Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Abeid Ighondo Ramadhani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia na mimi fursa ya kuchangia katika Wizara hii muhimu ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayofanya, lakini pia kwa usikivu mkubwa sana, Waziri huyu amekuwa msikivu pamoja na Naibu wake, tunapokuwa na changamoto mbalimbali kwa kweli huwa wanatusikiliza kwenye Kamati na hata nje ya Kamati na mimi naendelea kuwaomba kwamba, tabia hiyo waiendeleze wasibadilike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nichukue pia fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kazi yake nzuri anayoifanya katika kuitangaza nchi yetu kimataifa na lazima tukubali kwamba Tanzania sio kisiwa, nchi yetu sio kisiwa kwa hiyo, lazima tu-interact, lazima tujue fursa zinazopatikana nje ya nchi yetu na lazima tuzichangamkie. Kwa hiyo, Rais wetu anapofanya juhudi hizi za kwenda huku na kule lazima tumtie moyo na lazima tumuunge mkono. Na kimsingi kwa yeye ambaye ndio tunasema ndio first diplomat yale anayoyafanya kule watendaji lazima wayachukue na wayatafsiri katika maisha na katika mazingira ya nchi yetu na fursa zinazopatikana kule lazima wazitafsiri katika mazingira halisi ya Kitanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa lazima twende mbali kidogo, mimi nilikuwa nataka nijikite kidogo kuelezea faida tunazozipata ama ambazo tumeshazipata kama nchi kufuatia ziara alizofanya Mheshimiwa Rais wetu nje ya nchi na hapa nilitaka pia niombe jambo moja, Waziri labda atakapo-wind up atanisaidia, pale tunaposema mama yetu, tunapomtambua Mheshimiwa Rais kama mama, yes I real appreciate she is our mother, ndio mama yetu, ni mlezi wetu, lakini kama kiongozi wa nchi nilikuwa najaribu kujiuliza mwenyewe kwa nini tusimuite Mheshimiwa Rais wa nchi au Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?

Mheshimiwa Naibu Spika, tuitofautishe na mama; ndio ni mama kwa kuwa ni mama yetu ni mlezi wetu, lakini tumtambue kwamba ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Nitaomba hili kidiplomasia ikiwezekana Mheshimiwa Waziri hapa atupe muongozo sahihi. Ni mama yetu, Mheshimiwa Rais wetu anapenda tumtambue kama mama, lakini kimamlaka imekaaje? Kwa nini tusitambue kwamba huyu ni Mheshimiwa Rais kwa title yake kama Rais kwa nafasi yake?

Mheshimiwa Naibu Spika, kweli mfano Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje wewe ni mama, tuseme mama yetu Waziri wa Mambo ya Nje? Mimi nadhani tumtambue Mheshimiwa Rais kwa nafasi yake ya Urais. Tuiheshimu ile mamlaka aliyonayo kama mkuu wa taasisi ya Urais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nikizungumzia kwa uchache faida ambazo nchi imepata kufuatia ziara za Mheshimiwa Rais nje ya nchi; kwanza tumepata miradi mingi sana ya maendeleo kwenye maeneo mbalimbali, kwenye sekta mbalimbali. Tumepata miradi mingi kwenye sekta ya afya, kwenye sekta ya kilimo, kwenye maji, kwenye elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sote tumeona tumepata vyumba vya madarasa zaidi ya 15,000 nchi nzima. Haya yalikuwa ni matokeo ya ziara za Mheshimiwa Rais alipokwenda kutembelea nje ya nchi yetu ama kutembea nje ya nchi yetu, lakini pia tumepata wawekezaji kwenye sekta mbalimbali waliokuja nchini baada ya Mheshimiwa Rais kwenda wameona fursa ambazo nchi yetu inazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama haitoshi utalii umeongezeka, watalii wameongezeka na tunafahamu sekta ya utalii inavyoiingizia nchi yetu kipato au pato lililotokana na watalii ni fedha nyingi tunazopata kwa hiyo, lazima tuendelee kuyatafsiri mambo haya katika mazingira halisi sasa ya Kitanzania, ili watu waone umuhimu wa ziara hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tumepata mikopo ya riba nafuu kutoka nje ya nchi, lakini pia kufungua mahusiano ya kidiplomasia ya nchi yetu na nchi nyingine. Tunafahamu hapa katikati mambo yalikuwa magumu kidogo, lakini sasa hivi tunaona mahusiano yalivyokuwa mazuri, tunapata wageni, tunapata wawekezaji, diplomatically nchi yetu sasa hivi iko vizuri kiuchumi na hata kijamii. Kwa hiyo, lazima tuyathamini mambo haya na tuendelee kuyasema na tuendelee kumpa moyo Mheshimiwa Rais katika ziara hizi anazozifanya na watendaji sasa wayachukue mambo haya, wayatafsiri katika mazingira yah uku chini ili wananchi waendelee ku-support na kuelewa haya mambo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na moja ya fedha za miradi ambazo tumezipata, ametangulia kusema Mheshimiwa chumi hapa, kuna fedha ambazo tumezipata zinaelekezwa kwenye miradi mahususi. Mathalani zile ambazo zinakwenda kujenga, kuna fedha hizi ambazo tumepata Euro milioni 450 sawa na shilingi za Kitanzania trilioni 1.17 zinazotoka Umoja wa Ulaya. Fedha hizi zinakwenda kwenye kutekeleza ujenzi wa viwanja mbalimbali vya ndege hapa nchini, kuboresha hata ule uwanja wetu wa ndege wa kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere - Terminal II pale, uwanja wa Kigoma wa ndege, uwanja wa Shinyanga na vingine nchini. Kwa hiyo, vitu hivi tusipovieleza hapa haya anayoyafanya mama hayawezi kueleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna hili ambalo ni la hizi barabara, kuna barabara kubwa nne ambazo zinaenda kuboreshwa; kuna barabara hii ya Iringa – Msembe kilometa 104; kuna barabara ya Songea – Rutukila kilometa 111; barabara ya Rusahunga – Rusumo kilometa 92; kuna barabara ya Mtwara – Mingoyo – Masasi kilometa 201. Hizi fedha ni nyingi na hizi barabara ni muhimu kwa uchumi wan chi yetu, hatuwezi kuzungumza uchumi kama hatuna miundombinu mizuri ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nilifikiri niliseme hili ili hasa watendaji wa Wizara na hata…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ighondo ahsante, kengele ya pili.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, japo muda umekuwa mdogo, lakini na viwanja vyetu vilivyoko nje ya nchi huko viendelee kujengwa. (Makofi)