Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu na pia nakushukuru wewe kiongozi wangu kwa kunipa nafasi ya kuzungumza katika Bunge lako kuchangia Wizara hii ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watumishi wengine wote wakiwemo Mabalozi wetu ambao wanatuwakilisha katika nchi mbalimbali. Ninaamua kuwapongeza kwa sababu hivi karibuni kulikuwa na kongamano la biashara la nchi zinazozunguka Ziwa Tanganyika, Mheshimiwa Waziri uliwaruhusu Mabalozi wako wakaja kushiriki katika kongamano lile ambalo kwa sehemu kubwa lilikuwa linazungumza diplomasia ya uchumi, kwa hiyo nakupongeza sana wewe pamoja na Mabalozi wote wale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu imepita katika vipindi tofauti katika Sera zetu za mambo ya nje mtakumbuka mara baada ya uhuru sera yetu ya mambo ya nje hasa ilijielekeza katika ukombozi wa nchi za Afrika na baada ya hapo sera yetu ikajielekeza katika kuunda Umoja wa Afrika tukaanza na OAU baadaye kuja na AU na katika miaka ya 1990 tulipojielekeza katika sera za uchumi sasa ndiyo tukaanza kutazama diplomasia ya uchumi katika nchi za Afrika na hata nchi za Ulaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kuzungumza hapa ni kwamba sasa hivi dunia inazungumza uhusiano wa kimataifa ikiweka uchumi mbele na sisi kama Watanzania na hasa kwa sababu tunazo changamoto nyingi za kiuchumi zinazohitaji maendeleo ya watu wetu ni lazima diplomasia ya uchumi ipewe nafasi ya kwanza kabisa kuliko mambo mengine yote na hili naona Mheshimiwa Rais amelielewa na analisimamia vizuri na ndiyo maana utamuona yuko katika shughuli mbalimbali, anakwenda Dubai huko, zote zile ni kuhangaika na shughuli za diplomasia ya uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo ambalo linanisikitisha sana ni kuona kwamba tunakwenda kuhangaika na mambo ya mbali na yaliyo karibu tunayaacha. Hivi karibuni East African Business Council (Baraza la Biashara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki) lilitoa ripoti yake, katika ripoti hiyo imeonesha mwaka 2018 nchi jirani yetu DRC ilifanya biashara ya kuingiza bidhaa mbalimbali nchini kwao zenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 7.4; mwaka 2019 wamefanya biashara ya kuingiza nchini mwao bidhaa mbalimbali zenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 6.7; hizi ni fedha nyingi sana, lakini tujiulize sisi tunaohangaika na diplomasia ya uchumi katika kuingiza bidhaa hizo sisi kama Tanzania tumeingiza kiasi gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, katika taarifa hiyo ya Baraza hili la biashara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inasema China imekuwa nchi ya kwanza ambayo imeingiza bidhaa kwa 31.9%; South Africa imekuwa nchi ya pili 16%; Zambia imekuwa nchi ya tatu 13.32%; Kenya imekuwa nchi ya nne, sisi tuko kama nchi ya saba kwa 6.9% na sisi ndiyo tunaopakana na DRC. Huu kwa kweli lazima tuseme ni msiba mkubwa katika diplomasia ya uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jirani tusihangaike na ya Dubai tusihangaike na ya Ulaya jirani DRC kuna soko kubwa la kila bidhaa ambayo tuliyonayo hapa. Ukipeleka mbuzi wananunua, ukipeleka ng’ombe wananunua, ukipeleka kuku wananunua, ukipeleka cement wananunua, ukipeleka mabati wananunua kila kitu tatizo liko wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto zinazotukuta kutokana na hilo la kwanza mazingira yetu siyo rafiki, hatujatengeneza mazingira rafiki ya kibiashara kuanzia kwenye shughuli za kikodi mpaka za kidola hilo kongamano juzi walikuwa wanalaumiwa watu mbalimbali mpaka idara ya uhamiaji imelaumiwa. Kuna Mkongo mmoja alikuwa anashiriki kwenye kongamano hilo akasema siku moja aliambiwa na Afisa Uhamiaji kwamba na nyinyi kila siku mko huku hamtulii kwenu? Yaani mtu anawaletea fedha za biashara unamwambia hamtulii kwenu wakati dunia watu wa namna hiyo wanawapokea. Kwa hiyo ninachotaka kusema ni kwamba lazima tuwe na mazingira rafiki yanayowezesha kufanya biashara na jirani zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni urasimu katika nyaraka, vibali na mambo chungu nzima; la tatu ni kuchelewa kufanya maamuzi na hili jambo linai-cost nchi yetu kwa kiasi kikubwa sana, watu wengi wanaogopa kufanya maamuzi.
Mheshimiwa Naibu spika, naweza kutoa mfano mmoja tu leo tuna meli imekaa miaka saba na hiyo meli inatuunganisha na nchi za Zambia, nchi za DRC haitembei, nyingine ina miaka minne, hatuna meli hata moja watu hawafanyi maamuzi meli zimekaa kukarabatiwa tu tena kwa gharama ndogo zimekaa hapo meli hakuna meli hata moja. Nchi yetu moja ya jambo linalotu-cost ni watu kutokufanya maamuzi kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni miundombinu na katika hili nataka nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha Bwana Mwigulu Nchemba na Waziri wa Ujenzi. Mimi nimefurahi sana maamuzi mliyoyachukua ya kumsaidia Rais katika reli inayokwenda DRC badala ya kupita Kigali inapita Uvinza inakwenda Msongati inakwenda mpaka Kindu kule Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, lazima tuangalie miundombinu hii tunayoiweka ili kufanya biashara na wenzetu tunaijenga kwa faida ya kiasi gani kwa nchi yetu na kwa gharama nafuu, hapa mimi nakupongeza sana kwa uzalendo wako Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Waziri wa Ujenzi. (Makofi)
Kwa hiyo, ninachotaka kusema kwamba tunajielekeza katika diplomasia ya uchumi ili itutoe katika hali hii tuliyonayo na muelewe kwamba kiwango chetu cha kukopa na kukopesheka kinategemea namna sisi tunavyofanya biashara na nchi nyingine na kuingiza foreign currency.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie na suala la Kiswahili; sisi tumekuwa mabalozi wazuri wa kutetea matumizi ya Kiswahili, lakini Kiswahili hiki ni ajira, nikuombe Mheshimiwa Balozi ambaye pia ni Waziri wa Wizara hii utusaidie utakapokuja hapa kufanya majumuisho ni kiasi gani vijana wetu waliosoma Kiswahili wamepata nafasi ya ajira nje ya nchi kwenye vyuo mbalimbali kwenda kufundisha lugha ya Kiswahili. Tusiseme tu tunataka watu wazungumze Kiswahili lakini pia tunataka tunufaike na hicho Kiswahili ambacho tunakifundisha na tunakijua vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya naunga mkono hoja. (Makofi)