Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ili na mimi niweze kuchangia Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ambayo inahitaji shilingi bilioni 44. Kwa uchache tu kwamba hii shilingi bilioni 43 kwa Wizara hii nyeti kabisa bado ni ndogo sana sana, ilitosha tu iongezeke. Nilikuwa natarajia kwamba Wizara hii ije na maombi ya kuanzia shilingi bilioni 800 huko shilingi bilioni 900 kama Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, jukumu la kulea watoto wetu ni la kwetu sisi wenyewe kama wazazi, lakini pia wamesema Wabunge wengine kwamba mtoto kama mtoto hawezi kujisemea mwenyewe. Ni dhahiri shahiri kwamba mtoto anaweza akakosa hata lishe, lakini asiseme, hata kama anahitaji mahitaji maalum bado akashindwa kusema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakumbuka nikiwa mdogo enzi ya Mwalimu nchi yetu ikiwa bado changa sana na ni masikini lakini wazazi wetu walikuwa wakienda kwenye masuala ya kliniki watoto wanapopimwa wanapoondoka walikuwa wanaondoka na maziwa ya unga, walikuwa wanaondoka na mkate vitu kama hivyo.

Sasa mimi naomba Wizara hii pia mama yetu Dkt. Gwajima hebu iboreshe hii Wizara na vitu kama hivi viweze kufanyika at least kuwe na motisha kwa mtoto, hata ikifika tarehe ya mtoto kwenda kliniki mtoto mwenyewe wakati mwingine mwenye umri wa miaka mitatu/minne akaweza kukumbusha. Waweze kupata motisha mbalimbali kama maziwa, blueband na nini na mambo mbalimbali. Hata hivyo ninaamini kabisa wewe ni jembe kweli kweli, unaweza ukaandika na maandiko na nini Wizara yako ikaendelea kupata misaada kama hiyo na ikaenda kutolewa kwenye zahanati na vituo vya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, liko jambo ambalo liko kwenye jamii yetu ambalo limejitokeza sana, wako baadhi ya wanaume/akina baba, wanadhulumu haki za watoto kwa kunyonya maziwa ya mama ambayo mtoto ndio alipaswa anyonye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili limejitokeza katika mikoa mbalimbali niombe Wizara ifanye utafiti yako majibaba yanafakamia maziwa ya watoto wanawanyonya wale wake zao wanaonyonyesha. Badala ya mtoto anyonye maziwa yale na kupata ile lishe basi baba anakwenda ananyonya; na kuna mtu ameniongezea nyama hapa akaniambia hivi kwamba yale maziwa ya mama kwanza yana virutubisho sana wako baadhi ya akina baba wamegundua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia yale maziwa ya mama yanasaidia kukata hangover ya walevi ambao wanakuwa wamekunywa pombe na yanasaidia kukata hiyo hangover. Kwa hiyo, niombe sana Wizara iweke mpango mzuri na itoe elimu ili akina baba hawa wasiwadhulumu watoto haki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nizungumzie pia suala la kisiasa; kumekuwa na ukatili mkubwa sana wa kijinsia kwenye masuala ya kisiasa kwa wanawake ambao wanachipukia kwenye masuala ya siasa, hususan hata sisi Wabunge wanawake humu ndani, tumekuwa tukinyanyapaliwa kwenye maeneo yetu tunapofanya shughuli zetu za kisiasa. Kwa hiyo, huu ukatili Wizara imejipangaje kuhakikisha kwamba inatusaidia sisi wanawake tunaokua kisiasa kwenye maeneo mbalimbali, ili tuweze kufanya shughuli zetu za kisiasa bila kufanyiwa ukatili, ikiwemo ukatili wa kwenye mitandao?

Mheshimiwa Spika, maana Mbunge mwanamke anaweza akasema jambo hapa na Mbunge mwanaume akasema jambo hilo hilo, lakini utakuta Mbunge mwanamke ananyanyapaliwa kwenye mtandao, anatukanwa matusi makubwa makubwa ya nguoni. Tunaomba Wizara muone namna gani ya kusaidia jambo hili ili lisiendelee kujitokeza kwa sababu, sisi sote ni Watanzania na ni jamii moja.

Mheshimiwa Spika, nataka nizungumzie ukatili wa kingono…

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: …jamani naombeni leo sina… Naomba Taarifa kaeni nazo, leo hii naomba. Nina mambo mahususi sana hapa. Nina jambo mahususi sana la kuchangia. Tafadhali kaka yangu nakuheshimu, nakupenda sana. (Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Jacqueline Msongozi, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ramadhan Ramadhan.

T A A R I F A

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe Taarifa mzungumzaji, mama yangu kwamba wako wasichana na wanawake wengi wamekata tamaa kuendelea na shughuli za siasa kwa sababu ya unyanyapaa anaoendelea kuusema. Kwa hiyo, naomba nimpe Taarifa kwamba, hilo tatizo kweli ni kubwa na lazima hatua zichukuliwe. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Jacqueline Msongozi, unaipokea Taarifa hiyo?

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naipokea sana, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa nizungumzie ukatili wa kingono; Wabunge wenzangu wengi wamechangia hapa kuhusiana na ukatili wa kingono kwa wanawake. Ni kweli kabisa ukatili wa kingono katika nchi yetu ya Tanzania umeshamiri sana, lakini mimi nitaliongelea jambo hili kitofauti kidogo.

Mheshimiwa Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya UKIMWI na kwa kuwa ni Mjumbe wa Kamati ya UKIMWI, nitazungumza jambo ambalo linahusiana na suala la maendeleo ya jamii, lakini pia nitahusianisha na suala la ngono ambalo linaungana pia na suala la UKIMWI.

Mheshimiwa Spika, hapo unanipoteza unaponyanyua nyanyua microphone, naona kama unataka unikatishe. Naomba sana tafadhali.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Dakika moja, malizia.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, dakika moja.

Mheshimiwa Spika, wako wanaume ambao hawataki kufanya tohara na kwa misingi hiyo wanataka kuwaingilia wanawake kwa maana ya kuwapa huduma hiyo bila kufanya tohara. Sasa mimi nitoe wito kwa Watanzania wote wanawake wenzangu kwamba suala la mwanaume ambaye hajafanya tohara kushirikiana naye ni hatari kwa afya yako na niseme tu kwamba inasababisha saratani ya shingo ya kizazi. Kwa hiyo, haifai kabisa kwa matumizi ya binadamu na wakatae kutoa huduma hiyo endapo kama atamkuta mwanaume hajafanyiwa tohara kwa sababu inasababisha saratani ya shingo ya kizazi. Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)