Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Tecla Mohamedi Ungele

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Spika, ahsante, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunipatia uhai.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nakupongeza kwa kazi kubwa unayofanya kuongoza Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuona umuhumu wa kuwa na Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. Amewateua Mawaziri Dkt. Dorothy Gwajima na msaidizi wake Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis na Katibu Mkuu Dkt. Zainabu Chaula na timu yao ingine yote mpaka kule kwenye halmashauri wanaendelea vizuri kufanya kazi kubwa, kwa kweli ni wapambanaji timu yetu hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kujikita kwenye maeneo mawili na kama si matatu; la kwanza matukio kadhaa ya unyanyasaji wa watoto yameendelea kutolewa taarifa siku hadi siku, kila siku kunavyokucha mikoa yote, pembe zote za nchi hii, yanatisha sana na hii ni changamoto kubwa sana wakati mwingine najiuliza hapa ni nini? Ni changamoto ya afya ya akili ama ni kitu gani au ni mazingira magumu ya hali ya uchumi ni kitu gani. Hivyo takwimu mbalimbali zimetolewa kila mikoa na zinajulikana, lakini mimi nakuja na jambo la ushauri kwa Wizara hii. Kwenye miaka ya 1980s mpaka 1990s tulikuwa na changamoto kubwa kweli ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI na ilionekana kwamba suala hili ni la kiafya tu, na kwa kweli tulihangaika sana ilivyoonekana ni health sector peke yake washughulikie masuala ya UKIMWI, lakini pale ilipokuja kujulikana kwamba suala hili ni cross cutting, ni mtambuka ikaja ikarudishwa kwenye jamii na zikaanzishwa Kamati mbalimbali za kudhibiti UKIMWI kuanzia ngazi ya Taifa mpaka ngazi ya vijiji, tukaona kumbe suala la maambukizi ya virusi vya UKIMWI si matibabu peke yake lakini pia hata maambukizi yake yanaenda kwenye social culture issues. Kwa hiyo, inahitajika jamii ihusike mpaka kule kwenye ngazi. (Makofi)

Kwa hiyo, hata hapa naona kuna mazingira fulani yanayoendelea na hili suala la mambo ya unyanyasaji wa kijinsia, yakionekana ya ubakaji na mengineyo yanayofanana na hayo. Suala hili inabidi sasa muda umefika tuangalie jinsi ya kulitatua, tulirudishe kwenye jamii na wanaohusika sana kwenye jamii yetu ni wale wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wanahusika, wanakubalika sana kwenye ngazi ya jamii. Tulirudishe suala hili kwenye ngazi ya jamii ili uhusike na itakavyoendelea hivyo, basi elimu itolewe kwa kila jamii kuanzia ngazi ya kaya, familia na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, kwa kufanya hivyo itaonekana huu ukimya tunaouona hata humu ndani tumeendelea kupiga debe hii ni sisi wakina mama tu ndani tangu imeanza kuchangiwa, sijaona akina baba kuna nini hapa? Kwa hiyo hapa tayari kuna tatizo social culture issues, mambo ya kijamii, mambo ya tamaduni zetu, kuna nini katika suala hili la ubakaji na mengineyo yanayofanana na hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia niendelee kwenye makazi ya wazee; tumeona kuna makazi 14 ya wazee nchi nzima na bado kuna wazee 271 tu wako maeneo hayo. Lakini mimi nilikuwa naangalia angalizo kama haya makazi tunasikia huduma zao bado siyo nzuri, hazitoshelezi na kweli Serikali haiwezi ikakidhi huduma zote za wazee. Sasa nini kifanyike, mimi nilikuwa nashauri kwamba huko tunakoenda ni vizuri kabisa huduma hizi za wazee ikapewa sekta binafsi na iruhusiwe kama kuna watu binafsi wanaweza wakaanzisha makazi ya wazee iruhusiwe ili wenye uwezo basi watalipia, kama wafanyakazi wanaweza wakatunza pensheni zao ikatunzwa kule baadaye wanapokuja kumaliza kazi wakiwa na umri mkubwa zaidi wanahamia kwenye makazi yale na huduma zao na fedha zao zinakuwa zimetunzwa kule, ni jambo linawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine nilikuona naona bajeti ya Wizara hii. Tumeenda kwenye taasisi mbalimbali ya Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii kwa mfano kule Rungemba kunahitajika miundombinu ile irekebishwe. Kwa hiyo, tunaomba bajeti katika item ya maendeleo iendelee kupewa kipaumbele, ipewe fedha kubwa ili marekebisho mbalimbali ya vyuo yawezekane ili kwenye vyuo vile kuwe mahali pazuri pa kujifunza na kufundisha walimu wetu na hata vijana wetu wanaotoka mahala pale. Kwa kufanya hivyo jamii yetu itakuwa na hali nzuri tukiboresha maendeleo ya jamii na kila jambo litawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)