Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Dr. Eliezer Mbuki Feleshi

Sex

Male

Party

Ex-Officio

Constituent

None

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nichukue fursa hii kukushukuru kwa nafasi ambayo umenipatia, nitumie fursa hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri lakini na Kamati yenye dhamana na Mambo ya Ulinzi na Nje na mawasilisho ambayo umewasilisha kwenye Bunge lako tukufu, ninaunga mkono mawasilisho ya Bajeti ya Wizara, lakini nina wiwa walau kuchangia kwa machache kama yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza kwa uelewa wangu Serikali yoyote makini hufanyia kazi mawazo na ushauri inaoupokea kutoka kwa wananchi wake na kupitia kwa wawakilishi wao, lakini pili Serikali yoyote makini huheshimu sana mgawanyo wa madaraka uliowekwa na Katiba yetu. Sasa ningependa kuheshimu sana mawazo ya wachangiaji wengi ambao wameyawasilisha, lakini pia hata mawazo ya wasomi wenzangu wanasheria na nitagusia hili la ushiriki wa Tanzania katika Mahakama ya Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kumbukumbu zetu ziwe sahihi kwamba Tanzania ni nchi mojawapo muasisi wa Umoja wa Afrika lakini ni mwanachama mwaminifu na hai, lakini pia nchi yetu bado ni mwanachama wa Mahakama ya Afrika na hata sasa Rais wa Mahakama hiyo ni Mtanzania. (Makofi)

Sasa inapokuja namna ya kupeleka migogoro kwenye mahakama hiyo utaratibu umewekwa na protocol zinazoiongoza Mahakama hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, protocol ya tano imeorodhesha namna ya kufika kwenye mahakama ile na kwenye Ibara ya 3 inatoa fursa kwa nchi mwanachama aliyeridhia anaweza akatoa tamko kwa asasi za kiraia yaani NGOs na watu binafsi pia kufikisha mashauri yao kwenye mahakama hiyo. Wote tunafahamu Tanzania kwa sasa iliondoa tamko lake kwa NGOs pamoja na watu binafsi kupeleka mashauri yao au migogoro kwenye mahakama hiyo, lakini hiyo haimaanishi kwamba migogoro mingine baki inayohusu Tanzania na watanzania kwa maana ya zile haki zilizotolewa na kipengele cha A – E kufikishwa kwenye mahakama hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, msingi mkubwa ni lazima tutambue kwamba kwa mujibu wa Katiba yetu Ibara ya 107A(2) (a) mpaka (e) imetaja ile misingi ambayo migogoro yetu inavyotatuliwa. La kwanza; kwa sababu nchi yetu kama nilivyosema inaoongozwa na Katiba, migogoro imepangwa migogoro ya aina ipi ipelekwe wapi na Katiba yetu pamoja na sheria zingine zote inasema kwamba kabla ya kupata nafuu nyingine au kutafuta nafuu nyingine mamlaka zingine za nje ni vizuri kupata nafuu za kisheria kwenye mamlaka ya utatuzi wa migogoro tuliyonayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa misingi hiyo kwa kuwa tumesema kwenye Katiba yetu Ibara hiyo ya 107 kwamba mahakama ndiyo chombo pekee, lakini kwenye Ibara ya 13(6) namna ambavyo mtu ana haki ya kupeleka shauri lake kwenye ngazi za mahakama na vyombo vingine vilivyopewa dhamana hiyo. Kwa hiyo, ni msingi wa sheria zetu kwamba wananchi na mtu yeyote anayetaka kutetea haki yake apeleke shauri kulingana na jinsi ambavyo zile sheria zilizopo zimeainisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni kwa mantiki hiyo kwa sasa tutaona kwamba yapo mpaka mashauri ya Kikatiba ambayo yanapalekwa kwenye Mahakama Kuu na yanashughulikiwa. Lakini kwa mujibu kwa mfano kwa Sheria ya Madai na Sheria ya Uendeshaji wa Mashauri ya Jinai zimeanisha mashauri yapi yapelekwe wapi. Kwa hiyo, kitendo cha Serikali kuondoa lile tamko haimaanishi kwamba Serikali haina nia ya kurejesha haki ambayo kwa sasa hawapeleki, vilevile haimaanishi kwamba hao watu wanazuiwa kuleta mashauri yao kwenye mahakama hizi zingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ambalo tunawaasa wote ambao wanatafuta haki zao mahakamani; moja, ni kuzingatia mipaka ambayo tunayo na wote tunajua jinsi ambavyo hata hili Bunge lako tukufu lingependa sana migogoro ya Watanzania ishughulikiwe na mahakama kwanza ambazo zimewekwa kwa mujibu wa Katiba yetu na kwa sheria zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ile migogoro ambayo inafikia ile hadhi ya kwenda mamlaka za nchi, mamlaka zingine kama Mahakama ya East Africa, Mahakama ya Afrika, ICC basi zitafuata kwa mujibu wa zile nyenzo zilizopo za Kikatiba zinaoongoza namna ya kufikisha mashauri kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri kipindi hiki ninaweza nikasema kwamba hakuna yoyote kati ya NGOs pamoja na watu/raia waliokwenda Mahakama ya Afrika ambao walijaribu kuleta mashauri kwenye mahakama za nchi hii na wakanyimwa fursa hiyo, na endapo ikitokea hivyo basi hilo ni jambo ambalo vilevile linaweza likatapata suluhisho ndani ya mamlaka ya sheria zetu tulizonazo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika,tunazo sheria kama nilivyosema kwa mfano, tuna Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu lakini tuna Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai kifungu cha 7 kinaeleza kila shauri lianzie kwenye ngazi ya chini. Ukienda kifungu cha 264 Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai imepanga mashauri yapi ya kwenda Mahakama ya Wilaya, ya Mkoa. Sheria ya Mahakama imeeleza mashauri ya kwenda Mahakama za Mwanzo, ukija kwenye mabaraza yetu yote yaliyotungwa vilevile yaliyoanzishwa kisheria yanaainisha migogoro hiyo iende wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa mantiki hii hata protocol ya tisa ya Mahakama hii ya Afrika kwa mfano inatambua kwamba shauri hata kama lingekuwa kule linaweza likaenda kwenye mashauri yaani kwenye amicable settlement na unaporudi kwenye Katiba yetu Ibara ya 107A(2) (d) utakuta inasisitiza namna ya kukuza usuluhishi. Kwa hiyo, haiji akilini kwa nini ukaanze kutafuta usuluhishi kwenye mahakama ya juu au ya nje ukiacha mamlaka iliyo ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, itoshe niseme tu kwamba ninashukuru, lakini tutaendelea kuheshimu nafikiri mawazo ya wananchi kupitia kwa wawakilishi wao na kuendelea kufanya kazi nao na kuona namna ambavyo kila mmoja ataendelea kupata haki zake kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)