotengeneza sera kwa sababu najua ni Wizara mpya, lazima ione umuhimu wa kufikisha elimu hii kwa jamii nzima ili kwamba jamii sasa iweze kujua kwamba, tunapokuwa tunatarajia kupata watoto maana yake tunaambatana na wajibu. Na jamii ifikie mahali itambua kwamba wajibu wa malezi ya watoto ni wajibu usiohamishika na hasa watoto wanapokuwa miaka zero mpaka miaka 11, ni wajibu usiohamishika. Maana mara nyingi pia unakuta katika jamii yetu tunapenda kuamini kwamba mtoto atazaliwa, atapelekwa kwa ndugu yake fulani, hapana, this is non transferable responsibility. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na kama ni non-transferable, elimu hii inapaswa kuwaendea watu wote wanaotarajia kuwa na watoto hapo mbeleni, maana yake baba na mama; na wajibu huu, mimi ningependekeza hata mimba inapokuwa imetungwa na kama binti anapaswa kwenda kliniki basi na yule baba naye aende kliniki akapate elimu hii asisingizie kwamba, ni majukumu, hapana. Kama anafanya kazi mahali pa kazi, waajiri watoe ruhusa baba waende kliniki wakapate elimu ya malezi ya watoto. Na kwa sababu gani nasema hivi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati mwingine kama Taifa tumeongelea hali ya udumavu. Hali ya udumavu inatokana na kutokuwa na lishe bora wakati wa mimba. Sasa unakuja baadae kuhangaika, elimu ya msingi, elimu ya awali, sijui tuition, tuition itafanya nini kama mtoto alidumaa wakati wa mimba? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, habari ya lishe bora lazima iwe ni elimu ambayo itapelekwa kwa watu wote wahusika. Na mimi kwa kuongelea habari ya non transferable kama jukumu la malezi, hata inapofikia kuongea habari ya elimu tunayoitoa, hivi kuna sababu ya mtoto wa miaka sita kwenda boarding? Akalelewe na nani? Na matron na hao.

Mheshimiwa Spika, sasa tunakuta kwamba tunshindwa kujenga bond kati ya baba na mama mhusika anakwenda kujenga bond na matron, anakwenda kujenga bond na mtu ambaye hamfahamu. Kwa hiyo, unakuta hata mtoto anapokua hana bond na wazazi wake, lakini tuko hapa kwenye mitaala yetu ya elimu tunapendekeza shule za boarding za watoto wadogo, si sawa, si sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunapokuwa tunajadili msingi wa ustawi wa jamii mimi napendekeza ndani ya Bunge lako tukufu, nimesema sentensi ambayo nitairudia tena; wajibu wa malezi yam toto mchanga kwa wazazi wake is non transferable, na kama ni non transferable maana yake si matron wa chekechea au wa shule ya awali ambaye ana jukumu la kulea mtoto wako. Na kwa msingi huo tujadili kama kweli ni sahihi kuwa na shule za kulea watoto katika umri ule mdogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, elimu hii ikifikishwa napendekeza ifikishwe kwa namna zote, sasa hivi njia za kidijitali yawezekana ni za msingi sana kupeleka elimu hii. Kwa hiyo, Wizara iweke sera itakayohakikisha kwamba elimu hii inawafikia Watanzania wote ili tuweze kuwa na jamii ambayo ina ustawi.

Mheshimiwa Spika, ninaelewa muda wangu si mrefu sana niongelee jambo la mwisho katika ustawi wa jamii yetu. Ni kweli kwamba tunapenda burudani, sasa ninamfikiria mtoto mdogo aliyezaliwa yuko mahali fulani nyumbani, halafu katika jamii hiyo kuna club kubwa inayopiga muziki mdundo wake mpaka saa nane usiku na kuna mtoto mdogo hapa ambaye ngoma zake za masikio sidhani kama zinaweza kuhimili huo muziki. Lakini watoto wako majumbani, kuna wazee wenye pressure majumbani, kuna wazee ambao wanatamani utulivu lakini ngoma inadunda mpaka saa nane usiku, inasambaa kilometa tano kutoka ukumbi wa mahali ilipo, si sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nikutolee tu mfano unatoka hapa Dodoma unakwenda Mbeya unakwenda kwa ajili ya kuhudumia wananchi wako, halafu usiku huo unaofika umefika saa nne usiku unatamani uwe na masaa manane ya kulala, halafu ngoma inarindima usiku mzima, kesho utakuwa tayari kwa ajili ya kazi, hapana. (Makofi)

Kwa hiyo, ili tuweze kuwa na ustawi wa jamii teknolojia ya kuzuia muziki ipo, burudani tunaipenda ni kweli, lakini ikomee masaa ambayo jamii inapohitaji ustawi wa afya ya akili kama balozi anavyosema watu wapumzike ili tuweze kuwa kesho yake kutayarishwa kwa ajili ya kufanyakazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo napendekeza tunapoongelea ustawi wa jamii yetu pia hebu watoa burudani watuburudishe tunapenda, lakini watuachie muda tupumzike sisi, wazee, wenye pressure na watoto wetu wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)