Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Dr. Paulina Daniel Nahato

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi na mimi nikachangie katika Wizara hii. Awali yayote napenda kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipatia nafasi na mimi kusimama mbele kuchangia katika Wizara hii muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, mimi napenda kumshukuru sana Rais wetu mpendwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono aliyoyapata ya kuweza kuanzisha Wizara hiii. Wizara hii ni muhimu sana, Wizara hii ilipokuwa katika Wizara ya Afya ilikuwa ni kubwa mno kiasi kwamba akili yote au concentration yote ilikuwa katika masuala ya afya, lakini leo Wizara hii inajitegemea na mimi sina mashaka na Dkt. Gwajima pamoja na Naibu Waziri pamoja na timu nzima ni wachapakazi. Kwa hiyo, kwa hilo naipongeza sana wizara hii kuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la ukatili wa kijinsia limeongelewa sana kwa hisia kali na suala hili la ukatili wa kijinsia huwanyima wanaume na wanawake na watoto kufurahia haki zao za msingi ambazo kimsingi ni haki ya binadamu.

Mheshimiwa Spika, katika takwimu za Benki ya Dunia ambayo ilitolewa Aprili, 2022 imeonesha kwamba Tanzania ina asimilia 40 ya wanawake wote wameathiriwa kimwili au kijinsia na ambapo kati ya hao asilimia 14 wameathiriwa kwa kingono.

Mheshimiwa Spika, takwimu hizo hizo za Benki ya Dunia zinaonesha kwamba wanakwake wa umri kati ya miaka 15 mpaka 49 walifanyiwa ukatili huo na wenzi wao. Takwimu inaendelea kusema kwamba kwa wastani asilimia 30 ya wasichana chini ya miaka 18 walifanyiwa ukatili wa kingono.

Mheshimiwa Spika, hili suala ni zito, ukatili wa kijinsia ni jambo zito, ni jambo zito kwa sababu haliathiri tu maumbile, linaathiri hisia za wote wanaoathirika na mtu akiathirika kisaikolojia na kihisia ni rahisi sana kufanya mambo ambayo hakuyapenda kuyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aina za ukatili ambazo zinafanyika katika nchi yetu mojawapo ni ukatili wa kimwili kwa mfano mtu kupigwa au kujeruhiwa, nyingine ni ukatili wa kingono ambapo mtu huingiliwa bila ridhaa yake, inaweza ikawa ndani ya ndoa au ikawa nje ya ndoa, lakini kama hakuna ridhaa basi pia huo ni ukatili wa kingono, lakini pia kuna ukatili wa kisaikolojia, ukatili wa kisaikolojia; ni pale ambapo mtu anaumizwa kihisia na kujisikia vibaya na kutokufurahia Maisha, lakini ukatili mwingine ni ukatili utokao na mila na desturi zilizopo katika jamii zetu hizo ni kwa mfano kutokumiliki ardhi na wengi waathirika ni wanawake na nyingine ni ukeketwaji wa wanawake, nyingine ni ndoa za kulazimishwa, nyingine ni wajane katika mila mbalimbali kurithiwa lakini nyingine ni mauaji ya vikongwe wasiokuwa na hatia kwasababu mbalimbali. Lakini vilevile ni uuaji wa watu wenye ulemavu na nyingine ambayo pia ni ya ajabu ni miiko ya vyakula, kwa mfano wanaume hula chakula cha aina fulani na wanawake hawaruhusiwi kwa mfano kuku mapaja na nini wanaume ndiyo wanakula huo pia ni unyanyasaji wa kijinsia lakini vilevile hata ndoa ya mkeka pia ni unyanyasaji wa kijinsia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala kubwa linaloonekana hapa pia ambalo linachangia ni tatizo lipo ndani ya familia; ndoa zinakufungwa lakini baada ya muda panakuwa hakuna mawasiliano, baba na mama hawaongei miezi sita, mwaka watoto itakuwaje? Na hawa watoto ndiyo sisi huenda humu ndani na sisi wazazi wetu walifanya hivyo au babu zetu walifanya hivyo, baba kivyake, mama kivyake, baba anampiga mama, watoto wanaona, baba anamtukana mama watoto wanaona, watoto wanatukana, watoto wanaona, watoto hawaweze kuwapiga wazazi, mwisho wa siku watoto wanaamua kuondoka nyumbani na kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini lambo muhimu sana pia katika tafiti nyingi zimefanyika hata hawa wazazi hawajui jinsi ya kuongea na watoto wao. Hawajalelewa katika mazingira ya kuongea na watoto, hawajui waongee na watoto wapi, hawajui waongee na watoto lini, hawajui mbinu gani watumie kuongea na watoto. Watoto hawana uhuru na wazazi, watoto wamesema hawana uhuru ukiwauliza watoto wanasema ni afadhali akaongee na mwalimu na je, hata hawa walimu wameandalia. (Makofi)

Kwa hiyo hili jambo Wizara iliangalie, wazazi wapewe semina ya kutosha kuongea na watoto wao. Wazazi wanaishi na watoto wenyewe warekebishe tabia zao, lakini wawe karibu na watoto ili waongee nao. Watakapoongea na watoto watajua shida zao na mtoto atakuwa na furaha, hatokimbia nyumbani, hatoenda mitaani hata kama familia kiuchumi siyo nzuri mtoto atashiriki katika masuala ya uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kutokana na muda naomba niongee suala moja muhimu sana. Suala hili ni kuhusu hivi vituo vya kulelea watoto. Vituo viko vingi lakini naomba kuishauri Serikali, hivi vituo miongozo yake haieleweki watu wanakurupuka wanaanzisha vituo, miundombinu haijakaa vizuri, wataalam wa kutosha hawapo na hivyo unakuta wapo tu wanaanzisha vituo watoto wanalala chini, watoto mara wanakosa mlo, watoto wanapigana, watoto hivi, wataalam hakuna, na kadhalika. Hivi vituo viangaliwe, vigezo vya kutosha, checklist iwepo ili hivi vituo viwe vituo kweli vitakavyoleta watoto watakavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa ninaomba tu...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)