Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Vita Rashid Kawawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nitoe mchango wangu mdogo katika Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri Mbarouk Mbarouk, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu kwa kazi nzuri wanayoifanya na wamefanya kazi nzuri katika kutekeleza majukumu yao katika Wizara hii, katika kusimamia na kuratibu masuala ya uhusiano wa kimataifa kati ya nchi yetu ya Tanzania na nchi nyingine duniani na kwa kumshauri vyema Rais wetu katika kazi anayofanya ya diplomasia ya uchumi na ya siasa duniani na kwa ushauri wao mzuri mpaka wamefanya Rais wetu katika kipindi cha miezi 13 na nusu ameweza kutangazwa na gazeti pia la Times kuwa mmoja wa viongozi mashuhuri katika wale 100. Na inaelezwa katika vyombo vya habari kwamba kwa mara ya mwisho Gazeti la Times ambalo lina miaka 99 lilianzishwa mwaka 1923 lilimtangaza Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kuwa kiongozi mashuhuri mwaka 1964 miaka 58 iliyopita, mwaka niliozaliwa mimi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo katika kipindi cha miezi 13 na nusu Rais wetu amefanya kazi nzuri sana na mpaka ameonekana duniani anafaa kupata nafasi hiyo. Ni jukumu letu sisi kuwa proud na Rais wetu na tuendelee kumpongeza sana Rais wetu katika eneo hilo.

Ushauri wangu naomba muendelee kama Wizara kusimamia kwa umakini pia jukumu lenu la kuratibu masuala ya mikataba na makubaliano ya kimataifa, lakini pia muendelee kuratibu biashara ya kimataifa na diplomasia ya uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 ukurasa wa 184 imesisitiza kuhusu diplomasia ya siasa na ya uchumi. Tumeona Rais wetu amehudhuria mikutano mingi ya kimataifa na kikanda katika kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na kuifungua nchi yetu diplomasia ya kiuchumi. Mimi ushauri wangu naomba wananchi wote tuendelee kumuunga mkono Rais wetu Samia Suluhu Hassan, Chifu Hangaya kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuiunganisha nchi yetu na mataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu siyo kisiwa, nchi yetu inahitaji kujumuika pamoja na nchi za kimataifa na nchi za kimataifa pia zinahitaji nchi yetu. Hivyo ushauri wangu pia kwa kuwa Rais anatekeleza kwa vitendo kazi zilizoainishwa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ni muhimu kwa Wizara zingine pia katika majukumu yao yaangalie pia mambo ya diplomasia ya uchumi. Tunafahamu diplomasia ya uchumi tumeipa Wizara hii ndiyo jukumu lake, lakini kuna umuhimu wa sekta zinazoambatana na uzalishaji mali kwa mfano za kilimo, mifugo, uvuvi, viwanda, utalii na huduma, nishati na madini, Wizara zake pamoja na Kamati zake zinazozishauri na kuzisimamia Wizara hizi kuwa na mpango mkakati wa pamoja wa kufanikisha mahitaji ya masoko haya ya nje ambayo Wizara hii inayafanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii tumewapa Mabalozi na ni kweli wanaifanya kazi hii, lakini bila ushirikiano wa sekta zingine wakileta wateja kwa ajili ya masoko yao tunaweza kukawa kuna ugumu.

Mimi nitawapa mfano mmoja tu mfupi, katika Balozi yetu ya Misri mwaka jana ilitafuta soko la viungo vya ndani kama hiliki, mdalasini, pilipili mtama na kadhalika, angalau tani tano ziwe zinasafirishwa kwenda Misri kwa mwezi. Lakini soko lake lilikuwa taabu sana kupata bidhaa zile, maana yake ni kwamba wazalishaji walikuwa hawajaandaliwa, sekta husika ilikuwa bado haijajiandaa.

Sasa tunaomba sana huo ni mfano mmoja, sisi tumesema katika mifugo tuna ng’ombe milioni 36, sasa tuandae wafugaji wetu wasiwe wachungaji tu, wawe pia wanajiandaa kibiashara kwa ajili ya soko la nje. Lakini pia mazao yetu ya kilimo kama mfano niliyoutolea hapa tuwaandae kifikra, tuwape elimu ya soko hili la nje ili tuhakikishe kwamba wanapozalisha wazalishe kwa masoko ya nje, soko la ndani na soko la nje ili waweze kufahamu taratibu ya masoko ya kikanda na masoko ya kimataifa. Kwa hiyo ni muhimu sana sekta hizi zingine tusichoke kutoa elimu na kuwafunza wakulima wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye uvuvi pia tuna bahari kubwa, nakumbuka miaka ya nyuma kuna meli zilikamatwa zinazokuja kuvua katika eneo letu la bahari kuu. Hivyo hivyo maana yake ni kwamba tuna samaki wa kutosha katika soko la nje. Kwa hiyo, ni muhimu pia tuangalie eneo hili hapa la uvuvi wa bahari kuu yetu na kuweza kuzungumza vizuri na hao wanaohitaji samaki wetu ili tuweze kupata soko na kuweza kuuza katika soko la kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi mchango wangu ulikuwa mdogo huo wa diplomasia ya uchumi, nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri, naomba uzingatie ushauri uliotolewa na Wabunge katika maeneo mbalimbali ili muende kuyafanyia kazi na tunaomba mzingatie pia ushauri tulioutoa na Kamati. Tutaendelea kushirikiana na ninyi kuhakikisha tunaisogeza mbele nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)