Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Minza Simon Mjika

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Spika, ahsante napenda nishukuru sana kwa kunipatia muda huu, lakini vilevile nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya wema wake wa pekee ambao ametufanyia katika siku hii ya leo. (Makofi)

Awali ya yote nimshukuru sana Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ambaye anafanya kazi kubwa kwa ajili ya Taifa letu hili. Mama yetu anapambana, anakimbia huku na kule kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu, tunamshukuru sana na zaidi ya yote tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kumlinda na kumpatia afya njema. Lakini vilevile nipende kuwashukuru akinamama hawa Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayofanya. Mama Gwajima na Naibu wako tunakuona sana unavyofanya kazi tunakuombea afya njema na uendelee kuifanya kazi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, basi kulingana na muda wetu mimi napenda niseme sehemu tatu tu; sehemu ya kwanza napenda kuongelea habari ya hawa watu wabakaji. Hakuna watu wananiumiza roho kama hao. watoto wa kike wananyanyaswa sana na vijana wa kiume wananyanyaswa sana, lakini nikiangalia hatima yake naona kama vile yaani hawafanyi makosa makubwa. Mtu yule anatakiwa achukuliwe hatua kama vile anavyochukuliwa muuaji kwamba ameua, apewe sheria kali ya kukaa gerezani hata miaka 20 ili ajifunze kule, kwa sababu mtu anapofanya hivyo wanawaathiri sana watoto wetu wa kike. Wanawaharibu watoto wetu, wanakosa amani na wanakatisha njozi zao kwamba alitaka asome pengine amefanyiwa jambo baya na bado likashindikana hata kutatulika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kingine niseme kuna Mheshimiwa Kapinga kasema mtoto hawezi akaongea maneno yale mahakamani, ndio maana unajikuta kwamba ukisema mahakamani kwamba nilitendewa jambo baya unaambiwa jambo gani hilo baya litaje. Sasa mtoto hawezi kutaja kwa asili yetu sisi Watanzania. Tunaomba watu kama wale washughulikiwe, hata msamaha wa wafungwa unaotolewa wakati mwingine Disemba wakati wa sikukuu, Rais watu kama hao wasitoke ashauriwe kabisa watu hao waendelee kukaa gerezani kwa sababu kosa wanalolifanya ni kubwa lakini unaona mtu kafanya kosa kubwa kama lile unashangaa baada ya miezi mitatu minne unamuona mtaani. Sasa linachukuliwa ni jambo la kawaida kabisa, lakini akipewa adhabu moja tu miaka 20 akakaa gerezani anatoka kule alishachoka hawezi kila kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba sana hilo mlichukue pamoja na Waziri husika wapewe adhabu za kutosha na wasitoke kwa msamaha wa Rais watu wa namna ile kifungo chao wapigwe miaka 30 akae mle ajifunze. Nashukuru sana. (Makofi)

Mheshsimiwa Spika, naingia kwa upande wa wamachinga. Ninapenda nimshukuru sana Rais wetu amewakumbuka vijana wetu kupata sehemu maalum za kufanyia kazi kwa kweli kwa hilo ninampongeza sana. Vile vile, wameitisha mkutano hapa vijana wetu wamepata semina mbalimbali, jinsi ya kuchukua mikopo na mikopo ile waitumieje, kwa hilo tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende upande mwingine wa wakina mama kweli mikopo wanapata lakini ile mikopo haitoshelezi. Nilikuwa naomba wenzangu wameongea hapa ninashukuru mimi niliona bora iwe asilimia 16 kwa mchanganuo ufuatao; asilimia 10 wanawake na wasichana wapate asilimia 10; lakini asilimia tatu wapate vijana, lakini asilimia tatu tena wapate walemavu; hiyo itapendeza kidogo. Kwa hiyo, mtu atachukua kitu ambacho ni kikubwa na anaweza akafanyia kazi. (Makofi)

Kwa upande wa wanawake ninapenda niseme kwamba hakuna mtu anafanya biashara kama mwanamke, mwanamke ni mjasiriamali wa kweli, akipewa mafunzo ya kutosha mwanamke hakosei na anafanya kazi kwa bidii zote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, basi mimi naomba kulingana tu na kwamba hatuna wataalam wa kutosha tunaomba Serikali iongeze hawa maafisa maendeleo ya jamii, ili kwamba watu kabla hawajapata mkopo wakina mama wapewe semina mkopo ule ni wa kufanyia nini na ufanyeje lazima ajue. Lakini mtu anaweza akachukua mkopo siku hiyo hiyo anakwenda kujengea nyumba, anakwenda kununua cement anaanza ujenzi wa nyumba, marejesho atatoa wapi? Fedha ya mkopo sio ya kujengea, fedha tunayojengea ni ile inayotengwa kwenye mzunguko yaani ile faida inapopatikana basi iendelee kwenye shughuli za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini unakuta mtu anachukua mkopo, anaingia kufanya sehemu zingine ambazo haziko muhimu na akinamama hawa tunaona wana majukumu mengi. Kina mama kweli tuna majukumu sana yaani kama ni kwenye familia mama anachukua majukumu asilimia 85 baba anachukua tu asilimia 15. Kwa maana hii mama atachukua mkopo akishachukua mkopo chakula cha nyumbani ni mama, mboga ni mama, watoto kwenda shule ni mama, uniform, viatu ni mama, baba hana habari tena hususani kule kijijini hawana habari kabisa. Baba anajua issue ni kulewa tu, hana mambo mengine anamsumbua mama, hiyo ni kweli wala msibishe, ninasema kitu ambacho nimekifanyia utafiti ni kweli, baba anakunywa anarudi anataka chakula huku nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba wakina mama hawa wasaidiwe na kingine ninapenda niseme kwamba tunapowapa mkopo basi mkopo ule utolewe kwa wakati. Kwa mfano, mtu anataka mkopo alime nyanya, nyanya inalimwa kuanzia mwezi wa nne na kuendelea huko kwenye kiangazi…

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

T A A R I F A

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya wakina baba sio wakina baba wote ambao hawajali watoto zao, mimi nasimama nafasi ya baba na mama pia, ahsante. (Makofi)

MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana hiyo naipokea lakini ni kwa baadhi ya akina baba…

SPIKA: Mheshimiwa Mjika.

MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema sio akina baba wote.

SPIKA: Mheshimiwa Mjika, subiri kidogo.

MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Spika, bee.

SPIKA: Mheshimiwa Minza Mjika, unaikubali taarifa hiyo?

MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Spika, naikubali sio kwa akina baba wote wanaofanya hayo matendo kama nilivyosema kwamba hususani wengi kule vijijini. Mimi natoka Simiyu nawaelewa ndugu zangu kule, lakini sio kwamba wote sio wote nalitambua hilo.

Mheshimiwa Spia, kitu kingine wakina mama wapewe mkopo kwa muda muafaka. Anapoomba mkopo kwamba pengine anataka kuanzisha biashara yake apewe kwa muda muafaka, lakini anapocheleweshwa kupewa mkopo anajikuta sasa anakuwa nje ya matarajio yake na hafanyi vizuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, ninapenda niongee juu ya hili jambo kwamba wakina mama wapate muda mzuri wa kuweza kufundishwa ujasiriamali kama nilivyosema hakuna kitu kinapotosha kama hicho. Inapofika marejesho wakina mama wengi tunaona jinsi wanavyohangaika wanakimbia huku na huku kumbe hawakupata shule nzuri kabla ya kuchukua mkopo wao.

Mheshimiwa Spika, basi kwa hayo yote ninapenda nishukuru ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)