Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya mimi pia kuchangia bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru sana Rais wetu ama kama alivyotajwa mwanadiplomasia namba moja, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya kufungua milango ya nchi lakini pia kuitangaza Tanzania nje ya mipaka ya nchi yetu. Kazi anayofanya ni kubwa na commitment ya Serikali tunaiona kwa kupeleka fedha kiasi kikubwa kwenye balozi zetu, kukarabati lakini pia kujenga majengo mapya ambayo nia ni kuboresha makazi, mazingira rafiki ya watumishi wetu ili wafanye kazi kwa ufanisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii ni muhimu sana kwa mustakabali wa nchi yetu, lakini pia ni muhimu sana kwa sera zetu za ndani. Nasema haya kwa sababu moja, sasa hivi tunashuhudia mabadiliko makubwa ambayo yanaendelea huko duniani, changamoto ambayo inaikuta Ulaya ya Mashariki, Ulaya ya kwa ujumla kama Bara, lakini pia Marekani sisi hatuwezi kujitenga nazo. Vikwazo ambavyo makampuni mbalimbali yanawekewa kwa sababu ya vita ambavyo vinaendelea kule Ukraine sisi hatuwezi kujitenga navyo, tunajua tunawashirika wengi ambao wanajenga miradi mikubwa hapa ambao na wenyewe ni sehemu ya mizozo ambayo inaendelea. Pamoja na kwamba sitawataja kwa majina lakini tunafahamu miradi mikubwa ambayo inaendelea hatuna hakika ya kesho kwa sababu kila mmoja anajipanga jinsi gani ya kumdhibiti mwenzie. Ni kwa kiasi gani siasa zao zinaenda kutuathiri hilo ni swali ambalo tunapaswa kulitengenezea mkakati wa majibu yake hasa tunapoenda kutekeleza bajeti yetu ya mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unafahamu jinsi dunia ilivyogawanyika katika makundi ya Mashariki na Magharibi ambayo ilikuwa ni matokeo ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, lakini tunafahamu nchi zetu zilivyotengwa kwamba huyu atakuwa niwa Mashariki huyu wa Magharibi kutokana na siasa ambazo zilikuwa zinaendelea duniani. Kwa kiasi kikubwa nchi hizi ambazo zimetengwa Mashariki na Magharibi ni kwa sababu ya mlengo wa kisiasa, lakini moja kubwa ambalo tulikuwa tumetengwa tukifahamu kabisa kwamba tupo wapi ni zile nchi ambazo ni za Kusini na Kaskazini, kwa maana nchi za Kaskazini walikuwa ni matajiri, wameendelea kiviwanda na kiteknolojia na nchi Kusini ni maskini ambao hawajiwezi.

Sasa hapa katikati tumefanya vizuri, baada ya kuvunjika kwa ukuta wa Berlin na West na East kuungana tumefanyakazi vizuri katika jina la utandawazi na sisi kwa kiasi kikubwa tumeacha ile misingi yetu ya ujamaa na kujitegemea tukiwa sehemu ya hii Sera ya Utandawazi lakini hiki kinachoendelea sasa hivi hatujui kesho tunaenda kurudi kulekule tulikotoka ama dunia inatufungulia ukurasa gani katika historia ya mahusiano duniani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaishi katika kipindi ambacho tunapaswa kujipanga kwasababu tusipojipanga tutapangwa na katika namna hiyo ni muhimu sasa kurudia ile sera yetu ya kutofungamana na upande wowote ili tujenge uchumi wetu wa ndani lakini mataifa na mahusiano yetu na nchi za nje yajijenge katika namna ya kutusaidia kujibu changamoto zetu za ndani. Na katika hili tunaona dunia inavyonyenyekea inavyohangaika kuhusiana na masuala mazima ya energy, masuala ya gas na rasilimali zingine ambazo Tanzania tunazo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazi kwamba wakubwa wanatuangalia kwa hofu kwasababu wenyewe kwa wenyewe hawaaminiani na move wanazozifanya kuja Afrika zinawafanya wasilale sasa ni kiasi gani na sisi tunajipanga kutumia migogoro hiyo kama fursa kwetu kwasababu fursa lazima ujiandae nayo usipojiandaa nayo fursa itakupita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni wakati sasa wa kuangalia mataifa ambayo tumekuwa na mahusiano nayo ya muda mrefu Taifa kama Iran ambalo tuna mahusiano nayo ya muda mrefu wana ubalozi Dar es Salaam muda mrefu ni sababu zipi ambazo zinatufanya tusifungue ubalozi Iran hawa wenzetu wapo mbali katika teknolojia ya petrol, teknolojia ya gas kwanini hatuoni kwamba ni muhimu sasa wakati umefika wa kubadilishana nao ujuzi na skills katika maeneo ya petrol na gas kwasababu hawana marafiki wengi lakini sisi wachache ambao tupo kwanini tusitumie hiyo kama fursa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili tunapozungumzia Sera ya Nje ni lazima ijibu changamoto za ndoto lazima tuwe na Sera ya Ndani ambayo tunajua inataka kutupeleka wapi. Kwa hiyo, Sera ya Nje lazima itumike kama tool ya kujibu changamoto zetu za ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge lako lilijipa agenda ya kwenda kufanya mapinduzi ya kilimo na tunaona commitment ya Serikali kwa kuongeza bajeti ya kilimo tunaenda kufanya rural transformation, tunaenda kufanya rural empowerment ni kwa kiasi gani mikakati ya Sera ya Mambo ya Nje inaenda kujibu hizi changamoto ambazo sisi tumejipa jukumu kwasababu kama mikakati ya Sera ya Mambo ya Nje haijielekezi kwenda kujibu changamoto zetu vijijini basi kuna walakini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kazi kubwa ya Wizara ya Mambo ya Nje ni kuratibu taasisi za Serikali kwa maana Wizara zote, lakini asasi binafsi na mashirika, jinsi gani na mikakati gani ambayo wamejiwekea ndani, sisi tunatumia sera yetu ya nje kujibu ama ku-facilitate malengo ya ndani, na katika hili tuna suala la kilimo, mifugo lakini uvuvi. Huko teknolojia yetu iko nyuma, ni kwa kiasi gani bajeti yetu ya Mambo ya Nje inaenda kuchukua ujuzi ama inaenda kutuunganisha na watu ambao wamefika mbali kwa ajili ya kubadilishana ujuzi na uzoefu ili ku-transform sekta hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hilo wewe ni shahidi katika kipindi kirefu tulikuwa na sera inaitwa economic diplomacy ama sera ya kiuchumi. Sera hii ni nzuri, lakini inahitaji maboresho makubwa kwa sababu tunapitia mabadiliko makubwa ambayo hatujawahi kupitia katika kizazi chetu, ni lazima tukae, tutafakari domestically tunaenda wapi? Sera zetu zinatuelekeza wapi na kwa namna gani tutumie Sera ya Mambo ya Nje kujibu changamoto zetu za ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, short of that tutaendelea kuwa wasindikizaji wa wenzetu kwa sababu wenzetu wanamalengo, wenzetu wanandoto ambazo kama sisi tutashindwa kupeleka ndoto zetu na kuwatumia wao kama facilitator na kama partner katika kufikia malengo yetu basi tutakuwa sehemu ya kufanikisha malengo yao ambayo wanakijiji wetu, wananchi wetu hawatafaidika na hali hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hilo wewe ni shahidi, unafahamu diplomasia yetu wakati wa vita baridi, mashariki na magharibi. Kuna Taifa dogo sana ambalo katikati ya vikwazo vikubwa liliweza kujenga shule nne za kilimo pale Kibiti, Ruvu, Ifakara na Kilosa. Shule hizi zilikuwa specific kwa ajili ya kilimo na Taifa hili kwa kweli litaendelea kudumu kwenye fikra na maono ya Watanzania wengi na ndiyo maana Watanzania wengi walimlilia Fidel Castro kwa sababu alisomesha watoto wengi maskini katika familia katika kila kona ya Tanzania kupitia shule hizi nne za kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu alijua kama Taifa tunataka tujikomboe kupitia kilimo, alijua kama Taifa wananchi wengi wameajiriwa kupitia kilimo, alijua ili tutoke ni lazima wananchi wetu wale, washibe na ndio maana akatuletea ujuzi, lakini akatusaidia kutujengea shule ambazo sina hakika zina hali gani sasa hivi na nini mikakati ya Serikali kuhakikisha kwamba tunaboresha shule hizi ili ziendelee kuwa alama ya mahusiano kati ya nchi ambazo zinaendelea, nchi ambazo ziko kusini kama zinavyoitwa south cooperation, hiki ni kielelezo kikubwa cha nchi ambazo ziko kusini jinsi gani zinaweza zikashirikiana katika kubadilishana ujuzi, uzoefu lakini tukashirikiana katika maeneo ambayo tunaweza kubadilisha maisha ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu kwamba economic diplomacy kwa kiasi kikubwa imetuletea marafiki. Lakini umefika wakati sasa wa ku-adapt kitu kinaitwa innovative diplomacy, kwa jinsi gani tunatumia ubunifu kama njia ya kufikia mataifa mengine, lakini mataifa mengine kutufikia, kwa sababu tumejikita katika maendeleo vijijini. Ni wazi tunahitaji ubunifu katika viwanda vidogo, tunahitaji ubunifu katika kilimo, tunahitaji ubunifu katika uvuvi, tunahitaji ubunifu katika mazao na hata kupunguza wanaita prost loss harvesting (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu wana teknolojia, wenzetu wana ujuzi, ni kwa kiasi gani sera yetu ya mambo ya nje inaenda kutusaidia kwa kututengenezea food security, lakini kututengenezea ajira kwa wananchi wetu vijijini. Kwa sababu tunasema tunaenda kujikita kijijini, ni kwa jinsi gani mahusiano haya tunayaboresha kwa ajili ya kupunguza tatizo la ajira motivative... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa, kengele ya pili.

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)