Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi, kwanza kabisa nianze kwa kusema naunga hoja iliyoko mezani.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kipekee kabisa nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amejitahidi kuwa mwanadiplomasia namba moja kuhakikisha anaendelea kuiunganisha nchi yetu na nchi zingine ili kuleta maendeleo kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utajielekeza kwenye diplomasia ya uchumi na kwenye diplomasia ya uchumi nitaongelea mambo mawili; nitaongelea masoko, lakini pia nitaongelea zile nchi ambazo zina masoko, lakini tunaendelea kupitia vikwazo vingi ambavyo tunatamani kuona Wizara hii iweze kutusaidia.

Mheshimiwa Naibu spika, lakini kabla ya kuanza kuchangia mchango wangu nataka mchango wangu ujielekeze kwa kuzingatia Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo ina Sura 10; kwenye Sura ya Saba inaongelea kwenye Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye sura hiyo nataka nisome kwenye ukurasa wa 184 ambao Chama cha Mapinduzi kiliielekeza Serikali hii katika kipindi cha miaka mitano inapaswa kufanya nini. Katika kipindi cha miaka mitano Chama cha Mapinduzi kinaielekeza Serikali kwenye diplomasia ya uchumi kufanya mambo kadhaa yafuatayo:-

(a) Kukuza mahusiano ya kiuchumi na mataifa, Jumuiya za Kikanda na taasisi zingine za kimataifa.

(b) Kulinda uchumi na maslahi mapana ya Taifa kwa kutumia jiografia na nchi kimkakati una ushawishi wa historia hususan kwenye Ukanda wa Kusini.

(c) Kuhakikisha kuwa balozi zetu zinakuwa kiungo muhimu cha kukuza uwekezaji na upatikanaji wa masoko na bidhaa na huduma zetu.

(d) Kuweka mazingira wezeshi ya kuendelea kuratibu na kuhamasisha ushiriki wa Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) ili waweze kuzitangaza fursa zinazopatikana nchini na kushiriki kikamilifu katika kuchangia maendeleo hususan ya kiuchumi ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nataka ku-quote kidogo kwenye sera ya diplomasia ya uchumi inasemaje? Inasema hivi; diplomasia ya uchumi katika eneo hili pamoja na mambo mengine inapaswa kuwezesha wafanyabiashara kupata masoko na huduma na bidhaa zinazozalishwa na kutaka kukuza katika masoko ya nje katika jambo hili wanapaswa kuonesha ukubwa wa soko la bidhaa na huduma husika na taratibu za kuingia katika masoko hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ziko baadhi ya nchi ambazo zinatumia sana mazao ambayo tunazalisha hapa nchini kwetu ni pamoja labda na mchele ambao unatokana na mpunga, mahindi na mazao mbalimbali ya mikunde na zipo baadhi nchi nyingi tu kwenye ukanda wa SADC ambazo zinatumia mazao hayo. Lakini cha kusikitisha kwa kuangalia hiki kipengele ambacho kinasema balozi zihusike naweza kusema kwamba mwaka jana kulikuwa na mdororo sana wa bei za mahindi hapa nchini kwetu na ikapelekea Serikali kukopa bilioni 50 ili kununua mahindi yale kwa wakulima wetu, unaweza ukaona kwamba hili lilikuwa ni jukumu la Wizara hii wao kuendelea kuzitumia balozi zetu zilizopo nchi mbalimbali ili kuendelea kututafutia masoko kwenye nchi mbalimbali zipo nchi nyingi sana ambazo ziko hapa Afrika zinatamani kupata mahindi tukianza hata na nchi ya Congo yenyewe na nitaeleza hapo baadaye vikwazo kwenye point yangu namba mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini zipo nchi nyingine Kenya wanatumia mahindi kutoka kwetu, lakini pamoja na mazao mengine je, Wizara hii mmewajibika namna gani kuhakikisha mnaendelea kututafutia masoko, imagine hii bilioni 50 ingeweza kutumika kwenye mambo mengine, Serikali isingeweza kwenda kununua yenyewe kwa sababu mngekuwa mmefungua wigo wa wakulima wetu, wafanya biashara wetu kwenda kuuza mazao huko sehemu nyingine ikiwa Ilani yenyewe ya Chama cha Mapinduzi ambayo ni chama ambacho kimeweka Serikali madarakani kiliwapa jukumu hili kufanya katika kipindi hiki cha miaka mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nataka kuongelea vikwazo vya kibiashara ambavyo nchi yetu inapata kuelekea kwenye masoko mengine na hapa nataka kuliongelea sana soko la DRC Congo; sasa hivi Congo amekuwa ni mwanachama katika East Africa ni mwanachama wa SADC lakini ni mwanachama wa COMESA, ukiangalia sisi tulijitoa kwenye COMESA kwa hiyo Congo anao wigo mpana sana wa kimasoko sasa sisi zipo baadhi ya vikwazo ambazo tunavipitia kutoka nchi ya Zambia, nataka kurejea kitu kidogo kwenye hi sehemu (b) inayosema; kulinda uchumi na maslahi mapata ya Taifa kwa kutumia jiografia ya nchi kimkakati na ushawishi wa kihistoria hususani kwenye Ukanda wa Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushirikiano wetu na nchi ya Zambia ni wa kiasili kabisa, ni wa kibaiolojia hatukupaswa sisi Wizara yetu kuupuuza, angalia sasa hivi tumetafuta option nyingine ya kuzikwepa vikwazo vya Zambia kwa kupitia Ziwa Tanganyika, tumeziwezesha bandari zetu nyingi kule, tumetumia fedha nyingi sana kuhakikisha namna gani tunaingia kwenye Jimbo la Tanganyika, mimi nasema naunga mkono Serikali kutaka kwenda kufungua hata barabara upande ule kule wa Congo, lakini naweza kusema hii tuitumie kama fursa tu ya kutafuta namna gani tuweze ku-penetrant Congo katika Majimbo 26, lakini hatupaswi kuchukua kile kigezo ambacho tunaona kwamba Zambia wametuzingira, tunashindwa kuingia Lubumbashi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kutoka Dar es Salaam upite Tunduma ili uweze kuingia Lubumbashi ni rahisi sana kuliko kutoka Dar es Salaam, upite Tabora, uende ukaingie ufike kwenye zile bandari sijui Kasanga, Kabwe, Kalema ambayo imejengwa sasa hivi zaidi ya bilioni 49. Tulitakiwa tukae na nchi ya Zambia tujadiliane tuweke mambo sawa kule yale Majimbo kwa mfano lile Jimbo la Hot Katanga ambalo ndio Lubumbashi, Rwalaba ambapo ni Kolowezi tutumie hiyo njia ya Tunduma kufika kwa sababu ni rahisi sana, na huku tuangalie hayo majimbo kwa ajili ya kuingia kwenye Majimbo mengine ambayo yapo mengi kule Congo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumechukulia kama jambo hili kwamba tunajaribu kui-escape Zambia hakuna namna tunaweza tukai-escape Zambia kwa sababu bado tutataka kuingia kwenye nchi nyingine hata kama isipokuwa Congo. Tukitaka kuingia Zimbabwe tutaingiaje, tukitaka kuingia Botswana tutaingiaje ni lazima tutapita Zambia. Kwa hiyo ushirikiano wetu na Zambia si jambo la kuepukika si jambo la kupuuza Wizara hii mmechukua jukumu gani kuhakikisha tunaendelea kuji-expand/kujipanua zaidi kuona namna gani ambapo tunafikia soko la Congo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeliona hili jambo kama ni la kupuuza wafanyabiashara, madereva watu mbalimbali wanateseka sana. Sasa hivi imekuwa yaani unapopitisha mahindi Zambia ni kama umepitisha madawa ya kulevya na jambo hili sio kwamba Serikali ya Zambia ndio imelizingatia sana kwamba inaizuia Tanzania, wakati mwingine ni vita ya kiuchumi ambayo inafanywa na nchi nyingine, mbona South Africa wameaanza kujenga reli ambayo inapita Angola, iingie Lubumbashi iende mpaka Kolowezi. Hii ni vita ya kiuchumi ambayo wapo wafanyabiashara wanaendelea kutuchonganisha sisi na Zambia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi hatuwezi kugombana na Zambia sisi na Zambia ni ndugu, sisi na Zambia ni washirika wazuri ni washirika wa kihistoria ambao undugu wetu hauwezi kuepukika. Kwa hiyo mimi nilikuwa naona kuna haja kubwa sana Wizara hii itafute namna nzuri ya kwenda kukaa na nchi ya Zambia ili kuondoa vikwazo ambavyo tunavipata, ili wafanyabiashara ambao wanataka kupitisha mizigo yao kuingia Congo kwa kupitia njia ya Lubumbashi wapite kiurahisi na yale maboresha ambayo yamefanyika kwenye bandari zetu ili kuingia Jimbo la Tanganyika na majimbo mengine ambayo yapo Congo tuitumie kama fursa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Sichalwe, nilikuongeza dakika tatu.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)