Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Dr. Dorothy Onesphoro Gwajima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, napenda kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuhitimisha hoja niliyoiwasilisha mbele ya Bunge lako tukufu siku ya leo tarehe 30 Mei, 2022.

Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla ambao wametoa pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao wamekubali kabisa na kuona Wizara hii ilikuwa imechelewa ilitakiwa ianze siku nyingi sana ili haya yote ambayo yanatukuta hapa leo yangeweza yakawa yamerudishwa nyuma kwa kasi kubwa kwa sababu tungekuwa na mikakati hii tuliyonayo leo mfano ya malezi na makuzi ya watoto tusingekuwa na kizazi ambacho kina ukatili mwingi namna hii hivi leo.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo kila jambo linakuja kwa wakati wake, tunashukuru kwa maono yake na tumepokea pongezi hizi, tutazifikisha ili aone kwamba Bunge lako tukufu limeelewa tafsiri ya uamuzi wake mkubwa kwa maslahi ya Taifa letu kwa miaka 50 na miaka 100 mbele.

Mheshimiwa Spika, naishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa ushauri na kuisimamia Wizara yangu kwa umakini mkubwa, ushauri na maelekezo yao yamesaidia katika kuboresha utendaji wa Wizara hii hadi hapa ilipo. Wizara yangu inathamini sana michango yote iliyotolewa naomba nilithibitishie Bunge lako tukufu kuwa tutaifanyia kazi na majibu yote ya hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge hapa tutaziwasilisha kwenye ofisi yako ili waweze kuzisoma na kuelewa tumezitendeaje haki na kwa sababu hii ni process inaendelea ya Bunge tunaamini kadri tunavyokwenda mbele watakuja kuona kwamba tumezitendea haki.

Mheshimiwa Spika, nachukua tena fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliopata nafasi ya kuchangia hoja yangu niliyoiwasilisha leo Bungeni, michango yao ni mizuri sana ina lengo la kuboresha utekelezaji wa majukumu ya Wizara lakini kuboresha tija na ufanisi wa maisha ya watanzania kwa mingi ya vizazi vijavyo. Jumla ya Waheshimiwa Wabunge nimehesabu hapa 39 wamechangia hoja yangu ambapo kati yao 25 wamechangia kwa kuzungumza na hapo hapo Wabunge 14 wamechangia kwa maandishi.

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana pia Mheshimiwa Jafo naye namuongeza anakuwa wa 26 aliyechangia hapa akizungumzia athari nzima ya masuala ya mazingira tunayoishi katika nyanja za makelele na mitetemo jinsi gani inaweza kuathiri afya za Watanzania pamoja na watoto pamoja na wazee na wagonjwa hatimaye tukawa na akili ambazo siyo njema sana tukaanza kusababisha matukio makubwa makubwa na tukakosa tumeyatoa wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika michango iliyotolewa ipo inayotoa ushauri na mengine ni maswali na Waheshimiwa Wabunge waliochangia nimewaorodhesha naomba kwa kibali chako nitakapowasilisha taarifa yangu kwa maandishi niunganishe orodha yao.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa nitoe maelezo na ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge waliochangia hoja yangu na nikiri kwamba leo Bunge limeweza kuona ukubwa na unyeti wa hii Wizara kiasi kwamba huenda hii siku moja ikawa haitoshi ya kujadili hoja zote hizi maana hapa mambo ni mengi. Lakini nimebaini baadhi ya Wabunge bado hawajaelewa profile ya hii Wizara napenda kusema kwamba ni Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. Kwenye makundi maalum hapa tunao watoto, tunao wazee, tunao wajane na wamachinga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawa vijana na walemavu wako kwenye Wizara nyingine iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ingawa sisi kama Serikali mambo yanaingia huku na kule, kijana anaweza akaibuka akawa ni mmachinga, lakini bado kijana anaweza akawa bado kijana akawa tena mjane hivyo. Kwa hiyo, tunafanyakazi kwa pamoja nilikuwa nataka niweke tu sawa hili jambo hapa ili ninapojibu twende pamoja.

Mheshimiwa Spika, nikiri kwamba hoja zimetolewa za kutosha nikiangalia katika pillar ya governance nimeona hapa Wabunge wameongelea jinsi gani uendeshaji wa Idara za Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii zilivyo kule kwenye halmashauri. Kwa sababu bila wao kuwa na nguvu kule tunaweza tukasema sisi huku tunaongea sana tunatengeneza miongozo na Sera nyingi lakini kule chini utekelezaji tone yake ikabadilika kutokana na kwamba zile powers hawana ambazo zingekuwa zinaakisi ukubwa wa tatizo ambalo mmelijadili leo hapa.

Mheshimiwa Spika, mmeongelea masuala ya watumishi; upungufu wa watumishi kwa upande wa Ustawi wa Jamii pamoja na Maendeleo ya Jamii kitu ambacho hawa sasa ndiyo engine au hawa sasa ndiyo chachu ya kutengeneza jamii kule ikae sawa hata Wizara ya Elimu ikija, Wizara ya Afya ikija ya Kilimo ikija ya Nishati ikute jamii imeandaliwa kifikra kuweza kupokea haya mambo. Nashukuru kwamba mmelijua hili jambo na nina imani kwamba full council zetu zingekuwa zinajadili kwenye tone hii tungeweza kusukuma zaidi maamuzi na vipaumbele vya halmashauri kiasi kwamba tukapunguza changamoto hizi nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mmeona jinsi multi-sectorial approach ilivyo kwenye Wizara yangu kwamba sisi ni coordinator ni kama airport ya Amsterdam tunakaa pale tunapokea kila ndege inatua inaondoka, inaondokaje inategemea na Wizara yangu imewezeshwa vipi kuweza kuzipokea hizi ndege zinazo-take off pamoja na kuondoka, kwa hiyo, tunaamini kwamba imekuwa ni shule pia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwenye masuala ya uwezeshaji wa vitendea kazi kwa hawa maafisa wachache waliopo mmeweza kuona vizuri jinsi ambavyo tunahitaji kufanyakazi kubwa kuwawezesha hilo tumelipokea. Lakini pia mkiangalia sasa hivi kwenye upande wa miundombinu yao ya ufanyaji kazi bado ni changamoto mmechangia vizuri sana mmeweza kwenda kwenye upande wa huduma jinsi gani watatoa huduma kwenye maeneo mbalimbali bado ni changamoto inayotokana pia na wao kutowezeshwa.

Mheshimiwa Spika, mmechambua vizuri kuhusu jamii jinsi ambavyo ina nafasi pia kwenye masuala haya yote, kwa sababu jamii kama jamii ina mambo mengi yanaendelea ndani yake inategemea na utayari wao kuweza kuyatoa na kuyaibua kwenye vikao vyao halali kuanzia kata, kijiji tarafa mpaka Wilaya mpaka mkoa ndivyo hivyo ambavyo tunaweza kama Serikali kuyafanyia kazi kwa urahisi yote hii inaonyesha kwamba tunahitaji dawa ya jamii ambayo ni Afisa Ustawi wa Jamii tunahitaji Maendeleo ya Jamii.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa ridhaa yako naomba nijikite kwenye ukatili. Ukatili imekuwa ni sauti leo imevuma sana humu ndani na imegusa wengi sana, nafurahi kuona kwamba sauti hii imevuma sana kwangu mimi kama Waziri mwenye dhamana na kwa niaba ya Serikali haya ni mafanikio makubwa kwa sababu sasa ule mpango wetu wa MTAKUWWA unaoratibiwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu wa kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto ndiyo unafanyakazi na umefanikiwa sana. Nasema hivyo kwa sababu zamani matukio haya yalikuwa hayaripotiwi kabisa kila mtu alikuwa anaona aibu anayaficha hayakuwepo. Lakini baada ya MTAKUWWA kuanza mwaka 2017 na 2018 na inaisha Juni, 2022 Kamati zimeundwa mpaka ngazi ya kijiji na kule kwenye mitaa zimeanza sasa kuchukua role yake ya kuelimisha jamii, jamii imepata confidence ya kuanza kuripoti hivi vitu.

Mheshimiwa Spika, topic hii ni kubwa peke yake Mungu anisaidie niimalize ili niende na nyingine, lakini nafikiri ingetosha siku mbili.

Waheshimiwa Wabunge, walio wengi wamezungumzia ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kwamba vitendo vya ukatili vinaendelea kushamiri katika jamii na wanaofanya ni ndugu wa karibu. Utafiti wa UNICEF pamoja na Serikali mwaka 2021 Januari - Desemba umeonyesha kwamba 60% ya ukatili huu tunaoongea hapa unafanywa majumbani kwetu wakiwepo wazazi wetu, ndugu, wajomba na watu tunaowaamini huko huko tena usiku mwingi, unaamka mtoto kakatiliwa au mtoto wazazi wameondoka wameenda kwenye shughuli nyingine kakatiliwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kuna mmomonyoko wa maadili mkubwa sana na kukosa imani ya Kimungu na hofu ya Mungu katika jamii zetu huku ndani. Jambo ambalo ni kichaka cha mtihani mkubwa na hakihitaji sana fedha nyingi kupambana na hiki kitu, kinahitaji mioyo ya uzalendo na watu walioguswa wanaosema hili hapana kila mtu kwa nafasi yake apaze sauti ili masikio ya Watanzania yakisikia na macho ya Watanzania yakiona, asilimia 50 ya tatizo linaondoka kwa sababu wakatili sasa watajiona hawako salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aidha Waheshimiwa Wabunge wametoa ushauri mbalimbali katika kutatua changamoto hii ya ukatili. Serikali katika kushughulikia changamoto hii naomba niisemee kwamba imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na vitendo hivi ikiwemo kuanzisha Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto kuanzia ngazi ya Taifa, mkoa, halmashauri, kata, kijiji na mtaa. Kamati hizi uzuri wake ukiziangalia zina kila mtu mle ndani kama ni kwenye kijiji kuna kiongozi wa Serikali ya kijiji pale kuna walimu, kuna watu wa afya, kuna ASASI za kiraia pale pale kuna viongozi wa dini, pale pale kuna wanawake, pale pale kuna vijana, pale pale kuna watu maarufu, pale pale kuna polisi jamii na nilishukuru Jeshi la Polisi sana kwa kuzingatia hii ajenda limepeleka vijana wa polisi tena graduates zaidi ya 4500 katika kata zetu mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, hii inaonesha jinsi gani Serikali inafanya kila jitihada kuweza kuhakikisha kule jamii inaamka kwenye zile kamati kuna Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na Maafisa Ustawi wa Jamii. Lakini sasa changamoto tuliyonayo katika kupambana na hiki kitu kamati nyingi zimeundwa zinakuwa haziko hai, hata zile zilizojengewa uwezo. Ukienda kwenye full council zetu nyingi unakuta hii taarifa haiko itokanayo na utendaji wa hii kamati.

Kwa hiyo, tunapokwenda kujenga uwezo tunadhani kwamba sasa tutaagiza full council zote na vikao vyote vya halmashauri viagize kuwe na chapter ya taarifa hizi za ukatili ili watu waweze kuwajibika na kuona kwamba ni muhimu hii ajenda iende mbele kama kipaumbele chao.

Mheshimiwa Spika, lakini Serikali haijaishia hapo imeimarisha Madawati ya Jinsia Jeshi la Polisi na hapa mmechangia kwamba tuone namna gani jinsi ya kuyaondoa pale, kwa sababu suala hili ni la Kiserikali tutaenda kujadili chini ya uratibu wa Wizara yangu, lakini kwa ridhaa ya Mheshimiwa Waziri Mkuu tuone tunafanyaje. Aidha, kuwaelimisha watu wasiogope au kama inabidi hivyo ndivyo hii tathmini inayofanyika ituambie kwamba tuyapeleke eneo gani ili mwitikio uwe mkubwa zaidi.

Lakini pia ukiacha hizi Madawati ya Jinsia Jeshi la Polisi tumeanzisha vituo vya mkono kwa mkono (one stop centre) katika hospitali zetu mbalimbali na zoezi linaendelea na hivi vinakuwa vinatoa huduma jumuishi za kitabibu msaada wa kisheria na ustawi wa jamii kwa manusura wa ukatili na niseme hapa kuna tabia ya jamii kuficha ushahidi; wanakatiliwa, wanaanza kwa kusema huyu ni babu, huyu ni mjomba utapata laana wewe mtoto nyamaza.

Mheshimiwa Spika, kipindi tunapokuja kusikia kinyemela tunakwenda kuwapeleka kwenye haya madawati ushahidi umefutika. Nilitembelea Dawati la Chanika Dar es Salaam, akasema yule Afande yuko pale anaitwa Christina kwamba sisi tumepokea kesi nyingi sana na 99.9% zilizofika kwa wakati zilikwenda mahakamani zikashinda kesi.

Sasa shida inakuwepo imechangiwa hoja hapa kwamba mahakama saa nyingine zinachelewesha kesi nikaenda mpaka kule nikaenda mpaka Polisi nikaambiwa kwamba sasa unapeleka kesi haina ushahidi watu wameamua kupatana zirudi nyumbani wakamalize kindugu. Lakini wengine wamehongana hapo katikati, wengine wamekimbia wametoweka, lakini wale wanaofanikiwa kufika kwenye vituo hivi ushahidi ukachukuliwa asilimia 99.9 kesi zao zimekwenda haraka sana na wameweza kushinda na watu kila siku tunasikia wamefungwa miaka 30, wamefungwa miaka mingapi, hizi ni hatua ambazo Serikali inafanya. Hivyo jamii tunaomba ichukue wajibu wake kutoa msaada kwenye hii mifumo ambayo imeshaanzishwa ili tuweze kwenda sawa katika kufikia ufanisi.

Mheshimiwa Spika, lakini ukiacha hilo, tunazo nyumba salama, tunao watoto wengi waliofanikiwa kwenda nyumba salama waliweza kuepuka ukatili. Tatizo nyumba salama tunakubali bado ni changamoto na ni zoezi ambalo tumepanga kuendelea kuziongezea sambamba na utoaji elimu katika jamii zetu.

Mheshimiwa Spika, naomba tuseme kwamba kwenye vyuo vikuu nako ni mtandao wa ukatili upo lakini Serikali imefanikiwa kuanzisha madawati ya jinsia kwenye hivi vyuo vikuu pamoja na vyuo vya elimu ya kati. Hatujaishia hapo kwenye shule za msingi pamoja na shule za sekondari kule tunakwenda kuzindua kwenye siku ya Mtoto wa Afrika tarehe 16 Juni, Mabaraza ya Watoto yanakwenda kuzinduliwa pale, lakini Madawati ya Jinsia yanakwenda kuzinduliwa pale, klabu za watoto zitazinduliwa pale. Kwa hiyo, watoto wakikatiliwa nyumbani baba na mama hamna muda wa kusikiliza watakwenda kuyasema shuleni, lakini pale shuleni tunaweka utaratibu Maafisa wa Ustawi wa Jamii hata kama ni wachache tutaomba na wa kujitolea waliostaafu wawe wanakwenda pale kuwaimarisha hawa tupate mpaka ma-matron wanaoweza kuongea na hawa watoto ili waweze kufunguka na kusema mambo ambayo mengine hawawezi kuyasema kule majumbani kwao.

Mheshimiwa Spika, tunaendelea kufanya kampeni ya twende pamoja ya ukatili sasa basi, lakini tumeiboresha hii kampeni tumetangaza na tutatangaza tena kesho fomu maalum ya wazalendo wote wapambanaji popote walipo wakienda kwenye google ukaandika SIMAUJATA. SIMAUJATA ni Shujaa wa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii Tanzania, tumepata vijana wengi, muitiko ni mkubwa baada ya kutoa hizi elimu za mara kwa mara wanasema tunataka kwenda mstari wa mbele, sisi tumeshachoka kukatiliwa na kuona watu wanakatiliwa, wanajisajili.

Mheshimiwa Spika, itakuwa sasa kila mtaa tunaangalia tumemsajili nani wenzetu wa utalii wametengeneza Jeshi lao la USU na sisi tunatengeneza Jeshi la SIMAUJATA, waende mstari wa mbele, mlango kwa mlango, mkiona wanapita kwa baiskeli wameweka redio kama ndugu zangu wa Kolomije mfungue milango, watakuwa wanasema kile tulichowalisha maneno ili wananchi wasikie waweze kuona hatuwezi ku-afford kuwa na mabilioni ya pesa ya kununua magari kwenda kule, kuna vita vingine ni vya kizalendo tu na moyo katika kulitetea Taifa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hata ninyi Wabunge mlioko hapa wanawake kwa wanaume mnaombwa mjiunge kwenye hiyo kampeni, lakini niseme vita hii inasemwa sana kwenye centre ya uadui tunaona jinsia ya kiume inainuliwa pale. Wale wanaume siyo wote ni wanaume wachache lakini wanaume wengi walio wazuri ni kama vile wamekubali haya mambo yaendelee, hatuoni forum zao tunaona ma-kitchen party ya akinamama, tunaona majukwaa ya akinamama ya VICOBA, tunaona akinamama wanahangaika, tunataka kuona wanaume wanainuka wale waliobarikiwa wenye hekima wanasema kwa wanaume wenzao hapana hii haikubaliki wawakemee tunakimbiza mtu kaiba kuku anakwenda kusitiri njaa tunamshughulikia kweli kweli, lakini tunaacha mbakaji tunamstriri na wababa wapo, matumbo yabebe Watoto, yazae Watoto, wabakwe akinamama, wabakwe watoto wa kiume, wabakwe wa kike hii haikubaliki. Akina baba mko wapi? Wakina baba wazuri mko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, dunia sasa inachukua direction ya mkakati wa He for She; He for She maana yake ni kumnyanyua mwanamme atakayekuwa mfano wa nembo ya Taifa ambapo wanaume wengine wakimuangalia wanamuona kwamba sisi mbona kama vile siyo wanaume, tumchoreje mwanamme wetu wa jamii ya Kitanzania ambaye yuko mbali na ukatili, ni baba wa familia, ni mbeba maono ya familia na wengine wote wakimuangalia wanaona aibu, watakimbia wataogopa. Leo wakatli na wabakaji wanabeba nembo ya kiume wanaifanya ndiyo nembo ya sura ya mwanaume wa Tanzania, wanaume naomba muwakatae, amkeni mtualike kwenye vikao vyenu tuje tufungue vikao vya akinababa vinavyosema mwanamme kibaka wewe siyo mwanamme, wanaume wamekuwa na moyo mdogo akiudhiwa na mwanamke anamimina risasi saba kwenye kichwa cha mwanamke, ameuawa kule Shinyanga, ina maana wanaume kama ni viongozi wa familia mioyo imekuwa midogo kiasi hicho hasira kidogo umeua hasira kidogo umekomoa hii siyo sawa bebeni uanaume mseme hapana kwa wenzenu wanaowaharibia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tukisema wanawake wanaweza maswali yanakuwa mengi, sasa imeanza profile kubadilika, wanaume mnakwenda down na mnapelekwa na wenzenu wachache simameni kwenye nafasi zenu Mungu alizowapa, musimamie uanaume wa heri na baraka na furaha na amani kwenye maisha ya watoto hawa wa kike na wa kiume, kwa sababu silaha za kubakia sasa mmepewa nyinyi sisi tutafanyaje wanaume kataeni tuko pamoja na ninyi tupambane na wale wachache. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inaumiza sana na hapa ndiyo sehemu ya kusema ili tubebe spirit ya kitaifa, hili halina hata chama kipi, halina cha imani ipi, halina cha itikadi gani, ni jambo la kitaifa lazima tuende pamoja. (Makofi)

Vilevile Wizara inafanya tathmini ya utekelezaji wa MTAKUWWA kwa kipindi kilichopita kama tulivyosema, tutasubiri hiyo tathmini, lakini aluta continue vita lazima ianze mlango kwa mlango tupeane ushirikiano wakati tunaisubiri tathmini hiyo mbele ya safari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunao mashujaa wengine wamejiandikisha na walikuja hapa Bungeni leo watu wanajitokeza kwa wingi, tunao vijana wa Pink Tie ambao wanaongozwa na Pink Tie Foundation hawa ni akina Lilian Mwasha huyu ni mtumishi wa Mungu, akina Salma Dakota, akina Furaha Dominick tunao vijana akina Jacob kutoka Mara wamesajili Safe Network kwa uchungu kutokana na mambo haya haya na wanabeba ajenda kweli siyo suala la mwanamke tu ni suala la mtoto wa kiume pia. (Makofi)

Tunao Wanawake Live akina Joyce Kiria, tunao wengi na wengine siwezi kuwataja hapa, hii inaonesha kwamba sindano imeingia dawa, imeingia sasa ari ya vijana ya kuona kwamba Taifa linatokomea inachemka, utafanyakazi ya kurudisha nyuma na wakatili hawataweka makao makuu ya shetani mwa ukatili Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze sasa tunafanyaje maana yake nyuma ya ukatili pia tuna ajenda ya uchumi huku chini, tuna agenda ya mila ya desturi ambazo ni area pia zimewekwa kwenye MTAKUWWA, lakini tuna masuala ya kisheria niseme kwamba suala hili la hizi programu mbili za kulea watoto wetu malezi na makuzi ya awali ya mtoto tumeisema hapa tumeanza na vituo 20 Dodoma na kumi Dar es Salaam na 15 vimeanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, huu ni mwanzo tu vilikuwa vya majaribio, lengo ni kwenda nchi nzima, hapa nitoe wito kwa akinamama na akinababa ambao wanapenda kuhakikisha watoto wetu sasa wanaanza kukuwa vizuri tujitokeze, tunachangia harusi, tunachangia vitu vingi vituo hivi ni shilingi 10,000,000 hadi 13,000,000 tufanya force account, tuona tunafanyaje viende kwa kasi sana tunao wadau wanatusaidia, lakini na sisi Serikali tunaweka fedha pale, lakini na jamii ya wapenda maendeleo katika spirit ile ile ya kuchangia mambo yaende kwa kasi tujipange ndugu zangu hakuna kuchelewesha mtoto ukimchelewa leo kesho amepotea, vituo hivi vinatakiwa vijengwe nchi nzima na kazi inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natoa tu wito huu kwa ajili ya kuongezea kasi lakini Serikali mpango wake vishuke ilipo zahanati kama ni kwenye kata kuna hicho kituo ilipo zahanati kwenye kijiji kuna hicho kituo, ilipo shule kuna hicho kituo, walimu watapatikana ndugu zangu kuwalea wale watoto sio kazi kubwa sana hauhitaji ma-degree mengi, hawa hawa tulionao tutaanza nao wakati taaluma hiyo ya saikolojia na vitu vingine vikiendelea kukuwa sambamba na wanaustawi wa jamii wetu wanatengeneza sheria yao kwa hiyo tutakuwa mpaka na kliniki za wana ustawi wa jamii kama tulivyokuwa na kliniki za zahanati au vituo vya afya au za kiuuguzi ili waweze na wenyewe kusajiliwa kama ni private au kama government waweze kuwafikia wananchi popote kule walipo wakati huko tukiendelea kuajiri wa Serikali ili kufikia ile asilimia tunayoihitaji.

Mheshimiwa Spika, usawa wa kijinsia niongelee...

(Hapa kegele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, dakika tatu, malizia; kengele ya pili imeshagonga.

WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimia Spika, usawa wa kijinsia tumesemea sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan yeye ni kinara katika haki na usawa wa kiuchumi ambapo jukwaa hilo alilizindua mwaka jana tumesema, andiko linakamilika maana yake ni kwamba ukiacha mikopo ya asilimia 10 mmeisemea sana tunakwenda kuboresha tutaongea na Serikali maana yake ni agenda mtambuka.

Mheshimiwa Spika, tutakuwa na haya Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ambapo fedha zitakuja, wadau wanatuunga mkono, tutakuwa na madirisha ya posta yanaendelea kuwepo, tutakuwa na mikopo mingine ile ya Women Development Fund iliulizwa hoja hapa sio kwamba umefutwa ilitekelezwa kutoka mwaka 1996 hadi 2017, kukatokea changamoto fulani zikahitaji mwongozo utengenezwe, mwongozo unakamilika Serikali itatoa maelekezo jinsi ya kupata fedha na kuendelea kutoa hiyo mikopo kwa ufanisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, masuala ya uwezeshaji kiuchumi katika usawa wa kijinsia yanazingatiwa sana na kufika mwezi wa Julai tutakuwa tumeshaweza kuzindua andiko hili ambazo tumeagizwa na Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yameulizwa hapa na hapa niseme kwamba wasajili wasaidizi wapo kwenye halmashauri na mikoa yetu walikuwa wanachangamoto ya kukosa fungu la kutekeleza majukumu yao lakini mwongozo wa uratibu wa pamoja na mashirika hayo umeshaandaliwa na umetoa majukumu kwa mamlaka ya Serikali za Mitaa kuratibu ufuatiliaji wa miradi inayotekelezwa katika mamlaka hiyo. Natoa rai kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa kutenga fungu kwa wasajili hawa ili waendelee kutekeleza majukumu yao ya uratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mambo ni mengi sana lakini kama vita hii tumeikubali ya kuliokoa Taifa letu naomba halmashauri/full council zikae kwenye usukani, taarifa ya kila mwezi inayokuja ikijadiliwa kwa mapana kama ilivyojadiliwa kwenye Bunge lako tukufu, hawa wakatili sio kwamba hawana akili wanajua vizuri wataondoka wenyewe.

Kuhusu suala la ukatili wa mitandaoni tumeshasema tunaandaa sasa kikosi kasi kimeshaandaliwa na sheria itafanyiwa mapitio, sheria zetu huenda ni nzuri sana miaka 30 ni mingi mno lakini saa enforcement yake inategemea mwitikio wa jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tathmini ya MTAKUWWA itakapokuja itatuambia kama ni suala la kisheria hatutasita kulileta Bungeni mje mlijadili tuone tunafanyaje, lakini wakati huo jamii yetu twende tukaifungue kwa nguvu zetu zote unatokea ukatili vyumbani kwao sauti zifike hadi vyumbani kwao, mtu afike redio aiweke siting room aseme nimekuja hodi kama ni mtaani watu wasikilize hizi taarifa ili wawe empowered kuweza kuwa na confidence ya kupambana na hayo mambo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo ningetamani kuendelea kusema hadi kesho, lakini naona muda hauniruhusu naomba kuwasilisha na naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, naafiki.