Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Yahya Ally Mhata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba nichukue nafasi hii mchana huu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara hii Ndugu yangu Sokoine na wafanyakazi wote wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ambao kwa njia moja au nyingine wameshiriki kikamilifu katika maandalizi ya bajeti hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba nijielekeze katika maeneo matatu; kwanza juu ya diplomasia ya kiuchumi na hususan katika Mkoa wangu wa Mtwara ndani ya Jimbo langu la Nanyumbu. Pale ndani ya Jimbo la Nanyumbu tunalo Daraja la Umoja, daraja lile ndiyo kiungo kati ya Mkoa wa Mtwara na Msumbiji, ndani ya daraja lile Serikali yetu ya Tanzania imejenga barabara kwa kiwango cha lami hadi pale darajani. Sasa ukivuka lile daraja ndiyo unafika Mji unaoitwa Ngomano, ukivuka lile daraja na kutoka pale Ngomano unakwenda kilometa 300 unakutana na mji unaoitwa Silver Makua. Sasa pale ndiyo kuna njia panda ya kwenda Maputo na huku unakwenda mji mmoja unaitwa Pemba hadi Mtwara kwa upande ule.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kutoka pale Silver Makua kuja hapa Ngomano ni kilometa 300; bahati mbaya sana barabara ile mpaka leo ni ya vumbi. Lakini kulikuwa na makubaliano ya kimsingi kabisa kwamba Tanzania inajenga kwa kiwango cha lami hadi pale darajani na wale wenzetu upande wa pili wajenge kwa kiwango cha lami. Barabara hii ni muhimu sana katika kuifungua nchi yetu na hasa kwenda Msumbiji hadi South Africa, mfano mwezi Aprili pale Mtambaswala kituo chetu cha TRA kimekusanya shilingi 1,400,000,000; mwezi wa tatu shilingi 1,200,000,000; mwezi wa pili halikadhalika. Kwa hiyo, kuna mapato mengi ambayo Serikali yetu inakusanya kupitia pale.

Sasa rai yangu kwa Mheshimiwa Waziri naomba uendelee kufanya mazungumzo na Serikali ya Msumbiji, wafanye jitihada za makusudi kuweza kujenga barabara ile ya kiwango cha lami kutoka pale Silver Makua kuja pale Ngomano ni kilometa 300 tu kwa kufanya hivi ninaimani kabisa nchi yetu itafunguka na wananchi wetu watafanya biashara sana. Kwani hivi sasa hivi ninavyoongea mbao zote ngumu zinapita pale, hii shilingi bilioni 1.5 ni usafirishaji wa mbao, uingizaji wa magari, uingizaji wa mitambo na mambo mengine mengine. Kwa hiyo, kuna mambo mengi mazuri yakifanyika tutafanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa pili unahusu masuala mazima ya ukusanyaji wa mapato ndani ya Wizara hii. Mheshimiwa Waziri alipokuwa anaeleza hapa ameeleza mapato mbalimbali ambayo Balozi zetu inakusanya kwamba moja ya chanzo kikubwa ni pango, lakini hata Kamati imeeleza vyanzo mbalimbali vya mapato kule Ubalozini na changamoto ambazo Balozi zinakumbana nazo.

Sasa Mheshimiwa Waziri naomba nikushauri; tunalo Shirika letu la Nyumba, Kamati imezungumza tutumie sekta binafsi, tutumie mashirika yetu ya Tanzania yaweze kufanya shughuli hizi. Kwa kusema Serikali ijenge nyumba sasa hivi una Balozi 45 hutaweza Mheshimiwa Waziri. Tunalo Shirika letu la Nyumba, tumefanyiwa semina hapa na Ndugu yetu Msechu tunauona uwezo wao wa lile shirika, kama tatizo ni sera ni suala la kubadilisha ili shirika nalo likawekeze nje ya nchi. (Makofi)

Kwa kufanya hivi Mheshimiwa Waziri utakuwa umefanya mambo matatu makubwa; kwanza utakuwa umeweza ku-save fedha za kigeni. Tunatumia fedha nyingi za kigeni kupeleka nje ya nchi kila mwezi kwa ajili ya kulipia nyumba za wafanyakazi na Ofisi za Kibalozi. Tukitumia Shirika letu la Nyumba fedha za kigeni hazitatumika badala yake tutaweza kutumia fedha zetu za Tanzania kuilipa National Housing.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine Balozi zetu tukijenga kule Ofisi mfano Paris, Mheshimiwa Waziri unaingiza milioni 400 mpaka 600 kwa mwaka kwa sababu Ubalozi wetu wa pale pia tumewapangisha baadhi ya Balozi. Halikadhalika tukitumia shirika letu hili litaweza kujenga nyumba, ofisi na kuweza kupangisha Balozi zingine.

Kwa hiyo, ni wakati muafaka sasa hivi Mheshimiwa Waziri uendelee kutumia shirika letu ili liweze kujenga nyumba zetu kwa kufanya hivyo utaokoa sana. Tumeona mwaka jana hapa miradi ya maendeleo umeshindwa kutumia hata senti tano kwa sababu hukupata fedha na Kamati imezungumza haikutumika hata senti moja kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Mwaka huu umeomba shilingi bilioni nne ni hela ndogo sana, huwezi kujenga, una Balozi 45 na tunategemea kufungua Balozi zingine. Kwa hiyo, lazima tushirikishe sekta binafsi na mashirika yetu ambayo yanajihusisha na masuala ya ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la watumishi; nimemsikiliza sana Waziri kwamba mwaka jana watumishi wengi walikwenda Balozini, hili jambo nimelipenda sana na utaratibu huu Mheshimiwa Waziri uendelee, kila baada ya miaka minne kama sera inavyosema watumishi wanaokwenda waende na wanaorudi warudi. Ila tunazo changamoto, wale wanaorudi mara nyingi hawabakishwi makao makuu, wanaondolewa na kupelekwa sehemu nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii ndugu zangu ni Wizara muhimu sana watumishi wake wawekwe katika eneo moja. Haiwezekani mtumishi umemtoa Ubalozini umem-train, ana knowledge kubwa ya Ubalozi unafika hapa unampeleka kwenye Halmashauri. Unaenda kumuanzisha upya, unapoteza resource kubwa ambayo umeiweka. Sasa lazima hawa watumishi wakifika hapa tusiwaone kama maadui, yaani kuna chuki fulani inajengwa kwamba huyu ameula, ameula nini yeye ni resource, lazima huyu tumlee, tumlee ili baada ya muda tumpeleke tena. Kwa hiyo, kwa kufanya hivyo mimi ninaimani kabisa hii diplomasia ya kiuchumi tunayoihubiri hapa itakwenda na itatekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)