Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nashukuru na mimi nichangie Wizara hii muhimu na nilikuwa nadhani kwamba ni muhimu Mheshimiwa Waziri akatufanya Watanzania tukajua kwamba hii ni Wizara muhimu; mosi, inahusika na maendeleo ya jamii kwa mantiki ya kwamba jamii nzima ya Tanzania; pili, ni jinsia maana yake ni (ke) na (me) maana kuna watu wanafikiria ni Wizara ya Wanawake; tatu, wanawake wenyewe na makundi maalum ambayo ndio vijana, watoto, watu wenye ulemavu na wazee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesema niyaseme haya kwa sababu yamezungumzwa hapa na wachangiaji wengi sana, namna gani kumekuwa na ongezeko la ubakaji na kulawitiwa kwa watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nilikuwa napitia taarifa za UNICEF ambazo zinatuambia ili Waziri najua hizi taarifa unazo lakini ni msisitizo tu, ili ujue jukumu lililokuwa mbele yako kwa sababu watoto wako chini yako. Watanzania kwa idadi yetu tuliyonayo sasa hivi watoto chini ya umri wa miaka 18 kwa mujibu wa UNICEF ni milioni 29.7; kwa hiyo, kwa lugha nyingine population ya Tanzania asilimia 50 ya Watanzania wote ni watoto chini ya miaka 18. Sasa tunaambiwa huyu mtoto tusipomlinda akiwa mtoto ndio anavyokuwa mtu mzima kuna vituko mbalimbali huko vinatokea, alizungumza Profesa hapa asubuhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Wizara hii tusiichukulie kama Wizara ya mzaha mzaha, ni Wizara ambayo mmepewa majukumu makubwa ya kulea Taifa. Katika hao watoto milioni 29 mimi leo nitamzungumzia mtoto wa kike ambao wako milioni 14.7. Tunaambiwa kati ya nchi ambazo zina kiwango cha juu cha ndoa za utotoni Tanzania tunaongoza, ni miongoni mwa nchi ambazo tuna kiwango cha juu cha ndoa za utotoni. Tunaambiwa kati ya watoto watano wa kike; wawili wanaolewa kabla hawajatimiza miaka 18. Sasa tujiulize katika hawa watoto milioni 14.7 kwa mnaojua mahesabu kama ndani ya watano hao ukiwagawanya kiwatano/watano kila watano wawili wanaolewa chini ya miaka 18 Taifa linakwenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unajua maendeleo ya Taifa yanahitaji jinsia ya (me) na jinsia ya (ke) zifanye kazi kwa pamoja tuweze kwenda mbele. Waziri unajua kizazi cha sasa sio kama kizazi cha mababu zetu na mabibi zetu, vijana wa sasa tunataka mtoto wa kike ajitume na mtoto wa kiume ajitume mnawaza nini kwa watoto hawa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaambiwa mikoa mitatu bora takwimu zinatufanya tuangalie namna gani tunakwenda kutatua tatizo. Mikoa mitatu bora ambayo kati ya wasichana watano wawili wanaolewa chini ya miaka 18, Shinyanga asilimia 56, Tabora asilimia 58, Dodoma asilimia 51 tunakwenda wapi?

Mimi niiombe Serikali juzi nilikuwa napitia maana Tanzania ni Mjumbe wa Baraza la Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu katika hilo Baraza ni la Kidiplomasia ndio, lakini mnajitathmini kwa namna gani haki za binadamu zinatekelezwa kwenye nchi husika? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Halima Mdee, dakika moja, malizia. (Makofi)

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, ni masikitiko yangu dakika moja; katika maeneo ambayo tunataka Waziri hili ulijibu katika maeneo ambayo Tanzania imeweka pending, haijakubali bado kuyafanyia kazi; mosi, ni eneo la ndoa za utotoni; pili, ni eneo la masuala ya mirathi sote tunajua wakina mama wanavyoumia kuhusiana na mirathi; tatu, ku-deal na sheria hizi Customary Laws (Sheria za Kimila) zinazonyima wanawake wa Kitanzania kumiliki ardhi. (Makofi)

Sasa kwa sababu ninajua Waziri unajua nataka uniambie kwa nini Watanzania kwenye vikao vya Kimataifa huko vya haki za binadamu masuala ya mtoto wa kike na masuala ya wanawake sio kipaumbele; na kama jibu ni tofauti niambie mna taarifa gani tofauti na hii taarifa ya Umoja wa Mataifa ya Baraza la Umoja wa Mataifa linalohusiana na haki za binadamu. (Makofi)