Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu kwa ajili ya maendeleo ya wanawake. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anazozifanya na kuona umuhimu wa kuwa na Wizara hii ya wanawake na makundi maalum ambayo uwepo wake imesaidia sana kutatua kero na changamoto za wanawake ambao ndiyo walezi wa familia na jamii kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, dada yangu Dorothy Gwajima, Naibu wake Mwanaidi Ali, Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote kwa kazi nzuri wanayoifanya kuhakikisha wanatatua changamoto za makundi maalum, nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo ambalo napenda kulichangia ni Maafisa Maendeleo Jamii na uwezeshwaji wa wanawake kiuchumi; Maafisa Maendeleo Jamii ni watu muhimu sana katika jamii na napenda niseme kwamba ni changes agency ambao wanabadilisha mindsets katika jamii, lakini wamekuwa wakisahaulika sana, Serikali imekuwa haiwapi kipaumbele. Wamekuwa wakifanya kazi kwenye mazingira ambayo siyo rafiki, lakini pia hawana vitendea kazi na nyenzo nyingine muhimu za kuwasaidia kufanikisha majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kumekuwepo na matukio mbalimbali ya ubakaji kwa watoto wa kike lakini pia ulawiti kwa watoto wa kiume na vitendo vingine ambavyo kwa kweli havipendezi sana katika jamii yetu. Endapo viongozi hawa, Maafisa Maendeleo Jamii hawa wangeweza kuwezeshwa vizuri vitendea kazi na nyenzo nyingine muhimu kama ambavyo Maafisa Ugani wameweza kuwezeshwa pikipiki na vitendea kazi vingine wangeweza kufanya kazi kwa ufanisi na kuweza kuyafikia makundi mengi sana katika jamii, kuwapa elimu juu ya lishe bora, malezi bora lakini pia kuwapa elimu juu ya jambo hili muhimu ambalo liko mbele yetu sensa na makazi ya watu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niishauri Serikali iwaangalie sana Maafisa Maendeleo Jamii hawa, kama wenzangu walivyotangulia kusema ni watu ambao wanagusa karibia kila sekta, wakiwezeshwa wataweza kuyafikia makundi mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, lakini pia katika Mkoa wangu wa Singida kuna uhaba mkubwa sana wa Maafisa Maendeleo Jamii hususan katika Kata, wale Maafisa Maendeleo Jamii ambao wako Wilayani kutokana na jiografia ya Mkoa wa Singida hawawezi kufika kila sehemu. Maeneo ambayo wanaweza kufika ni maeneo machache sana. Lakini endapo kutakuwa na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika kila kata wataweza kuielimisha jamii na vitendo hivi mfano vya ukatili wa kijinsia ukiwepo wa kubaka watoto, ulawiti wa watoto wa kiume, mmomonyoko wa maadili, wataweza kuielimisha jamii na mambo hayo yataweza kupungua sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo napenda kulichangia ni uwezeshwaji wa wanawake kiuchumi; ni ukweli usiopingika, ukimwezesha mwanamke umeiwezesha jamii. Lakini ipo mikopo ambayo inatolewa katika halmashauri, mikopo ya asilimia 10; wenzangu wametangulia kusema, mikopo hii haitoshi kabisa, lakini pia imekuwa ni mikopo ambayo haina tija. Mfano kikundi kina watu 15, wanapewa kiasi cha shilingi milioni tatu, wanaishia kugawana laki mbili, mbili. Hapo tija iko wapi? hakuna tija yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikari ni vyema sasa kuiangalia na kuitathimini mikopo hii na kuangalia njia bora zaidi za kuweza angalau kuwapa mradi. Mfano mradi wa kufuga kuku au mradi wa kulima mbogamboga au mradi hata wa kufuga nyuki pamoja na kuwapa mafunzo. Jambo hili lingekuwa linatija sana kwa wanawake ambao hawa wanawake ndiyo walezi wa jamii na walezi wa familia lakini wamekuwa wakiangalia matibabu, wamekuwa wakilipa hata ada za watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia napenda kuishauri Serikali ni vizuri sasa kukawepo mkakati mahususi wa kuangalia namna bora zaidi, kwa sababu nimejaribu kuangalia hapa kwenye bajeti, lakini sijaona mahali popote ambapo kuna mkakati mahususi wa kupinga hivi vitendo vya ukatili wa kijinsia hususani ubakaji wa watoto wa kike ambao wamekuwa watoto innocent, hawana hatia, hawajui, wanakuwa wanaharibika kisaikolojia. Naishauri sana Serikali kuweko na mkakati wa kitaifa wa kuweza kuendesha kampeni ya kuzuia ukatili wa kijinsia.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja na nawapongeza sana viongozi wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya na nakupongeza wewe kwa kuliendesha Bunge letu vizuri. Nakushukuru. (Makofi)