Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru na nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kutujalia nan kutupatia afya njema tukawepo hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kuitangaza Tanzania katika kuongeza diplomasia ya Kimataifa na sasa hivi naona hali ya Tanzania kutambulika katika Umoja wa Mataifa na duniani inakuwa kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru Mheshimiwa Waziri Mama Mulamula, Balozi Mbarouk - Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu. Hii timu yote ilikuwa katika Balozi mbalimbali, kufanya kazi kwao hapa ina maana wamekuja kutuongezea uwezo na juhudi walizozipata, maarifa waliyoyapata ili kutuongezea na sisi kuweza kufanya kazi vizuri katika hii Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge ni mhimili kama mihimili mingine ambayo ni Mahakama na Serikali Kuu na sisi tunapenda watambue kama mhimili wa Bunge lazima utambulike katika masuala ya kimataifa. Kunafanyika mikutano mbalimbali na maazimio mbalimbali ya Umoja wa Mataifa, ya Commonwealth, kuna summit mbalimbali lakini bahati mbaya muda mrefu hatujapata mrejesho. Nitoe mfano katika Umoja wa Mataifa kuna maazimio kila mwaka yanapitiwa iwe maazimio ya usalama, maazimio ya haki za binadamu ikiwemo walemavu, haki za wanawake, haki za watoto, haki za vijana na maazimio mengine ya Umoja wa Mataifa kuhusu United Nations for Climate Change. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini maazimio yale yote hayafiki Bungeni tukayafanyia kazi. Hivyo Wabunge wengi wanapata taarifa zao aidha wasome katika mitandao, lakini je, utaitegemea mitandao wakati saa nyingine katika mitandao kuna taarifa ambazo sio za kawaida, ni fake news. Hivyo tunaamini kabisa wao kukaa kule walete yale maazimio yaliyotoka kule ili yaje katika mhimili wa Bunge, katika kuleta katika mhimili wa Bunge, Bunge itaifanyia kazi na ikiifanyia kazi sheria ile itakuwa inawasaidia kwenda chini. (Makofi)

Mheshiiwa Naibu Spika, nataka ni-declare interest mimi ni mlemavu, lakini ulemavu wangu sio wa kuzaliwa ni wa kupata ajali ya gari. Tuna maazimio yanapita kila mwaka katika Umoja wa Mataifa, lakini kutokana na Bunge halipati taarifa za watu wenye ulemavu tunapata taabu sana ushiriki wetu katika mikutano ya Umoja wa Mataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano leo ukitaka kwenda kuhudhuria mkutano ule wanaleta mlolongo lazima upitie Wizara ya Sera, Kazi, Ajira na kama Waziri haendi basi ina maana watu wengine hata taasisi zingine iwe SHIVYAWATA, CHAWATA watu ambao inabidi nao wakashiriki katika Mikutano ile jibu wanakuambia kwa vile Waziri haendi na ninyi wengine mnakosa fursa, hii kitu lazima muirekebishe.

Nishukuru jana nilikutana na Naibu Katibu Mkuu kwa kweli inabidi nimpongeze Mama Fatma nafikiri ni mama ambaye ana uelewa mkubwa na kutokana na uzoefu aliokuwa nao, amenifariji sana na amefanya kazi ya ziada kuhakiksiha haki za watu wenye ulemavu zinafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya Umoja wa Mataifa ndio sisi ni wanachama Tanzania ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa na kama ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa, sheria na maazimio yale yakifika huku kwetu yanateremka mpaka chini kwa ajili ya kufanyia kazi na kujua haki zao ni nini. Lakini matokeo yake hivi vitu vinapuuziwa huu ni mwaka wa tano Tanzania hatujashiriki katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Watu Wenye Ulemavu. Matokeo yake kama wao hawaendi na huku chini kote watu wanashindwa kufanya kazi. Vyama vya watu wenye ulemavu havihudhurii kwa ajili ya urasimu ambao umewekwa na nataka nitambue tena, Bunge ni mhimili, hatutaki tena mpitie milolongo mingine pelekeni direct katika Bunge, Spika apokee taarifa zetu na azifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sio hivyo itakuwa tunapata taabu, ndani ya Bunge kuna Kamati hizi Kamati inabidi zitumike kwa kupitia mhimili wa Bunge. Kwa mfano, kunapita Mikutano ya Umoja wa Mataifa kutokana na Mabadiliko ya Tabianchi (United Nations for Climate Change), lakini Wabunge hawahudhurii wala Kamati haijui chochote, sasa matokeo yake unajiuliza sisi tumekaa hapa kufanya kazi gani, tunakuja hapa kufanya kazi na wenzetu duniani wanafanya nini. Mwaka 2007 tumekwenda kuridhia haki za wenye ulemavu katika Umoja wa Mataifa Watanzania tulikuwa watano, Kenya alikuja mtu mmoja lakini nimekwenda tena mwaka 2016 Wakenya wako 80. Hivi vitu msivione kama ni vya kawaida vinaturudisha nyuma kiupeo wa maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unapohudhuria Mkutano ule sio unahudhuria kwa ajili ya walemavu kuna masuala ya uchumi, kuna masuala ya ajira, kuna masuala ya elimu, kuna masuala mbalimbali ya maendeleo ambayo sisi tunayakosa tuko katika kisiwa ambacho kinabidi kisiwa hiki kiongezwe kiweze kufanya kazi ya msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mabalozi nimelizungumzia karibu mara mbili kila Balozi ajitathmini katika Balozi zake je, niko hapa kwa kufanya kazi gani? Kazi ya kwanza ya Balozi kuiangalia Tanzania inanufaika vipi na kilimo, inanufaika vipi na uchumi wake na kuitangaza pale na pawepo na ma-desk maalum ya kuitangaza. Nilikuwa nazungumza mimi nakwenda pale New York lakini unakuta desk la utalii halina kazi maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mama ameipeleka royal tour duniani je, kama ma-desk haya hayafanyi kazi hizi royal tour hazitakuwa-sustainable kabisa, hatutaweza kufanya kazi. Ni lazima wajitambue kama wako pale kuisimamia nchi ya Tanzania iweze kuondokana na umaskini twende katika uchumi na uchumi ni ku-share resource baina ya wenzetu na sisi. Kama watakaa pale hawajitathmini basi haina haja ya kuwapeleka watu ambao hawana nafasi katika Balozi zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia suala la mjusi narudia tena. Mjusi Dinosaur ni haki ambalo lipo Ujerumani sitaliacha hili mpaka ufafanuzi upatikane, ule ni uchumi na kama uchumi ule wa Dinosaur ambaye yuko Ujerumani Lindi hatufaidiki na chochote. Si hivyo tu mwanzo nikafikiri ni nchi kumbe ni kikundi/taasisi kimechukua lile Dinosaur wanafanya biashara, wanafanya uchumi mkubwa kuhusu Dinosaur lile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jiulize mapato yanayopatikana ndani ya Serikali ni yapi; tuna royalty gani ndani ya Serikali ni yapi; je, Balozi wetu ambaye yupo Ujerumani anatuambia nini anatupa ripoti gani kuhusu mafanikio ya mjusi wanayoyapata wale vs nchi yangu, mkoa wangu na Lindi yetu nayo ifaidike na mjusi. Haiwezekani, maana yake sasa hivi taarifa tulizokuwa nazo mijusi yote mikubwa sita au Dinosaur makubwa sita yanatoka mkoa wa Lindi, ndege wakubwa 13 wanatoka Mkoa wa Lindi, lakini mpaka sasa hivi pamekaa kimya hakuna ripoti hakuna nini tunapeana tu kila mmoja anajiona mimi kama ni Wizara… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante, ahsante.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Naibu Spika, Maliasili haina miliki ya peke yake ni Wizara ya Elimu na Wizara zingine na Wabunge vilevile tuna haki ya kupambana na mjusi na haki zetu zifanikiwe. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo naunga mkono, ahsanteni sana. (Makofi)