Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ambayo pia mimi ni mjumbe wa Kamati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijasema lolote kwanza nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Waziri na timu yake pamoja na maafisa wote ambao kwa namna moja au nyingine wameshiriki katika kufanikisha hotuba hii ya bajeti. Lakini pia wanafanya kazi nzuri sana ya kupokea wageni, ya kuratibu ziara za Mheshimiwa Rais na viongozi mbalimbali katika Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizi niseme jambo moja nimeona katika michango yetu baadhi yetu Wabunge na mimi kama Mbunge, lakini hasa kama Mjumbe wa Kamati ningependa kuliweka sawa kwa sababu wananchi wanatusikia sasa tusije tukaenda nje ya mjadala katika suala zima la uraia pacha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri sana tukaelewa kama Wabunge kwamba suala la uraia pacha pamoja na kuwa ni jambo la Kikatiba, lakini jambo linalokuja kwenye masuala ya uraia Wizara inayohusika ni Wizara ya Mambo ya Ndani. Kwa hiyo, tusije tukawabebesha mzigo Wizara ya Mambo ya Nje katika jambo hili ambalo kwa kweli tumeshalisema mara nyingi lakini bado linarudi kule kule kwamba ni suala la Kikatiba lakini ni suala la Wizara ya Mambo ya Ndani kama linaamua kufanyiwa kazi katika mifumo ya Kiserikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende pia kutumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kama mwanadiplomasia namba moja, nimelisema hili mara kadhaa jinsi ambavyo anakuwa mwanadiplomasia namba moja kwa vitendo na kuitangaza diplomasia yetu ya uchumi. Tunaposema diplomasia ya uchumi maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba vile ambavyo tunaweza, tukatumia mbinu zote za kidiplomasia kama Taifa katika kutafuta maslahi mapana ya Kitaifa kama vile kutafuta wawekezaji, kama vile kufungua fursa za kibiashara, kama vile kutafuta masoko ya bidhaa zetu. Kwa mfano, sisi tunaotoka Iringa na Njombe tumeona kabisa kwamba tumefungua fursa za mazao kama vile mazao ya misitu lakini pia na zao la parachichi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hiyo ni kazi kubwa sana inayofanywa na mwanadiplomasia namba moja ambaye ni Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama Samia Suluhu Hassan, lakini pia kuvutia wawekezaji na mimi ninasema haya ni mmoja wa wanufaika wa diplomasia hii ya uchumi ambao Mheshimiwa Rais kama mwanadiplomasia namba moja anaitendea haki. Sisi katika Jimbo la Mafinga tuna wawekezaji wengi ambao wamekuja kutokana na Taifa letu kutangazwa kupitia hii diplomasia ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sio hivyo tu kupitia mwanadiplomasia namba moja kama Taifa pia tunanufaika, tunapata mikopo ya riba nafuu, yako maeneo tunapata misaada au kama grants lakini pia tunapata fursa za kimasomo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa uniruhusu nitoe mfano, sisi watu wa Iringa tukiongozwa na Mheshimiwa William Lukuvi kwa miaka mingi sana tumesema kuhusu barabara ya kutoka Iringa kwenda Ruaha National Park, hivi juzi tumeona Benki ya Dunia imetoa mkopo wa riba nafuu wa trilioni 1.2 ambao mkopo huu sio tu kwamba utatunufaisha sisi watu wa Iringa kwa kujenga barabara ile ya kutoka Iringa kwenda Ruaha National Park, lakini pia yako maeneo yatakayonufaika na ungeniruhusu niyataje machache kuonesha jinsi ambavyo mwanadiplomasia namba moja kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje kazi inavyofanyika inatuletea manufaa katika Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkopo huu wa trilioni 1.2 kutoka Benki ya Dunia, pamoja na mambo mengine utaenda kujenga barabara ya Mtwara – Mingoyo – Masasi ya urefu wa kilometa 201; utajenga barabara ya Rusahunga – Rusumo kilometa 92; utajenga barabara ya Songea – Rutukila kilometa 111; lakini pia utaenda kujenga hiyo barabara ya Iringa kwenda Ruaha National Park pamoja na kujenga viwanja vya ndege vya Lake Manyara, Iringa na Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hii ndio maana halisi ya diplomasia ya uchumi kwamba, kupitia ziara hizi mbalimbali, kupitia makubaliano mbalimbali tunafungua fursa za kibiashara, lakini pia fursa za kimikopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona Mheshimiwa Rais alipoenda Dubai Expo 2020 kule, tumeona mikataba na hati za makubaliano 37 zilisainiwa ambazo pamoja na mambo mengine zitaendelea kufungua hizo fursa na hapa mimi kama zao la Wizara ya Mambo ya Nje nipate kupata ufafanuzi kidogo kwamba tunaposema hati na makubaliano watu wengine walikuwa wanajaribu kubeza kwamba hayo si ni makubaliano tu, kumbe katika nyanja ya kidiplomasia huwezi kufanya jambo lolote kabla kwanza hujafanya makubaliano yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, na ndio maana nitumie nafasi hii kupongeza Ubalozi wa Abudhabi pamoja na Dubai kwa kushirikiana na watendaji wa Serikali kufanikisha maonesho hayo ya Dubai Expo, lakini pia nitumie nafasi hii kumpongeza Balozi Mbelwa Kairuki ambaye kupitia majadiliano na makubaliano mbalimbali Taifa letu limekubaliwa kuingiza muhogo na soya katika soko la China. Huwezi tu ukaingiza hizo bidhaa bila kufanya makubaliano mbalimbali, yote haya yanatokana na kazi nzuri inayofanywa katika dilpomasia ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uniruhusu pia kupongeza kwa kufunguliwa Ubalozi wa Lubumbashi, nakumbuka toka nimekuwa Mbunge hapa mwaka 2016 na wewe ukiwa Mwenyekiti wetu kuanzia kwenye Kamati, tumeshauri sana na hatimaye Ubalozi mdogo Lubumbashi umefunguliwa. Hii ni manufaa kwetu ikiwemo watu wa Iringa ambao pale Lubumbashi kwenye mpaka wa Mokambo zaidi ya malori 400 kwa siku yanaingia katika nchi ya Congo. Kwa hiyo, tumefungua masoko mbao zetu kutoka Mafinga zimepata soko Lubumbashi. Na sasahivi DRC imekuwa sehemu ya Afrika Mashariki, tuna imani kwamba, tutaendelea kunufaika na soko hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo nitoe ushauri, kazi yetu ni pamoja na kushauri; pamoja na changamoto za kidunia baadhi yetu wamesema iko sasa sababu ya kufikiria kama Serikali na mifumo mingine ya Kiserikali kuona umuhimu wa kufungua ubalozi katika nchi ya Iran. Iran imepiga hatua sana katika suala la textile industry na sisi hapa tunalima pamba, tunaweza tukajikuta kwamba tunafungua fursa sio tu za kibiashara, lakini pia fursa za kugawana uzoefu katika eneo kubwa la viwanda, hasa hususan viwanda vya nguo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wa pili; niishauri sana Wizara mambo mengi tukitaka tufanikiwe tupitie zile tume za ushirikiano za pamoja kwa maana ya kwamba tume za kudumu kwa maana ya zile JPC. Kupitia hizi mambo mengi yatanufaisha nchi yetu na Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wa tatu; kama Wizara ningeshauri sana Wizara i-take lead katika kuhakikisha kwamba kama Taifa tunanufaika na mifuko mbalimbali katika dunia inayotoa fedha katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alishiriki kule Glasgow kwenye mkutano wa mazingira na aliwaambia wakubwa wa dunia ambao kwa sehemu kubwa wanaongoza katika kuchafua mazingira kwamba waheshimu zile ahadi zao na kwa uchache nitaje, kuna mifuko kama Green Climate Fund, Africa Climate Change Fund ambao uko chini ya Benki ya Maendeleo ya Afrika, kuna Adaptation Fund, kuna mifuko kama Climate Investment Fund, na kadhalika iko mifuko mingi.

Kwa hiyo, niiombe Wizara, Rais wetu ameshiriki kule kikamilifu na kwa kweli alikuwa ni miongoni mwa viongozi waliohutubia. Sasa Wizara itusaidie katika kuratibu kama Taifa tunaweza tukanufaika vipi na fedha hizi za mifuko ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi watu wa Iringa, watu wa Mafinga, watu wa Njombe, tunalima, kwa mfano mwaka huu kutokana na matatizo ya mvua tutaelekeza kilimo chetu kwenye kilimo cha mabondeni, kilimo cha vinyungu kwa hiyo, tukinufaika na mifuko hii itakuwa ni fursa kwetu nzuri...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Chumi kwa mchango mzuri.

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya naunga mkono hoja na kama kawaida nasema Mungu atubariki sote na Taifa letu. (Makofi)