Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Prof. Kitila Alexander Mkumbo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ubungo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Spika, wanasaikolojia hueleza maana ya maisha kuwa ni mchakato wa binadamu na jamii yake kusaka na kutunza furaha, yaani tunafanya mambo yote haya ya maendeleo katika nyanja zake zote ili hatimaye tupate furaha kama mtu mmoja mmoja, jamii na hatimaye Taifa. Kiwango cha furaha katika nchi ni kigezo na kiashiria muhimu sana katika kupima ubora wa maisha katika jamii na nchi husika. Ni kwa sababu hii kila mwaka hutolewa taarifa ya dunia kuhusu kiwango cha furaha katika kila nchi.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya mwaka 2022 iliyotolewa na taasisi inayojihusisha na kupima kiwango cha furaha duniani ya Gallup World Poll wastani wa kiwango cha furaha katika nchi yetu kilikuwa ni 3.623 (kiwango cha juu ni 10.0), tukiwa ni miongoni mwa nchi kumi duniani ambazo watu wake wanaonesha kiwango cha chini cha furaha. Nchi zngine ni Burundi (3.775), Yemen (3.658), Tanzania (3.623), Haiti (3.615), Malawi (3.6), Lesotho (3.512), Botswana (3.467), Rwanda (3.415), Zimbabwe (3.145) na Afghanistan (2.523). Taarifa hii inapatikana https://dmerharyana.org/world-happiness-index/

Mheshimiwa Spika, ukisoma majukumu ya jumla ya Wizara hii utaona kuwa jukumu la msingi la Wizara hii ni kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya kuleta furaha na kuamsha matumaini kwa jamii na kwa mtu mmoja mmoja. Na mimi katika mchango wangu ninataka nichangie maeneo mawili ambayo ninashauri Wizara ichukue hatua kadhaa za kisera na kisheria katika kuleta furaha kwa jamii yetu.

Kuhusu haja ya kinga jamii wa wazee; kwa kuzingatia makadirio ya idadi ya watu (population projections) ya NBS, Tanzania inakadiriwa kuwa na watu 61,280,743 na inatarajiwa kuwa na watu 67,036,280 ifikapo mwaka 2025. Kati ya idadi hii ya watu, wazee[1] ni watu 2,801,541 kwa mwaka 2022 (sawa na asilimia 4.6) na inatarajiwa kuwa 3,038,267 mwaka 2025. Hawa ni Watanzania ambao kwa nyakati tofauti waliwahi kuitumikia nchi yetu ama katika nafasi za kuajiriwa au kujiajiri au katika mashamba huko vijijini.

Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha pia kwamba katika nchi yetu zaidi ya asilimia 80 ya wazee wanaishi vijijini na wakiwa huko wanalazimika kufanya kazi zozote ili waendelee kuishi. Wengi wao hawana msaada. Aidha, takwimu zinaonesha kuwa wazee ndio wanaotunza watoto yatima; asilimia 40 ya watoto yatima Tanzania wanatunzwa na wazee ambao nao wanahitaji kutunzwa.

Mheshimiwa Spika, takwimu nyingine muhimu ni kwamba ni asilimia 6.5 pekee ya wazee nchini Tanzania ndio wanaopokea malipo ya uzeeni (pensheni). Wazee walio wengi hawana msaada hasa kufuatia kuanza kuvunjika kwa mfumo wa familia jamii (extended family) kwenda katika mfumo familia ya kibaolojia (nuclear family). Aidha, tafiti zinaonesha kuwa kiwango cha umaskini kwa kaya zenye wazee nchini kipo juu kwa asilimia 22.4 zaidi ya wastani wa kitaifa!

Kutokana hali yao, wazee wengi wanakabiliwa na ukosefu wa usalama wa kifedha, wapo katika hatari zaidi ya kuugua magonjwa sugu, na wanakabiliwa na upweke.

Mheshimiwa Spika,nini kifanyike? Ninapendekeza tutekeleze kinga jamii (social protection for all). Mwaka 2010 Serikali ilifanya utafiti mzuri sana unaoitwa Achieving income security in old age for all Tanzanians: a study into the feasibility of a universal social pension. Pamoja na mambo mengine, utafiti ulipendekeza kulipa wazee kinga ya jamii kwa kiwango cha shilingi 16,586. Kwa bei ya leo hii inaweza ikawa sawa na shilingi 28,586. Kwa idadi niliyoeleza hapo juu hii ni sawa na shilingi bilioni 80 kwa mwezi sawa na shilingi bilioni 961 kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, nini faida ya kinga jamii kwa wazee? Katika mpango wetu wa maendeleo wa tatu wa miaka mitano (2021/22-2025/26), pamoja na mambo mengine, tumejiwekea lengo kuwa ifikapo mwaka 2025/2026 tuwe tumepunguza idadi ya watu maskini (wanaoishi chini ya mstari wa umaskini) kutoka watu milioni 26.4 mwaka 2020/2021 hadi watu milioni 20.2 mwaka 2025/2026. Lengo hili sio dogo kwa kuzingatia kuwa pamoja na kwamba uchumi uliendelea kukua vizuri hadi kufikia hatua ya uchumi wa kati wa chini, ukuaji huu haukwenda sambamba na kupungua kwa idadi ya watu maskini. Ukweli ni kwamba idadi ya watu maskini iliongezeka kwa watu takribani milioni mbili katika kipindi hicho.

Mheshimiwa Spika, faida za hatua ya kutoa kinga ya jamii kwa wote ni kubwa. Ukiacha kuongeza furaha kwa wazee wetu hawa, tafiti zinaonesha kuwa hatua hii itapunguza kiwango cha umaskini miongoni mwa wazee kwa asilimia 57.9. Aidha, hatua hii itasababisha kuwaondoa watu zaidi ya milioni 1.5 katika wimbi la umaskini wa kutupa. Kwa maneno mengine, hatua hii itasaidia sana katika kufikia malengo tuliyojiwekea katika mpango wetu wa maendelea katika kupunguza idadi ya watu maskini. Tayari nchi nyingi zimechukua hatua hii na matunda yanaonekana. Nchi jirani ya Kenya walitumia taarifa yetu ya utafiti na sasa wanatekeleza mpango huu. Nchi zingine Afrika ni pamoja na Mauritius, Lesotho, Afrika Kusini, Eswatini, Zambia, na Uganda wapo katika majaribio.

Mheshimiwa Spika, haja ya kuondoa zuio la kutafuta furaha wakati wa asubuhi na mchana; juzi nikiwa Dar es Salaam nilipata malalamiko kutoka kwa mmoja wapiga kura wangu kutika katika Kata ya Makubiri. Mpiga kura huyu ni daktari wa binadamu anayefanya kazi katika kitengo cha mortuary katika moja ya hospitali za Serikali katika Mkoa wa Dar es Salaam. Mara nyingi huingia usiku na kutoka asubihi. Kwa utaratibu aliojiwekea, kila anapotoka asubuhi hupitia baa iliyopo karibu na nyumbani kwake na kunywa bia sita kabla hajaenda nyumbani kulala. Alilalamika kuwa kila anapopita baa na kunywa hukamatwa na askari na huachiwa baada ya “mazungumzo”. Aidha, mwenye baa pia hukamatwa na kuachiwa katika mazingira hayo hayo.

Mheshimiwa Spika, siku ya Ijumaa tarehe 20 Mei, 2022 nilikutana na wafanyabiashara zaidi ya 200 kutoka katika Jimbo la Ubungo kwa lengo la kusikiliza kero na ushauri na kupokea maagizo yao kuhusu mambo ambayo wangependa niyawakilishe hapa Bungeni. Moja ya malalamiko makubwa yanafanana na ya daktari niliyemwelezea hapo juu kwamba wafanyabiashara katika jiji la biashara wanazuiawa kufungua biashara asubuhi na kuzuiwa kufanya biashara baada ya saa sita usiku! Baada ya kufuatilia na kuzungumza na baadhi ya Maafisa Biashara na maaskari wanaosimamia utaratibu huu, nimebaini kuwa tunayo Sheria ya Vileo (The Intoxicating Liquors Act, 1968) ya mwaka 1968. Katika kifungu cha 14, sheria imeweka muda wa kuuza vileo ambapo ni kuanzia saa sita mchana hadi saa sita usiku kwa siku za kazi. Ni wazi kuwa sheria hii imepitwa na wakati ukizingatia kuwa ilitungwa mwaka mmoja baada ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha na wakati huo nchi ikijulikana kuwa ni nchi ya wakulima na wafanyakazi.

Mheshimiwa Spika, sasa ni muhimu sheria hii na zingine zinazopangia watu muda wa kufurahi ziangaliwe. Kawaida majiji duniani kote huwa yanafanya kazi saa ishirini na nne na kuna watu ambao wanafanya kazi usiku na kupumzika mchana. Tunaweza kuzipa mamlaka za Serikali za Mitaa zikatunga sheria ndogo kutokana na mazingira yao kulikoni kuendelea kuwa na sheria moja ambayo inakwaza sana biashara na kuondoa furaha za watu.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003, dhana ‘mzee’ hutafisiriwa kwa kuzingatia umri mkubwa, majukumu aliyonayo na hadhi ya mtu katika jamii. Katika maoni yangu haya ninazingatia umri wa mtu ambapo kwa mujibu wa sera hii mzee ni mtu yeyote mwenye umri wa miaka 60 na kuendelea. Kigezo kikubwa ni kwamba katika umri huu binadamu huanza kupungukiwa nguvu za kufanya kazi.