Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Husna Juma Sekiboko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa fursa na mimi kuchangia bajeti hii lakini awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa busara na maamuzi magumu aliyoyafanya kuiweka sekta hii kwenye Wizara kamili, ni jambo kubwa sana na ni jambo la kupongezwa.

Mheshimiwa Spika, mpaka Mheshimiwa Rais anafanya maamuzi ya kusimamisha Wizara hii kuwa Wizara kamili ameangalia mambo mengi, ameona nchi yetu inahitaji ustawi wa hali ya juu na tukiangalia kwenye mazingira yetu tunapotoka tunaona sehemu kubwa ya changamoto zinazokabili Taifa letu ni maendeleo ya Jamii, nataka niseme jambo moja kuna usemi kwamba siasa hapo ulipo; politics is local. Siasa ya nchi yetu locality yetu, changamoto zetu ni changamoto za mwanamke na mtoto wa kike, hizo ndizo changamoto kubwa ambazo tunaza Tanzania na nitasema kwa nini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu na wachangiaji wengi hapa wamezungumzia masuala ya ukatili wa kijinsia wamezungumzia namna ambavyo watoto wetu wananyanyasika kwenye maeneo mbalimbali, lakini nataka niseme ukweli watoto wengi wanaopata hayo manyanyaso ni watoto wa maskini, sijaona mtoto wa tajiri au pengine sio wengi ambao wanapitia kwenye hayo manyanyaso na hii ni sababu ya umasikini. Kama tunataka kutatua changamoto ya unyanyasaji wa kijinsia, ukatili wa aina yoyote, jambo la kwanza kabisa ni kuziimarisha familia zetu kiuchumi. Leo tunazungumzia suala la kusimamisha mawakili kwenye Halmashauri kwenye Idara ya Maendeleo ya Jamii ili kumsaidia mwanamke anapolia na mirathi apate msaada wa kisheria, mtoto wake anapobakwa apate msaada wa kisheria, lakini hii ni nini ni kwa sababu familia zetu nyingi ni maskini, wenye uwezo wa kusimamisha mawakili watetezi, wanasheria kwenye mahakama zetu ni wale ambao wana uwezo wa kifedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nini niishauri Serikali; kwenye Halmashauri zetu tuna asilimia 10 tuliyotenga kwa ajili ya kukopesha vijana, kinamama na watu wenye ulemavu, lakini hile fedha haitoshi, niiombe sana Serikali na niiombe Wizara hii, iangalie namna nzuri ya kuweza kuweka mikopo ya akinamama na hususani akinamama kwenye Halmashauri zetu ili familia zetu ziweze kuimarisha kiuchumi, waweze kusimamia vizuri malezi kwenye familia zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, malezi na mmomonyoko wa maadili kwa namna nyingi na kwa maeneo mengi umesababishwa na akinamama na akinababa kuhemea mpaka usiku wa manane kuwaacha watoto peke yao, watoto wengi ambao unaambiwa wameenda kulelewa na familia nyingine na baba mkubwa na shangazi ni wale ambao unakuta kwenye familia baba, mama ameenda kuhemea anashinda shambani, anarudi usiku, baba anaenda kutafuta anarudi usiku, muda wa kuzungumza na watoto kwenye familia hakuna wote wanakwenda kuhemea. Sasa namna nzuri ni kuimarisha hizi familia kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano Wilaya ya Lushoto, Wilaya ya Kilindi, Wilaya ya Handeni ni Wilaya ambazo zipo pembezoni Wilaya hizi makusanyo yake hayafiki hata shilingi bilioni 1.5 kwa mwaka, mapato ya ndani ukisema hata utenge asilimia 10 haifiki hata shilingi bilioni moja kwa mwaka, lakini akinamama ni wengi, nini sasa kifanyike maana yake Serikali i-subsidize hiyo ten percent, iongozee kwenye zile Wilaya za pembeni kuwawezesha akinamama wengi zaidi kuweza kupata mikopo ya bei nafuu na hili liendane sambamba tumekuwa na wimbo wa muda mrefu wa Benki ya Wanawake Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mpaka tunavyozungumza sasa hatujaona effectiveness ya hiyo Benki ya Wanawake Tanzania imewakopesha akinamama vijijini huko wangapi, imewawezesha kubadiisha maisha ya akinamama wangapi, hii bado halijaleta tija ningeomba sana ningeishauri Wizara hii iangalie namna nzuri ya kutenga fungu maalum kwa ajili ya kuwakopesha akinamama hasa akinamama maskini ambao wapo Wilaya maskini ambazo zipo pembezoni ambapo mapato yao hayafanani kama Wilaya za mjini, halmashauri zao zina mapato madogo ambayo ukitenga hiyo ten percent haiwasaidii akinamama kuwainua kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna jambo la dawati la kijinsia na mwaka jana niliuliza swali la msingi humu ndani, kuna sababu gani lile dawati la kijinsia kukaa polisi? Familia zetu tunafahamiana akinamama na Watoto wengi wanaogopa kwenda kwenye vituo vya polisi, dawati lile lingesogezwa kwenye huduma ya maendeleo ya jamii, kwenye ustawi wa jamii, hospitali matukio mengi yangeripotiwa na tungepata namna nzuri ya kushughulikia hayo matukio na mwisho wa siku jamii yetu ingestaarabika.

Mheshimiwa Spika, kwa ajili ya muda naunga mkono hoja, nashukuru sana. (Makofi)