Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia Wizara ya Wanawake, Jinsia, Wazee na Watoto. Kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu. Mheshimiwa Rais wetu amechukua kwa namna ya kipekee ndani ya Taifa letu kuangalia kwa namna na jicho la kipekee wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia niwapongeze walioteuliwa kupewa nafasi hii, muda bado tunao, tutawapa pongezi za ufanyaji kazi nafikiri baada ya miaka miwili au mitatu, kwa sasa tuwapongeze kwa kuteuliwa. Lakini pia tukiwa kama wenzenu tuna imani kubwa kwamba mtafanya kazi vizuri na tunaamini kwamba tutafika pale ambapo Mheshimiwa Rais anatarajia tufike. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze na suala la ubakaji; leo takribani Wabunge wako wote waliosimama hususan wanawake wamezungumzia suala la ubakaji. Ndani ya Taifa letu suala la ubakaji limekuwa suala la simanzi na kilio hususan kwa akinamama. Tunafika wakati wanawake tunaulizana maswali, hivi kinababa hawatusikii, hawaoni, hawajui au kwao wanaona ni jambo la kawaida? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tulitegemea kuona Wabunge wanaume wakiungana nasi katika suala zima la kulizungumzia suala la ubakaji, na nilitegemea hili kwa sababu suala zima la ubakaji watoto wanaobakwa wamo ndani ya majimbo yao. Hili kwao limekuwa la Viti Maalum na wakati suala la ubakaji ni kwa Taifa zima na wanaobakwa ni watoto wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Tanzania Bara kuna mwenzangu mmoja alizungumza akasema takribani sasa imekuwa tukio kila wiki la suala la ubakaji. Kwetu sisi Zanzibar si mambo hayo, imekuwa takribani kila siku kuna suala la ubakaji. Tumeamua sasa Wabunge tupaze sauti zetu, tunaamini, tuishauri Serikali yetu kwa namna ya kipekee Mheshimiwa Waziri liangalieni. Wakati unamuomba Mheshimiwa Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi atengeneze pacha wako hakusita, haikuzidi siku mbili au siku tatu kwa upande wa Zanzibar naye Mheshimiwa Rais alitupatia Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mategemeo yetu hasa sisi tunaotoka Zanzibar utafanya kazi na Waziri wa Zanzibar kuangalia changamoto iliyoikabili Tanzania yetu hususan kwenye suala la ubakaji na unyanyasaji. Wanawake wamekuwa na matatizo makubwa kila unapopita ndani ya nchi hii. Kila unapokwenda suala ni moja tu, sisi tukiwa kama viongozi tunaowakilisha mikoa yetu, huna unapokwenda kukanyaga ukafanya mkutano usikute wanawake wanalia wanasema ubakaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hakuna ajenda tunayoweza kwenda kuizungumza nje. Unapokwenda kuzungumza suala ni moja tu Mheshimiwa Waziri ni ubakaji, tushirikiane tuone tunatatua vipi tatizo hili. Kuna mambo mengine mazuri, tunaweza tukawa nayo huku kwa upande wa Tanzania Bara tukayapeleka Zanzibar yakafanyiwa kazi kutatua tatizo, lakini kuna upande wa Zanzibar yakaletwa huku. Zanzibar kuna eneo la Pemba, kuna eneo la Mkoani kuna eneo kwa ajili ya suala hili wameweka mkakati kunaitwa mkono kwa mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mkono kwa mkono kwamba lile tatizo linatatuliwa askari polisi yuko hapo hapo, yuko daktari, akitoka kwa daktari mtoto anaingia kwa askari na tatizo linatatuliwa. Takribani tatizo hili kusuasua kwake hasa ni kwenye kupoteza ushahidi. Mtoto anavyofanyiwa tukio lile, anapochukuliwa kwenda kupelekwa kituoni, akirudishwa kwa daktari ushahidi umepotea. Hayo Mheshimiwa Waziri mnaweza kuyachukua na kuona tunawezaje kuendelea kuboresha kuona kazi tunaweza kuzifanya vipi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini suala la unyanyasaji; takribani kila mwanamke leo aliyesimama Mbunge kazungumzia suala la mirathi, suala la haki ya mwanamke anayoipata. Ingawa suala hili pia lipo katika kisheria na kwa upande wa dini pia. lakini Mheshimiwa Waziri angalia maeneo mahususi, mama amewapa nafasi amejua mtamshika mkono, mtampa nguvu. Tuangalie kama wanawake masuala haya tunayatatua vipi. Pamoja na ugumu uliokuwemo ndani ya mila zetu, ndani ya dini zetu, ndani ya tamaduni zetu lakini bado tuna fursa ya kuwasaidia wanawake wa Tanzania ili haya mambo yaende kwa utaratibu, yaende kwa haki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri kuna mfuko wa asilimia 10; mfuko wa asilimia 10 ni kwa wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum. Mheshimiwa Waziri fedha zipo, sisi tumo kwenye Kamati ya LAAC fedha tunaziona. Kuna halmashauri ziko Tanzania hii hii zimekusanya mamilioni ya pesa, vijana waliokuwepo maeneo yao hawajui kama kuna huo mfuko. Mheshimiwa Waziri tunaishauri Wizara yako ijikite kwenye kuwaelimisha wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, inawezekana vijana wengi na wanawake wanakosa fursa kwa sababu hawazielewi hizo fedha. Waliokuwepo ndani ya halmashauri zetu wamezikalia hawazizungumzi, hawatoi elimu, hawatoki kwenda kuwaambia watu kwamba fedha zipo, Serikari ina pesa inaweza kuwakopesha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwanamke mwenzetu, Mheshimiwa Waziri lichukue, unapokwenda kwenye mikutano yazungumzeni, halmashauri ina fedha kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum. Fanya tathmini ukutane na Waziri wa TAMISEMI, angalia kila halmashauri ina shilingi ngapi? Kuna fedha zimelimbikizana miaka mitatu, minne, mitano hazijaenda kwa walengwa. Tatizo ni mipango iliyokuwepo ndani ya halmashauri yetu ni mipango mibovu ndio maana zinashindwa kufanyiwa kazi ipasavyo. Mheshimiwa Waziri kwa kuwa tunaamini uwezo wako wa kufanya kazi hatuna mashaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine kuna nyumba za kulelea wazee. Si jambo baya, muda huu tunamuda mkubwa wa kukushauri, muda huu tuliokuwa nao wa kukushauri ili tuweze kuona Wizara yetu inafanya kazi vizuri. Kuna nyumba za kulelea wazee, kuna mtu hapa alitutolea mfano kusema kwamba Zanzibar zipo, kweli Zanzibar ipo, na mara nyingi nilikaa nikajaribu kuangalia kwa upande wa Tanzania…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)