Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Ahmed Mabukhut Shabiby

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Gairo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuwa mmoja wa wachangiaji katika Wizara yetu ya Mambo ya Nje. Kwanza ifahamike kwamba tunapochangia hatuchangii kwamba tunaipinga Serikali au mambo mazuri yanayofanywa na Serikali, kazi ya Mbunge ni kuishauri Serikali, hiyo ndiyo kazi ya Mbunge. Sasa Serikali walichukue au wasilichukue ni juu yao (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunataka tusema tu kwamba mimi naunga mkono hoja hii, lakini tunataka tumshauri mama yetu na Waziri wetu, labda kwanza nianze na hili tu ambazo ameliacha mama la uraia pacha. Uraia pacha ni muhimu kwa nchi yote hata kama kuna kuja hilo neno la hadhi maalum au chochote na tunaposema uraia pacha yule mtanzania atakayepata hiyo passport labda atakuwa na passport mbili, sisi hatuna haja kama mimi sina haja mimi nataka passport ya Tanzania tu inanitosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wengi waliokuwa kule ughaibuni ni wale watu ambao wameenda kutafuta maisha hawajaenda kule kutalii, watu lazima wafahamu hicho kitu, ebu tuzungumze je, hawa wanafunzi wanaomaliza vyuo vikuu au hao watu wanaomaliza shule hapa Tanzania kuna kazi za kuwapa? Hakuna kitu kama hicho, watu wanakwenda kule kutafuta maisha tuchuke kama nchi ya Philipines, Philipines leo inajengeka lakini inapata fedha nyingi sana kutoka kwa hao watu wake ambao wapo nje. Kwa hiyo mpango wowote na Wizara ya Mambo ya Nje haijawahi kufanya Semina ituambie je, kuna shida gani kwenye uraia pacha. (Makofi)

Mheshiimiwa Naibu Spika, kuna shida gani kwenye usalama, kuna shida gani kwenye hiki, hatujawahi kufanyiwa semina sisi Wabunge. Kwa hiyo Mbunge akisimama akizungumzia kitu kama hicho haki yetu lazima tukizungumze kitu kama hicho, lakini uraia pacha kwa watu waliokaa kule, waliopo kule sizungumzii kwa waliopo ndani ya nchi, uangaliwe utaratibu wa aina yoyote hawa watu wapewe uraia pacha kwa sababu wanamaliza hata fedha za Tanzania bila kujua. Mimi nina mtoto labda yupo Marekani au Uingereza raia wakule halafu nimeuza shamba unafiriki mimi simtumii fedha hizo na yeye akapata urithi, kwa hiyo fedha si inakwenda huko nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tuangalie nilitaka kuzungumza kwa kifupi tu kwamba Serikali ijaribu kujipanga vizuri iweke utaratibu kama kwenye vyombo vya usalama, kama kwenye siasa ijue vyote lakini kuwapa uraia ni kitu cha msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la kwangu kubwa la leo Mheshimiwa Waziri amezungumzia habari ya diplomasia pamoja na biashara na kwamba ametuambia anatengeneza sera inayokuja, lakini nataka niseme hii nchi hii sasa hivi Mama yetu Rais yupo katika mpango wa kufungua nchi, lakini ukiangalia sisi tunafungua tu Mawaziri lazima muwe makini sana, sisi tunafungua wapi kuja kufanya biashara Tanzania, lakini hatufungui wafanyabiashara wa Tanzania waende kufanya biashara nchi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni shahidi na nafiriki pale Kariakoo ipo chini ya Jimbo lako, hivyo leo Wachina wanauza hadi vikombe vya plastiki, wanauza karanga, huko ndiko kufungua nchi? Halafu Watanzania tunakatazwa kwenda China, sasa hivi nchi zote mimi sio mfanyabiashara wa kutoka China, sifanyi biashara yoyote kutoka china zaidi ya kuagiza magari naagiza kwa IDC likija baya nawarudishia basi, lakini wapo watu wanaofanya retail, wanaofanya wholesale hizi kweli ni biashara ya kidiplomasia kweli za kufanya wachina kwenye hii nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Waziri wetu wa Mambo ya Nje pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara lazima waangalie hili suala Watanzania leo Wachina wanakuja kama shamba la bibi kila siku wanaingia, lakini Mtanzania hauruhusiwi kwenda China, unaambia uagize kwa whatsApp bidhaa, kwa hiyo aliyekuwa na bidhaa anaweza akaagiza anayetaka kwenda kuanza biashara au anayetaka kupeleka vitu China akauze China haiwezekani kitu kama hicho kwa sababu unajua hivi ni vituko, nchi zote Europe kweli China ni rafiki yetu, lakini angalia wa Europe, angalia India, angalia Dubai, angalia Marekani ukiwa una chanjo unaingia hiyo nchi bila kufanywa chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini China mpaka leo uchanje usichanje hakuna kitu, ndege yetu ya Tanzania imejaribu kwenda mara ya kwanza wakaambiwa kuna watu wana corona, mara ya pili kuna watu wana corona Wachina wenyewe hao hao ndege msileta, lakini KLM inaruhusiwa inakwenda kutoka hapa hadi China dola 14,000, kutoka China kuja hapa dola 7,000 na ndege ya Tanzania imezuiliwa na kila Ijumaa ndege ya Tanzania inakwenda China, lakini inakwenda tu kuchukua mzigo hairuhusiwi kupakia hata mtu mmoja. Sasa huu urafiki au diplomasia ipi! Hebu tuulizane hapa swali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wao wa China kuja Tanzania wanakuja kwa wingi basi hata wangeturuhusu ndege yetu iwapakie wao tu kwa dola 14,000 maana tukipakia watu 40 ndege imelipa, lakini hata hiyo ndege hawataki kupanda wanaenda kupanda KLM sasa hivi naona Ethiopia imeruhusiwa na Kenya Airways nayo imeruhusiwa diplomasia hii ya kibiashara lazima iwe fair wao wafaidike na sisi tufaidike, hiyo ndio diplomasia na lazima pawe na sheria na utaratibu kuhusu mambo ya biashara ya nchi za nje hizo sio biashara ndogo ndogo anazofanya Mtanzania anakwenda kufanya mtu wa nje haiwezekani hicho kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Kariakoo mtu akichukua kontena moja mbili za vitu china ujue ni mara yake moja, mara ya pili mchina anakuja kufungua duka Tanzania, yaani ukionekana tu unafanya biashara pale ya vitu vitu hivi ukileta siku ya pili wanaleta wao. Sasa Watanzania wataendelea kuwa wachuuzi siku zote haiwezekani, mimi ushauri wangu kwa mama yetu aangalie…(Makofi)

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nilitaka kumpa taarifa mchangiaji kwamba Watanzania wengi tunafanya biashara na China na hata kukubali kuchanja chanjo za corona tulitegemea nchi zitafunguka kwenye sehemu zetu za biashara kama China na nchi nyingine zimechanjwa madawa kama ya kwetu kutoka Marekani na sehemu nyingine wanaruhusiwa kuingia Marekani, lakini sisi tuliochanjwa za China, sisi tuliochanjwa hizo dawa tunaonekana bado hatujapona.

Kwa hiyo nilitaka kukupa Taarifa Mheshimiwa kwamba tulichanjwa ili tukubali masharti ili tukubali kuingia China kwa sababu ndio mji wa kibiashara kwa Tanzania.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Shabiby.

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubali taarifa yake, ipo vizuri kabisa.

Kwa hiyo la mwisho nataka kumshauri mama yetu akae na hawa kama wanataka na wao wawe wanaingia huku na sisi waturuhusu na sisi watu wetu waingie kule, kama hawataki na sisi tuwe hatuna imani na chanjo zao sio wao wanafanya biashara na nataka nikwambie wanatumia akili sana mwishoni biashara zote za Tanzania, sisi tutakuwa tutabaki tu kuuza mahindi na maharage, watafanya wao, wao Wachina, watu wa Europe kama anavyosema Mheshimiwa Musukuma wanaruhusiwa kuingia lakini watu wa Afrika hawaruhusiwi kuingia. Kwa hiyo tusipoamka tutakuwa tunawafanyia wao biashara, ahsante sana. (Makofi)