Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Jumanne Kibera Kishimba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kahama Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi kuchangia kwenye Wizara hii ambayo ni mpya kwetu. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri hasa kwa dawati la jinsia ambalo linasaidia sana hasa majimbo yetu ambayo yana watu wengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala sasa hivi linatutatiza sana hasa vijijini na sielewi kama suala hili ni sheria au ni utaratibu na uzuri Mheshimiwa Waziri alikuwa Waziri wa Afya kwa muda mrefu kidogo. Suala hili linaleta mgongano sana hasa kwenye jamii zetu za kienyeji, suala la kwenda na kinamama wajawazito na wanaume zao kliniki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unaposema mtu wa kijijini aende na mke wake kliniki unaleta taharuki kubwa sana kwa sababu kwa mila zetu na kwa dini zingine unaruhusiwa kuoa wanawake mpaka wanne na huwezi kuwaoa kwa wakati mmoja. Sasa kama mtoto wako wa kwanza wa mke wa kwanza ana mimba na huyu wa kiume naye mke wake ana mimba na mke wako mdogo ana mimba; je, mtakwenda wote kliniki na siku ya kliniki ni siku moja tu kwa wiki itawezekana? Lakini kwa mila zetu mimba kwetu siyo ugonjwa, ila inapokuwa limetokea tatizo ambalo ni mara chache sana na hata mimba ukiwa unamsalimia mtu mjamzito kawaida huwa tunamuuliza tu vipi mwenye mzigo ameutua au bado? Anasema bado hajatua mzigo, siyo ugonjwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa pole pole inaanza kuwa kero, kule kwangu Kahama yamewekwa mabango ya watu kukodisha wanaume wa kwenda nao kliniki kwa sababu wanaume wanakataa na je, sheria hiyo ni sheria model gani? Wewe ni mwanasheria, anayeenda kuadhibiwa pale hospitali ni yule mwanamke, lakini atatakiwa aje na mume sasa mwenye kosa ni mwanaume aliyekataa na kwa mila za kwetu mtu anakataa anasema mbona hii kitu sisi hatutaki anayeteseka ni mwanamke, matokeo yake inasababisha mpaka vifo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu huyu mama hana uwezo wowote wa kujieleza, tuelewe watu wetu tunaowaongoza ni watu wa hali ya chini sana, tunapopewa utaratibu na wazungu lazima tuwe tunauliza wazungu jamani hiki kitu unakipeleka kule Afrika na hasa kwetu Tanzania wataweza watu wetu wa kule kijijini kufanya hiki kitu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, humu ndani kuna Wabunge akinamama na wengine ni wajawazito, ukimuuliza tu humu ndani kwamba hii mimba shemeji ni nani hamsalimiani mwezi. (Makofi/Kicheko)

Sasa watunga sheria hawataki kuitekeleza, tena unamuuliza tu na ninajua kama ingekuwa wanafanya hivyo Wabunge tungeona wamejirusha kwenye WhatsApp sijaona hata siku moja Mbunge mjamzito amejirusha kwenye WhatsApp akiwa kwenye bench la kliniki na mumewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri inawezekana ni sababu kubwa pia inayosababisha kuwepo kwa mlundikano wa kesi kwenye dawati la jamii, maana yake unapokodishiwa mke na jina anaenda kuandika yule mume, je, ikitokea yule mtoto akazaliwa yule mume aliyekuwa anampeleka mke akamkatalia mtoto, utafanyaje? Haitawezekana, tumuombe Mheshimiwa Waziri alitizame kwa makini sana hili suala linasumbua mno.

Mheshimiwa Spika, suala lingine tumesema kujifungua akinamama ni bure, lakini ukweli siyo bure, sasa hivi imezuka kama iliyokuwa kwenye shule imehamia hospitali, anaambiwa aje na vitenge pair saba, aje na beseni, aje na gloves, anaambiwa vitu vingi sana. Kwa hali ya sasa ya maisha ya kijijini na hali ya watu wetu ni sahihi kweli na je, watoto wa sasa hivi ndiyo wamebadilika? Ni kitu gani kimetokea hapa katikati ambacho mtoto wa sasa hivi anahitaji vitu vingi namna hiyo na uzuri Mheshimiwa Waziri yeye ni daktari, ajaribu kutueleza kimetokea kitu gani hapa katikati maana yake akifika pale hospitali kama hana vile vitenge, aidha, atoe rushwa au aambiwe kanunue vitenge kwenye eneo lile, lakini kitenge kipya kinaweza kubeba mtoto mchanga kweli? Haiwezekani, ni lazima iwe nguo iliyotumika.

Kwa hiyo, tumuombe Mheshimiwa Waziri aliangalie sana hilo suala kwa sababu linatupa wakati mgumu sana na hasa sisi kwenye majimbo ambayo yana watu wengi sana kwa ajili ya shughuli za migodi na ukulima na ufugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpaka miaka ya 1985 wagonjwa walikuwa wananywea dawa hospitali, ilikuwa mtu hawezi kupewa vidogo ili aende akanywe nyumbani na wakati ule hospitali zilikuwa mbali mbali na barabara hazikuwepo, pikipiki hazikuwepo, teknolojia haikuwa hiyo, lakini kwa utafiti hata ukiangalia leo asilimia 70 au 60 ya dawa watu hawamalizi dozi wanakunywa, wakipona wanaziacha mle ndani, kwa nini Serikali isirudishe utaratibu wa zamani ili wagonjwa wa vijijini wakanywee dawa hospitali ili kusudi inawezekana dawa nyingi tunapoteza bure na tunakataa kuwatibu watu bure. Kwa sababu mimi ninafahamu mtu mpaka leo anaweka alarm kwenye simu ya kujikumbusha kunywa dawa hasa wagonjwa wale ambao ni wa kisukari au pressure, lakini wagonjwa wengine baada ya kuwa wamepona hasa kijijini mgonjwa anapimwa kwa kuweza kunywa uji, ukinywa uji tu ukamaliza au ukala wanakwambia twende shambani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwa hiyo, madawa mengi yanashinda tu kule ndani, kwanini sasa Serikali isiruhusu watu wakanywee dawa hospitali ili mimi kama nimeandikiwa sindano tano, mimi ni mtu wa kijijini nikichomwa mbili nikaona nimepona, mimi siendi, maana yake hata ukinipa dozi nyumbani kwani wewe unakuja kunithibitishia mimi kama nazimaliza, hakuna mtu anayenifuata kama nimemaliza dawa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tungemuomba kwa kuwa sasa zahanati ni ni nyingi na barabara ni nzuri na ni kila kijiji turudishe huo utaratibu kwa sababu pia utatuondolea mgogoro wa dawa fake na kama dawa zitanywewa pale hospitali sidhani tena kama kutakuwa na kesi ya dawa fake na itakuwa vizuri zaidi kwa sababu ukweli kabisa wote tunafahamu kwamba dawa nyingi sana zinabaki majumbani hasa huu tumepita muda wa corona mtu ananunua dawa hii akinywa vitatu, amepona typhoid mpaka inadawa 50 lakini mtu anakunywa nusu siku ya tatu anaachana nazo, kwa hiyo, zipo tu ndani. Kwa hiyo, inaweza ikaisaidia hata Serikali pia kupunguza baadhi ya gharama bila sababu yoyote.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa kumalizia tu nimuombe Mheshimiwa Waziri aliangalie hili suala kama labda tulijaribie kwenye maeneo ya ndugu zetu labda Tanga na Pwani ili wao waruhusiwe kwenda na wake zao, lakini sisi kule ni ngumu, huwezi kuwa unatoka kulima, utoke kulima na siku ya kliniki ni moja, je, nani atalinda mpunga shambani haitawezekana, maana hamuwezi kwenda wote kliniki mkapangane kweli kwenye fomu wewe na watoto wako na mkwe wako, mpangane hapo kweli na nguo zenyewe za shida aangalie tu kama mimba ina tatizo aniite mimi mwanaume ili mimi niende siku hiyo kwa special maana yake haiwezekani mimba zote zina matatizo. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)