Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Donge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Naibu Spika, Bismillah Rahman Rahim, na mimi nikushukuru kwa kunipa nafasi hii kuweza kuchangia katika Wizara hii muhimu, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini halikadhalika napenda vilevile kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mulamula pamoja na Mheshimiwa Balozi Mbarouk na timu yao ya Wizara kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakifanya katika kuboresha diplomasia ya uchumi pamoja na kuhuisha mahusiano mema ya Tanzania ya kikanda na kimataifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, halikadhalika kabla sijaenda mbali naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi kwa kitendo cha uungwana alichokifanya ambacho hakuwa amekipangia cha kuweza kuwahudumia vizuri wale wakimbizi wa Ukraine ambao walikuwa wamekwama kule Zanzibar wakati kwao lilipotokea lile tatizo la vita na wakawa hawana jinsi isipokuwa wabakie Zanzibar, na katika hili pia napenda kuishukuru Wizara kwa sababu Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Tanzania ndiyo ilishirikiana na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi kuweza kuwahudumia wale wakimbizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo nimpongeze vilevile ndugu yangu Balozi Simbachawene kwa jitihada zake ambazo alizifanya hivi karibuni na kitendo kile kimeonesha mfano wa Mabalozi wetu kwamba wanaweza wakafanya kazi nzuri katika hali ya dharura. Kuna vijana ambao walikuwa wavuvi wetu kule Zanzibar, walipata tatizo baharini na wakaenda wakaokotwa Kenya. Lakini ubalozi wetu wa Kenya ulifanya kazi kwa haraka na vijana wetu wale wakashughulikiwa, wakahudumiwa, wakalazwa na wakasafirishwa mpaka Zanzibar kwa muda muafaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hiki kinatufundisha kitu, kitu gani tunasoma hapa; kwamba ni muhimu Wizara, Mheshimiwa Waziri Mulamula tutenge fungu la fedha za dharura katika Mfuko wetu wa Maafa ambao unaweza ukahudumia majanga kama haya ambayo hatuyategemei kutokea wakati wowote ule. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini halikadhalika naomba sasa niende katika diplomasia ya kiuchumi ambayo wenzangu pia wamezungumzia. Diplomasia ya kiuchumi kabla sijazungumzia hapa nafikiri kwanza nipeleke pongezi zangu kwa Mama Samia kwa sababu yeye ameonesha kivitendo na kiuhalisia umuhimu wa diplomasia ya kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunakumbuka kwamba Tanzania ikiwa ni kama nchi inahitaji tuzidi kuifungua. Tayari imefunguka kwa sababu kazi ya kuifungua tofauti na wenzetu wanavyozungumza hapa Tanzania imefunguliwa na toka Rais wa Kwanza Baba Nyerere, akaja Mheshimiwa Mkapa, Ali Hassan Mwinyi, amekuja vilevile Jakaya Mrisho Kikwete, Magufuli na sasa hivi Mama Samia tunaendelea kuifungua nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, siyo kwamba labda nchi ilikuwa imekwama haijafunguka, lakini sasa hivi Mama Samia amekuja katika utaratibu ule mpya ambao mwenzangu amegusia hapa, ile innovative diplomacy kwamba issue ya royal tour imekwenda kuifungua na siyo kuitangaza tu Tanzania, lakini imekwenda kuifungua kiuchumi na ku-unlock zile fursa za maendeleo na kiuchumi ambazo zilikuwa kidogo zimekwama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika hili naomba tu Wizara sasa mama ameanza na mabalozi wetu waichukue hii royal tour katika hatua ya pili. Tungetegemea sasa hivi mwakani tukija tukikutana hapa, tuje tutoe taarifa ya ongezeko la makongamano ambayo yamefanyika katika nchi mbalimbali kutokana na wenzetu hawa mabalozi katika maeneo yao ambayo tutakwenda kupima kutokana na ongezeko la wageni ambao wameongezeka katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kuongelea suala zima la ushauri katika maeneo mbalimbali hasa kwa upande wa Zanzibar kwa sababu royal tour bahati nzuri ime-reflect Zanzibar vizuri sana. Sasa wakati royal tour inaongea vizuri kuhusu Zanzibar, nafikiri ni muda muafaka sasa tuongeze wigo wa uwakilishi wa ubalozi na watendaji au Maafisa Ubalozi katika balozi zetu mbalimbali duniani ili tuongeze vivutio au tuongeze wigo wa fedha za maendeleo ambazo zinakwenda Zanzibar kupitia balozi zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano hivi sasa watalii ambao wanakuja Tanzania ni kama theluthi moja, hata haifiki vizuri ambao wanakwenda Zanzibar. Sasa kwa kutumia balozi zetu hizi twende tukahamasishe balozi ziweze kufanya kazi za kuweza kusaidia wigo wa kuimarisha maendeleo ya Zanzibar. Lakini pia naomba jambo lingine la muhimu tukaongeza wigo wa wawakilishi katika mikutano yetu ya kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika uwakilishi wa mikutano yetu hii kuna mikutano mingi ambayo Tanzania imeridhia, mfano kuna UNCC-COP yaani Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi, kuna United Nation Conference on Biodiversity, kuna United Nations on Control and Combat Desertification kuna mikutano ya trades ya kibiashara, kuna mikutano mbalimbali ambayo tumeridhia kama Tanzania. Lakini uwakilishi wa Zanzibar hauko vyema na hata tunapokwenda kuwakilisha sijaona kama kuna mkutano ambao Chief Negotiators amekuwa ni Mzanzibar, lakini always Chief Negotiators wanatoka upande wa pili wa Muungano, sasa na hii wakati mwingine kidogo inaminya maendeleo au zile fursa za uchumi kwa upande wa Zanzibar. Kwa hiyo, naomba hili tukalisimamie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, halikadhalika pengine twende mbali zaidi kwenye masuala ya sera, kwa sababu foreign policy ya Tanzania ina-reflect vilevile United Republic of Tanzania. Sasa iko so generic kiasi kwamba haioneshi Zanzibar hasa inakuwa reflected vipi katika policy ile. Kwa hiyo, naomba Waziri ikiwezekana japokuwa sera yetu ni ya mwaka 2015 lakini tuna uwezo wa kuifanyia marekebisho mapema tukaangalia sasa hivi na Zanzibar ina-fit vipi katika maeneo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kwenye mikutano hii kama kuna Chief Negotiators basi kuwe na Deputy Chief Negotiators ambaye atatoka upande wa pili wa Muungano. Kama Chief Negotiators atatoka Zanzibar basi msaidizi wake atoke Tanzania Bara, halikadhalika kama atatoka upande wa Bara basi msaidizi wake atoke Zanzibar. Lakini halikadhalika katika mabalozi pia siyo lazima tufate utaratibu ambao upo sasa hivi duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile sisi tuna Muungano na Muungano wetu ni very unique, tunaweza tukaamua sasa balozi akawa na msaidizi wake. Kama balozi atatoka Tanzania, msaidizi balozi atoke Zanzibar. Na hii itaisaidia Zanzibar kuweza kujitangaza zaidi na kuweza kutengeneza fursa nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho kuna mikataba miwili hii ambayo ina reflect kibiashara; kuna mkataba mmoja unaitwa Basel Convention ambao ni International Treaty on Control of Transboundary Hazardous of Waste and their Disposal; halafu kuna mkataba mwingine wa sites ambao ni Convention on International Trade in Endangered Species; mikataba hii yote ni mikataba ya kibiashara. Sasa ombi langu kwa sababu ni ya kibiashara hii, sekta ambazo zinatekeleza hii mikataba zote ziko Tanzania Bara kwa upande wa Basel Conventions sekta ambayo inahusika ni NEMC kwa Bara na kwa upande wa sites ni Maliasili.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba tu kwa sababu hizi Mzanzibar akitaka kusafirisha vyuma chakavu au akitaka kusafirisha hizi aina za wanyama ambazo ni adimu inabidi aje Dodoma, aje afuatilie vibali. Kwa hiyo, inapoteza muda na inaingiza gharama zaidi. Naomba tu mikataba ya namna hii tuangalie uwezekano wa kuwa na uwakilishi wa zile institutions za Zanzibar ambazo zinaweza zikatoa vibali vilevile.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kama NEMC kuna ZEMA kule Zanzibar inaweza ikafanya kazi hiyo, lakini halikadhalika kwa upande wa Maliasili na Zanzibar vilevile kuna Idara ya Misitu na Maliasili Zisizorejesheka inaweza pia ikafanya kazi hiyo. Kwa hiyo, naomba tukaangalia uwezekano wa kuweza ku-reflect hizi taasisi nazo kwa hii mikataba mbalimbali...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele ya pili.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naomba kuunga mkono hoja asilimia mia moja.