Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Amber. Mbarouk Nassor Mbarouk

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mwingi wa Rehma kwa kuturuzuku uhai na afya njema na kutuwezesha kujadili hotuba hii siku ya leo. Aidha, nichukue fursa hii kwa kipekee kumshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini kuhudumu katika nafasi ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia sina budi kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Phillip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushauri na maelekezo yao katika kutekeleza majukumu yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumshukuru Mheshimiwa Spika na wewe binafsi kwa namna mnavyoliongoza Bunge letu kwa hekima, busara na umahiri mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ninaomba kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa maoni na ushauri wao walioutoa kupitia taarifa iliyowasilishwa asubuhi hii. Hii ni Kamati makini sana, Wajumbe wake wanauelewa mkubwa wa masuala ya kidiplomasia na hivyo wamekuwa wakitoa mchango mkubwa ambao umeendelea kusaidia kuboresha utendaji kazi wa Wizara na diplomasia ya nchi yetu kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda pia kumshukuru Mheshimiwa Balozi Liberata Mulamula, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa uongozi wake mahiri ndani ya Wizara na ushirikiano mkubwa anaonipatia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ninamshukuru Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara na taasisi zote zilizopo chini yake kwa ushirikiano mkubwa ninaoupata kutoka kwao bila kuwasahau Mabalozi wote ambao wapo nchi za nje wakituwakilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ninapenda kuishukuru familia yangu kwa upendo na uvumilivu wao na kuendelea kuniunga mkono wakati nikitekeleza majukumu yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri nijielekeze katika kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge, lakini kwanza nitoe shukrani kwa Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia na kutoa maoni yao katika hoja ambayo imeletwa na Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana pia kwa pongezi nyingi ambazo Waheshimiwa Wabunge mbalimbali wamezitoa kwa Wizara yetu na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri tunawaahidi Waheshimiwa Wabunge wote kwamba pongezi hizi kwetu ni deni ambalo tutalilipa kwa kutekeleza majukumu yetu kwa bidii na ufanisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jumla ya Waheshimiwa Wabunge 20 wamechangia hoja hii na michango ya Waheshimiwa Wabunge wote tumeipokea na tunaahidi kuijumuisha katika utekelezaji wa mipango ya Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nianze kuhusu suala la viwanja, ujenzi na ukarabati wa majengo ya Ofisi za Balozi zetu. Suala hili limeongelewa takribani na nusu ya Wabunge ambao wamechangia leo hapa. Wizara tayari imekamilisha taratibu za manunuzi za kuwapata wakandarasi watakaotekeleza miradi ya ujenzi na ukarabati kwenye Balozi zetu nje ya nchi. Miradi hiyo ni ujenzi wa jengo la kitega uchumi katika Ubalozi wa Tanzania Nairobi ambapo mkandarasi aliyepatikana ni SRJE East Africa Limited, ujenzi wa jengo la ubalozi na kitega uchumi katika ubalozi wetu wa Kinshansa mkandarasi ni China Railways Construction Engineering Group Limited na ujenzi wa makazi ya jengo la ubalozi na makazi ya balozi katika ubalozi wetu Muscat mkandarasi aliyepatikana ni Arab Contractors na pia ujenzi wa jengo la ubalozi la kitega uchumi katika ubalozi wa Tanzania Comoro mkandarasi aliyepatikana ni Suma JKT Construction Company Limited, mradi wa ukarabati wa jengo la zamani la ubalozi R Street katika ubalozi wa Tanzania Washington mkandarasi ni Kampuni ya M&R Construction Group. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mikataba ya miradi hii tayari imeridhiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na hivi sasa ni Wizara ipo katika hatua za kukabidhi maeneo ya miradi (site possession) kwa wakandarasi ili ujenzi uanze mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika ubalozi wetu wa Msumbiji ambalo kuna jengo lenye ghorofa tisa tayari limekarabatiwa na lipo katika hatua za mwisho kukamilika. Aidha, kuhusu utekelezaji wa kiwanja cha ubalozi mpango wa kukiendeleza umeanza kufanyika kwa kukamilisha michoro na makabrasha ya jengo linalopendekezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ubalozi wetu wa Zambia kesho Wizara yetu ina kikao na Benki Kuu, Shirika la Nyumba la Taifa na Wizara ya Fedha pamoja na Wakala wa Majengo Tanzania kwa ajili ya kujadili namna ya kuviendeleza viwanja hivyo kwenye mwaka huu wa fedha. Hata hivyo, majengo sita yaliyopo Lusaka tayari yamekarabatiwa na yapo katika hadhi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ilielezwa hapa kwamba katika Ubalozi wetu wa Ufaransa tuna jengo bovu. Kwa kweli Ubalozi wetu wa Ufaransa hatuna jengo bovu, Wizara ina majengo mapya ambayo yamenunuliwa mwaka 2015 kinachofanyika ni ukarabati wa mara kwa mara hasa kutokana na vipindi vya joto na baridi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ilizungumziwa kuhusu ukarabati wa jengo la Ofisi ya Wizara iliyopo Zanzibar naomba kulitaarifu Bunge lako kwamba ukarabati wa Jengo la Ofisi ya Mambo ya Nje Zanzibar tayari umekamilika na jengo hilo sasa lina muonekano wenye hadhi ya Ofisi ya Mambo ya Nje. Aidha, kuna utaratibu pia saa hizi unaoendelea wa kuanza kujenga jengo jipya la Ofisi ya Mambo ya Nje ambalo tunategemea litakuwa sehemu ya Tunguu mara tutakapokabidhiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi naomba kukufahamisha kwamba hivi sasa Wizara yetu inaendelea na utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kujadiliana na taasisi za fedha hapa nchini kwa lengo la kuendeleza viwanja kwa kujenga majengo ya ofisi, vitega uchumi pamoja na makazi ya watumishi wa ubalozini. Hadi sasa kwa kutekeleza maagizo hayo tayari tumeshafanya vikao viwili na Benki ya CRDB kwa nia ya kuwa na utaratibu maalum wa kutekeleza maelekezo hayo. Tunafurahi kwamba hata leo hapa wawakilishi wa CRDB walikuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niongelee kidogo kuhusu suala jingine ambalo limechangiwa hapa na Waheshimiwa Wabunge wengi hili ni suala la wafanyabiashara wa Watanzania kuzuiwa kwenda China kwa kipindi hiki.

Waheshimiwa Wabunge ni vizuri tukaelewa kwamba ndugu zetu Wachina ugonjwa huu wa UVIKO ulianzia kwao na ulileta madhara makubwa ikiwemo zaidi ya watu 4,000 kupoteza maisha yao. Hali hiyo iliwafanya waweke masharti magumu ili kudhibiti maambukizo ikiwemo kuzuia raia wa kigeni kuingia China na kuwataka raia wao wanaorudi kwao kukaa quarantine siku 21 hotelini kwa gharama zao na kuyataka mashirika ya ndege ya kimataifa kupunguza safari za ndege hadi kufikia safari moja kwa wiki na katika safari hizo ndege isizidishe ujazo wa abiria kwa asilimia 60 ili kuwepo na social distance ndani ya ndege.

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, masharti hayo si tu kwamba yamewaathiri wafanyabiashara wetu bali pia yanawaathiri na raia wao na raia wa mataifa mengine yote ulimwenguni tangu mwezi Machi hadi leo hii tunavyozungumzia jiji la biashara la uchumi la Shanghai lipo kwenye lockdown baadhi ya wilaya za Jiji la Beijing nazo pia zipo katika lockdown na imeelezwa na ubalozi wetu kwamba kwa zaidi ya siku 60 sasa katika Jimbo la Shanghai wananchi wameambiwa wasitoke ndani ya nyumba zao na maduka yote yamefungwa, usafiri wa ndani umesimama, shughuli za mabenki pia zimesimama, shughuli za bandari, soko la hisa na viwanda vingi navyo vimesimamisha uzalishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo inatuonesha dhahiri ni jinsi gani ndugu zetu hawa wanavyochukulia ugonjwa wa UVIKO-19 tofauti na nchi nyingine duniani. Hatua zao si tu zinaumiza wafanyabiashara wetu, bali pia zinawaumiza wananchi wao. Hivyo tuvute subira na tuwe na matumaini kwamba mambo yatafunguka na wenzetu wakiwa tayari watatufungulia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tukisubiria hilo, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuwawezesha wafanyabiashara wetu kutimiza malengo yao ikiwa ni pamoja na kufungua dawati la viwanda na biashara kwa ajili ya kutoa huduma kwa wafanyabiashara wanaotaka kuagiza bidhaa China. Aidha, Serikali imefungua Ofisi ya Ubalozi mdogo Guangzhou ambayo itaendelea kufanya kazi hiyo kwa ufanisi zaidi. Aidha, Serikali imeanzisha safari za ndege za Air Tanzania na kusafirisha mizigo ya wafanyabiashara wetu ili kurahisisha upatikanaji wa mahitaji yao kwa haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kuna habari njema, na habari ambayo tumeipokea wiki hii ni kwamba kuanzia Juni mwaka huu shirika letu la ndege limeruhusiwa kuanza tena safari za kubeba abiria kwenda China. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kidogo kuna suala hapa pia lilizungumziwa kuhusu kufungua ubalozi nchini Pakistan na Iran. Kwanza nataka nikubaliane na Waheshimiwa Wabunge kwamba Pakistan na Iran tuna mahusiano nao mazuri sana na tumekuwa tukishirikiana katika mambo mbalimbali, lakini kuhusu mpango wa Serikali kufungua ubalozi wake nchini Pakistan na Iran, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki tayari imeanza kufanya utafiti wa kuona namna ya kufungua ubalozi katika nchi hizo kwa kuangalia faida za kiuchumi na maslahi mapana ambayo nchi yetu inaweza kunufaika nazo ikiwa ni pamoja na kuainisha gharama za ufunguzi wa ubalozi na uendeshaji wake, mara zoezi hilo litakapokamilika, basi Wizara itawasilisha mapendekezo na ushauri kwa mamlaka kwa ajili ya maelekezo zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa hoja hapa kuhusiana na fursa za ajira katika nchi mbalimbali huko nje ikiwemo Qatar. Ni kweli kwamba Tanzania na Qatar zilisaini MOU kwa ajili ya vijana wetu wapate fursa za kwenda kufanya kazi nchini Qatar. Hata hivyo, mara tu baada ya kusaini huko kukatokea ugonjwa wa Covid ambao ulizuia kidogo kuendelea na process hiyo. Lakini hivi sasa tayari mazungumzo yameshaanza tena na hivi karibuni tutapata habari njema. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri maliza. Mheshimiwa Waziri, maliza, sekunde 10.

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)