Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ASYA SHARIF OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza nichukue nafasi hii nikushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii ya mara ya pili kusema tunakupongeza wewe binafsi kwa namna unavyoliendesha Bunge hili tukufu, tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kukulinda na tunasema tupo pamoja na wewe, mwanamke anaweza na ndiyo maana ukaweza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani hizo, mimi nianze kuchangia na kuchangia nianze kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu lakini na Rais wetu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi kwa namna wanavyoendelea kutuongoza katika nchi hii katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo, kiuchumi, kijamii na kisiasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nianze kuchangia hoja yangu kwenye wizara hii kwenye suala zima la ukatili wa wanawake na suala la uzalilishaji wa kijinsia wakiwemo watoto.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba wanawake wengi wanakabiliwa na suala la udhalilishaji wa kijinsia ikiwemo ukatili na ukatili huu ambao wanapata wanawake wengi ikiwemo kutekelezwa na familia, na hii hutokea pale baadhi ya wanaume wanaposahau wajibu wao wakawaacha wanawake hawa na mzigo wa watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wanawake hawa wengi wanapatwa na vilema kutokana na ukatili unaoendelea kwa baadhi ya maeneo katika nchi yetu. Wanawake hawa pia wananyang’anywa mali ambazo wamezichuma pamoja na mwanaume ambaye walifunga ndoa. Kufuatia hali hii mimi nina ushauri wangu kwa Wizara husika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza naiomba Serikali kuwajengea uwezo wanawake hawa kielimu ya uthubutu ili wanawake hawa sasa waweze kuvunja ukimya. Wanawake wengi wamekuwa kimya sana, wamekuwa wanaogopa. Sasa kuogopa kwao hii inapelekea wanapata maumivu makali ya kunyanyaswa bila ya sababu ya msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali kupitia Wizara hii kuwachukulia hatua wale wote ambao wanahusika na udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto. Ni dhahiri kwamba wanawake wanateseka kwa kulea watoto peke yao, lakini inapelekea kuwa na ongezeko kubwa la watoto mtaani kwa sababu watoto hao wanakosa matunzo ya baba na mama na wanasahau kwamba mwanamke yule hakuweza kuzaa peke yake, alizaa kwa ushirikiano na baba. Lakini leo cha kushangaza sijui inakuwaje mwanamke huyu anatekelezwa na watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niiombe sana Serikali impe nguvu mwanamke anapofika kwenye vyombo vya maamuzi ili kuweza kupata haki ya kuwatunza Watoto, lakini pia kuendelea kufurahia maisha yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasema kwamba wakati umefika wa wale wote wanaozalilisha watoto na kuwatumikisha wakiwa na umri mdogo kufunguliwa kesi maalum. Kuna wimbi kubwa la baadhi ya watu kuwaajiri Watoto au niseme ajira za watoto. Hili wimbi ni kubwa sana, hata hapa Dodoma tumejionea baadhi ya maeneo kuna watu wanawaajiri, tukiwauliza anakwambia mama ndiyo amenipeleka kule mimi nifanye kazi za majumbani. Kiubinadamu haielekei, mtoto ana miaka 12/13/14 mtoto wa mwenzio unakwenda kumtuma, hasomi. Hivi kweli kama ni wa kwake angefanya hayo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naiomba sana Wizara husika jambo hili msilifumbie macho, mlichukulie hatua kwa sababu ni jambo lipo na linaathiri nguvu kazi. Lakini naendelea kusema watoto wana haki ya kuishi, watoto wana haki ya kusoma, watoto wana haki ya kusikilizwa, watoto wana haki ya kucheza. Lakini yote haya leo hawayapati, baadhi yao hawayapati; na hawayapati kwa sababu watu wamekosa imani, lakini watu wanajaribu. Naamini Serikali yetu sisi iko imara na uwezo uko wa kuweza kushughulikia watu wa aina hii ili wasiweze kutuharibia Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo kabla sijaunga mkono hoja. Nasema kwamba, naomba nimnukuu Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu kwa kauli yake ambayo ameisema hivi karibuni kwamba; “sasa umefika wakati tupaze sauti zetu kila mtu kwa nafasi yake, alipo popote kuhakikisha kwamba tunapinga vitendo hivi vya ukatili wa kijinsia....” (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Malizia Mheshimiwa sekunde 30.
MHE. ASYA SHARIF OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)