Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Kenneth Ernest Nollo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nikushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika Wizara hii ya Mambo ya Nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa dhati nianze kuipongeza Serikali kwa namna ilivyoahidi mwaka jana kwenye bajeti iliyopita kuhusu kufungua ubalozi mdogo pale Lubumbashi, ila vilevile niipongeze kwa kufungua sasa ubalozi Indonesia. Indonesia sasa ni nchi ambayo inaelekea kuwa nchi ya nne katika kuwa na uchumi wa kilimo. Kwa hiyo, ni jambo zuri na naipongeza Serikali kwa dhati.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niongelee habari ya sera ya mambo ya nje na wataalam katika masuala ya diplomasia wanasema sera ya mambo ya nje ni kitu kinachoishi yaani sera ya mambo ya nje ni kitu kinachoishi, kwa hiyo, sera zetu katika miaka ya 1980 miaka ile tunafanya ukombozi wa Afrika wakati wenzetu bado hawajapata uhuru haziwezi kulingana na leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mabadiliko yametokea katika nyanja hizo na sera ya mambo ya nje inabadilika kila wakati, inabadilika kutokana na mazingira ya dunia, lakini vilevile inabadilika kutokana na namna ya uongozi unavyokuwa madarakani. Lakini Tanzania nataka niseme tumekuwa vinara wazuri katika sera ya mambo ya nje na kikubwa zaidi ambacho tumeshikilia ni kuhusu suala la kutokufungamana na upande wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nitoe maoni yangu binafsi kwamba kumekuwa na maneno wakati mwingine yanatoka ndani ya Serikali kwamba miaka sita iliyopita nchi yetu kama ilikuwa imejifunga yaani kwamba sasa nchi yetu ilikuwa imefungwa, yaani haina uhusiano na nchi zingine na bahati mbaya niliwahi kunukuu hata balozi mmoja anasema sasa Tanzania inafungua milango yake baada ya kuwa na siasa ambayo ilikuwa imejifunga na international community.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kama nchi tuwe na msimamo, ni balozi gani tulifunga kwamba tumefunga ubalozi kutokana na ugomvi huo? Ni balozi gani tulimfukuza kwamba sasa kutokana na hili tumekufukuza, tumekuondoa. Kwa hiyo, tumekuwa tunajibebesha maneno kana kwamba nchi yetu iliingia kwenye mgogoro mkubwa wa kimataifa na tukafunga kila kitu, kitu ambacho si kweli. Biashara zimeendelee kama kawaida, si kwamba sasa ndiyo tumeanza biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme maneno haya, inawezekana tukawa tunabomoa kwa upande mmoja, aidha kwa kutokujua au katika propaganda ambazo zinatoka katika upande mwingine wa dunia. Kwa hiyo, nchi yetu imeendelea na sera madhubuti za kuimarisha hasa hasa uchumi na tulipofika hapa leo ni muendelezo wa kipindi chote, hakuna sehemu ambapo kama ni behewa lilikatika, tunaendelea hivyo hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme wenzangu wamechangia kuhusu diplomasia ya uchumi na kama nilivyosema foreign policy, siasa ya mambo ya nje ni siasa inayoishi. Kazi tuliyonayo sasa ni nchi yetu kuamua namna gani inaweza kukuza biashara kati ya mataifa mengine duniani. Mimi nataka niseme kuhusu Pakistan. Pakistan ni Taifa ambalo tumekuwa tunafanya nalo biashara kwa muda mrefu, mwaka 2019/2020 biashara yetu kati ya Pakistan ilikuwa kati ya dola bilioni 69 sisi tuliuza Pakistan na Pakistan nao waliweza kuuza kwetu bilioni 80.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa bahati mbaya hatuna ubalozi Pakistan. Balozi anayetumika anatoka India lakini na Waziri leo kasema kwamba kati ya India na Pakistan kumekuwa hakuna mahusiano mazuri ya kisiasa. Kwa hiyo, naomba sana Serikali kwamba iongeze, ifungue ubalozi Pakistan. Kenya na Uganda mwaka jana jumla wameuza dola milioni 154 biashara waliyoifanya na Pakistan. Kwa hiyo, kama tulivyofungua Indonesia tufungue na Pakistan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumekuwa na rafiki zetu wa damu katika nyakati mbalimbali, Iran ni mojawapo ya Taifa ambalo tumepita nalo katika nyakati mbalimbali kwa sera ya Mwalimu Nyerere alivyokuwa anatetea haki na unyanyasaji duniani kote. Iran limekuwa ni Taifa ambalo sisi tumesimama nalo katika nyakati mbalimbali, lakini kwa bahati mbaya Iran ni Taifa kubwa japo kama mtu halisemi, haliandiki lakini ukweli unabaki Iran ni Taifa kubwa hapa duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuna Ubalozi Iran, tumefungua Ubalozi Israel, sitaki kusema kwamba kufungua Ubalozi Israel basi na Iran ufungue, lakini kwa umuhimu, kwa undugu wetu wa damu na Iran ni lazima tufungue ubalozi hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naiomba sana Serikali na Mheshimiwa Waziri jambo uliangalie na utumie kwamba sisi hatufungamani na upande wowote na Iran ni sehemu yetu muhimu kwa maana ya biashara na mahusiano yetu ya kindugu kama nilivyosema.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka niseme kwenye economic diplomacy mambo makubwa yaliyofanyika kwamba ni biashara, sisi tunafanya biashara mbalimbali, tunatoa huduma kwa mfano Tanzania katika bandari yetu ile ni huduma, kuhudumia nchi ambazo hazina bandari.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba Serikali ijipange katika suala hili. Tumeichukua Congo katika East Africa na bahati nzuri sasa mizigo yetu mingi na nchi nyingine/wenzetu majirani walikuwa wanapata sasa imelekezwa kwetu. Lakini bado viko vikwazo vya kufanya biashara kwa maana ya kwamba kwenye mizani yetu kuna ucheleweshaji mkubwa, lakini na efficiency ya bandari yetu. Nilikuona naomba sana jambo hili Serikali iliangalie.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nilitaka niongelee habari ya huduma ya matibabu. Nchi nyingi duniani na hata sisi wenyewe tumekuwa wakati mwingine tunaenda sana katika Taifa la India kwa ajili ya matibabu. Nataka nikwambie na nikupe taarifa kwamba Hospitali yetu ya Benjamin Mkapa sasa inapokea wagonjwa wengi kutoka nchi zinazotuzunguka hasa za Maziwa Makuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba Serikali itangaze kwa makusudi kwamba Benjamin Mkapa sasa ni center of excellency katika East and Central Africa, na tukifanya hivyo tuweke sasa huduma muhimu zinazopatikana kwenye suala la magonjwa kama ya figo, upasuaji na vitu vingine, sasa hospitali inafanya vizuri. (Makofi)

Kwa hiyo, nilikuwa naomba Waziri kupitia pamoja na Wizara ya Afya Hospitali ya Benjamin Mkapa ipewe vifaa vyote na huduma zote stahiki lakini tuitangaze kwamba kwa tangazo maalum sasa hii ni center ya excellency kwa East and Central Africa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka niongeze jambo la sisi kuteuliwa na SADC kwamba tuwe ni supplier wa dawa na ukiangalia kama Waziri alivyosema kumekuwa na wenzetu wanasuasua kutumia Tanzania kama sasa ndiyo procurement agency kwa ajili ya wao kupata dawa. Ni vyema Serikali ikawekeza kwamba badala ya sisi kuwa kama ni dalali basi tuwe na viwanda ili wenzetu wa SADC waweze kununua kwetu. (Makofi)

Kwa hiyo nilikuwa naomba sana na haileti logic kwamba mimi nikakununulie halafu nikuletee dawa kwa kuuzia. Ni bora tuweke viwanda vya kutosha hapa vya dawa ili waje wanunue kwetu badala ya sisi kuwa madalali kwa SADC.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho kabisa, Mheshimiwa Waziri amesema habari ya kwamba sisi sasa ndiyo kitovu cha kupambana na ugaidi katika nchi za Kusini mwa Afrika (SADC). Habari hii ni njema lakini katika hisia si habari njema sana na sijui kwa nini Serikali walilichukua hivi na kutamka lile jambo lile nzito kwamba sisi tumekuwa excellency.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)