Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Juma Othman Hija

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tumbatu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua fursa hii kukushukuru wewe kwa kunipatia nafasi hii ya kutoa mchango wangu katika hotuba hii ya makadirio na mapato ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Pili nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu wake pamoja na watendaji wake wote kwa kutayarisha na hatimaye kuiwasilisha hotuba hii katika Bunge lako tukufu kwa ufasaha na umakini mkubwa. Wizara hii ni miongoni mwa Wizara muhimu sana katika nchi yetu inayoonesha sura ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuchangia hotuba hii napenda kuchangia katika maeneo yafuatayo; kwanza ni kuhusu mapato. Wizara hii ni Wizara kama Wizara nyingine, ina malengo na makusudio yake. Moja katika malengo yake ni kujiwekea target ya matumizi na mapato ya Wizara. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Wizara ilijiwekea lengo la kukusanya shilingi 2,550,879,000. Lakini hadi kusomwa kwa hotuba hii ni asilimia 33 tu ya lengo ndio iliyokusanywa. Hii ni rekodi isiyoridhisha kwa Wizara.

Mheshimiwa Naibu Spika, uchunguzi wangu unaonesha kuwa vyanzo vilivyotarajiwa kutumika haviko imara (not stable), hivyo basi kuna haja ya kuangalia vyanzo vingine zaidi ili kutimiza lengo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu katika suala hili la makusanyo ya mapato ni kama ifuatavyo; hivi sasa nchi yetu inasifika kwa zoezi zima la Royal Tour. Napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuanzisha Royal Tour. Nchi nyingi zinapenda kuja kuona vivutio vyetu. Lakini watu wengi katika baadhi ya nchi hawavijui vilipo na hadhi yake. Ofisi zetu za ubalozi za nje zingetengeneza ramani ya nchi yetu huko kwenye ofisi za mabalozi zinazoonesha vivutio vyetu pamoja na hadhi ya vituo hivyo zikawaonesha watu wa nchi hizo kwa gharama ndogo pamoja na vipeperushi vinavyoonesha vivutio vyetu. Lengo ni kuuza ili kuongeza mapato, lakini pia kuwashawishi kuja nchini kuangalia vivutio vyetu. Hii itaongeza mapato kwa Wizara na kwa nchi kwa jumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa elimu kwa umma; hotuba ya Mheshimiwa Waziri imetaja namna ya kuelimisha umma juu ya yanayofanyika nchini mwetu. Hii ni habari nzuri sana kwa umma, lakini kasoro ya zoezi hili ni vyombo vinavyotumika sio sahihi kwa kuwafikia wananchi wa maeneo ya vijijini. Hotuba imetaja vyombo vinavyotumika ni magazine, television, radio na vipeperushi. Vyombo hivi si rahisi sana kuwafikia wananchi wa vijijini ambao ni sehenu kubwa ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu katika jambo hili kwa Wizara na Serikali kuweka kikosi kazi kwa kutumia usafiri wa magari kwenda vijijini kuwaelimisha wanavijiji wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Chuo cha Diplomasia; naipongeza Serikali yetu kwa kuweka chuo hiki, kimekuwa ni miongoni mwa vyuo muhimu sana katika nchi yetu. Serikali inapaswa kuchukua juhudi za makusudi kuboresha chuo hiki kwa kukiwekea mazingira mazuri ya kimataifa. Bado kuna hali isiyoridhisha kwenye miundombinu za chuo hiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mitaala ya chuo hiki pia ni vyema ikajielekeza kuwafundisha vijana wetu pamoja na mambo mengine namna ya kuweza kujitegemea wenyewe baada ya kumaliza mafunzo yao. Bado mpaka leo mitaala ya chuo hiki inawatengeneza wahitimu wetu kutegemea ajira za Serikali. Hivyo kuna haja ya kuwatengeneza watu wetu katika hali ya kujitegemea.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya ajira kwa upande wa Serikali nafasi haziwezi kukidhi kuajiri vijana wetu wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.