Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee naomba nichukue fursa hii kukushukuru sana kwanza kwa kunipatia nafasi asubuhi ya leo kuwasilisha mbele ya Bunge lako tukufu hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kukushukuru kwa dhati kwa kusimamia kwa umakini mjadala wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Umeonesha unaifahamu sana Wizara hii kutokana na kwamba ulikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishukuru tena kwa dhati Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama chini ya uongozi mahiri wa Mwenyekiti wa Kamati, Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Namtumbo na Mheshimiwa Vincent Mbogo, Mbunge wa Nkasi Kusini na Wajumbe wa Kamati kwa ushauri na maoni yao. (Makofi)
Niwahakikishie Wajumbe wa Kamati kuwa Wizara imepokea taarifa ya Kamati, tumepokea ushauri, tumepokea na maoni na tutayazingatia wakati wa kutekeleza majukumu ya Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Balozi Nassor Mbarouk, Mbunge na Naibu Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya na kwa kunisaidia kutekeleza majukumu ya Wizara, kwa hakika ni jembe. Ninamshukuru kwa majibu yake na ufafanuzi alioutoa kwenye hoja zilizoibuliwa kwenye mjadala huu. (Makofi)
Aidha, nawashukuru tena watumishi wa Wizara na taasisi zilizo chini ya Wizara chini ya uongozi wa Katibu Mkuu, Balozi Joseph Sokoine na Naibu Katibu Mkuu, Balozi Fatma Rajabu kwa kusimamia kikamilifu maandalizi ya bajeti ya Wizara. Nimefarijika sana kwa pongezi ambazo mmezitoa kuhusu uongozi wa Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho lakini siyo kwa umuhimu naomba kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge waliochangia kwa ujumla wenu kwa kuzungumza na wale waliochangia kwa maandishi. Nadhani haijawahi kutokea, leo tumepata michango kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge 21, kwa kawaida huwa hatufiki hata kumi. Kwa hiyo, naomba niwashukuru sana sana sana Waheshimiwa Wabunge na niwahakikishie kabisa na kwa moyo mkunjufu kwamba michango ambayo mmeitoa tumeipokea na tutaifanyia kazi, maoni na mapendekezo yaliyotolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kutokana na ufinyu wa muda, Wizara yangu haitaweza kuzijibu hoja zote kwa hapa, lakini tutazitolea maandishi na tutaweza kuwasilisha kwenu. Nipende pia kuwahakikishia Wabunge kwamba sisi pamoja na kwamba ni Wabunge lakini ni watendaji, ni watendaji ambao tunazingatia yote ambayo tunazingatia Ilani ya Chama cha Mapinduzi, tunazingatia mpango wa maendeleo, tunazingatia sera yetu ya mambo ya nje, tunazingatia maagizo yanayotolewa na viongozi wa kitaifa lakini tunazingatia maelekezo na maoni na mwongozo kutoka Bunge hili tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo ya utangulizi, naomba nitoe ufafanuzi kwenye masuala machache yaliyoibuliwa kwenye mjadala wa hotuba ya bajeti yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Naibu Waziri kwamba amepitia hoja ambazo zilikuwa zimechangiwa na Wabunge wengi lakini naomba nimshukuru kwa aina ya pekee Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu kwa kutolea maelezo kuhusu jukumu la Mahakama ya Haki za Binadamu na Watu na jinsi gani ushiriki wa NGOs na watu binafsi wanaweza kupeleka kesi zao huko, umelitolea maelezo mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumuhakikishia Mheshimiwa Mbunge ambaye ameliongelea hili kwamba tutaendelea na nitaomba kwamba tuendelee kuweza kuwasiliana maana Serikali imejipanga tunaendelea kuliangalia kwa mapana yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na pengine Mheshimiwa Salome nikufahamishe kwamba tumepata heshima kubwa ya kuwa na Jaji ambaye ni Rais wa Mahakama hiyo, Mheshimiwa Iman Aboud ambaye tuko naye. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge napenda baada ya kikao hiki unaweza pia na wewe ukatumia fursa hii ukaweza kuongea na Rais wa Mahakama hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingi zilitolewa lakini naomba nijikite kwenye hoja moja ambayo ilikuwa specific kuhusu suala la barabara ya Singomakua kwa upande wa Tanzania kama alivyoeleza Mheshimiwa Yahya Ally Mhata kwa upande unaohusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tayari imeshajengwa na Serikali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, napenda kulifahamisha Bunge lako tukufu kwamba Serikali ya Msumbiji tayari imetenga fedha za kujenga barabara zake ili kuunganisha na barabara zetu kwa lengo la kurahisisha mawasiliano na biashara kama alivyosisitiza Mheshimiwa Mhata. Leo hii nimeletewa taarifa kutoka Serikali ya Msumbiji kwamba barabara hizo ambazo zinafanyiwa matengenezo ni barabara ya Negomano mpaka Muenda ambayo ni kilometa 200, barabara ya Muenda mpaka Mount Pwezi ambayo ni kilometa 150 nayo inafanyiwa kazi na barabara ya kutoka Mount Pwezi mpaka Singomankua ambayo ni kilometa 90 tayari zimetengewa pesa kwa taarifa niliyoipata kutoka Serikali ya Msumbiji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge ambao wameliongelea vizuri sana au wameliweka vizuri sana diplomasia yetu ya uchumi ambayo ndiyo sera yetu ya mambo ya nje imejikita katika utekekezaji wa diplomasia ya uchumi. Tuliulizwa kuhusu mchango wa Wizara na balozi zetu nje na taasisi hizo chini ya Wizara katika kutekeleza diplomasia ya uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kulijulisha Bunge lako tukufu na kuwahakikishia kwamba tumejipanga vizuri katika kuteleleza hii diplomasia ya uchumi na mifano ipo mingi, lakini kwa uchache wa muda naomba tu kuainisha michache.
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa Mabalozi wetu wote wameelekezwa kwamba wawe na mpango mkakati unaoonesha jinsi gani wanatekeleza diplomasia yetu ya uchumi ikionesha malengo, ikionesha jinsi gani wakiainisha fursa na kujiwekea kama ninavyosema kipimo kwamba wanafanikisha vipi na sasa hivi tumeanza kupata hiyo mipango na kama Wizara inaifatilia kwa karibu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niseme katika mwaka wa fedha 2021/2022 Mheshimiwa Rais alianzisha Idara Maalum ya Diplomasia ya Uchumi kwenye Wizara yetu ambayo pamoja na mambo mengine inajukumu la kuratibu utekelezaji wa diplomasia ya uchumi. Kwa hiyo, idara hii inaratibu na kufanya ufuatiliaji wa karibu wa fursa za biashara, uwekezaji, utalii na nyinginezo zilizopo ndani na nje ya nchi kwa kushirikia na balozi zetu, taasisi za Serikali na sekta binafsi kwa lengo la kuhakikisha Taifa linanufaika na fursa hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na nilifarijika kumsikia Mheshimiwa Mbunge mmoja akisema kwamba ili kufanikisha diplomasia ya uchumi kwamba Waheshimiwa Wabunge na ninyi muwe mabalozi wetu, tushirikiane kwa pamoja tuweze kufanikisha hii diplomasia yetu ya uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee pia kwamba balozi zetu zinajitahidi sana kutangaza fursa za biashara na fursa za masoko. Na kama mlivyotaja Balozi wetu, Mheshimiwa Kombo alioko Italy hivi majuzi tu ameweza kuwaleta wakulima wa kawaida tu kwenye maonesho ya kilimo na niliwaona wengi wao walikuwa ni kinamama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika mazao yale hasa matunda na mboga zili-attract watu wengi sana. Kwa hiyo, hiyo ninayosema ni jitihada zinazofanywa na balozi zetu kuhakikisha kwamba mazao yetu, bidhaa zetu zinajulikana huko nje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme pia katika hotuba yangu nilieleza namna ambavyo nyama na bidhaa za nyama kutoka Tanzania vimepata soko katika nchi za Mashariki ya Kati na hivi karibuni Saudi Arabia imefungua soko la nyama yetu na watakuja kuwekeza kuhakikisha kwamba wanapata nyama ile ambayo inasoko katika nchi ya Saudi Arabia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, soko hilo limepatikana kutokana na jitihada za kutumia diplomasia, kushawishi mamlaka za Serikali na sekta binafsi katika nchi hizo kukubali kununua bidhaa zinazozalishwa nchini. Niseme mwezi uliopita nilienda ziara Saudi Arabia nikifuatana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi kuhakikisha kwamba tunafanikisha hili. Serikali ni moja, tunakwenda pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ninapenda kutambua mchango wa kituo chetu cha AICC ambacho kimekuwa mwenyeji wa kongamano la habari, lakini pia kitakuwa mwenyeji wa Shirikisho la Mpira (CAF). Kwa hiyo, nadhani hii itakuwa karibu sana tutashiriki huko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, najua limeongelewa hili kwa mapana yake suala la diaspora, suala la uraia pacha na hadhi maalum. Kuhusu suala la uraia pacha nimemsikia sana sana na nashukuru kwa mchango wako Mheshimiwa Gwajima, Mchungaji wetu nakushukuru kwa kuweza kufanya tuseme tafiti (research). Umetueleza kwamba karibu nchi 75 duniani zinaruhusu uraia pacha, lakini pia Mheshimiwa Mbunge na Mchungaji wangu nikueleze kwamba kuna nchi zaidi ya 100 ambazo hazikubali uraia pacha. Kwa hiyo, siyo Tanzania tu na sababu ni nyingi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuhusu suala hili napenda kulialifu Bunge lako tukufu kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Uraia ya mwaka 1995 suala hilo linahitaji mjadala mpana wa kitaifa. Tayari Serikali inaendelea na mashauriano ya ndani na wadau mbalimbali wakiwemo wana-diaspora wenyewe ili kuweza kufikia uamuzi utakaonufaisha diaspora kwa kuwapa hadhi maalum hasa ikizingatiwa kuwa siyo nchi zote duniani zinaruhusu uraia pacha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, labda nimfahamishe pia Mheshimiwa Mbunge kwamba katika nchi za Gulf tukiamua kuwapa Watanzania uraia pacha wanaondolewa uraia wa nchi za Gulf. Sasa ndiyo maana nasema tulifanyie mjadala vizuri tuweze kwamba wengine wasiumie, wengine wakafaidika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimesikia utatoa mshahara, nahitaji mshahara tuendelee na majadiliano na mashauri ili kusudi tuweze kufikia muafaka kuhusu suala hili muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia Waheshimiwa Wabunge wameongelea kuhusu suala la hadhi maalum ambayo inalenga kuwatambua diaspora na kuondoa baadhi ya changamoto mlizozitaja za kisheria na kisera zinazowakwamisha katika kushiriki kikamilifu katika kuchangia maendeleo ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, naomba niwaeleze kwamba tumekuwa kwenye mchakato huu baada ya kuonekana suala la uraia pacha kwa kweli kwa sasa hivi tusingepata kutokana na hayo ambayo nimeyaeleza. Lakini tukafanya utafiti kwamba nchi ambazo hazina uraia pacha zina mpango gani? Kwa hiyo ndiyo tukakuta kwamba hii hadhi maalum pengine ndiyo compromise kwamba Mheshimiwa Mchungaji wangu umesema umeishi Marekani, hadhi maalum ni kama green card ya Marekani ambayo ukipata green card unapata haki zote. Unaingia bila viza, unafanya biashara yako, kwa tukasema kwa nini na sisi tusijikite hapo. (Makofi)
Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo Wizara inapanga kuwa na Semina kuhusu hili suala lakini suala la mchango wa diaspora kwa mapana yake tutaiangalia uraia pacha lakini hadhi maalum kwa kweli ukiangalia India mmetaja hapa Pakistani, Iran wote wana hadhi maalum ikiwemo hata Ethiopia nayo ina hadhi maalum kwa wale ambao na nini. (Makofi)
Kwa hiyo mimi nazani labda tu kama mlivyotoa mapendekezo kwamba kutoa elimu, tutatoa semina. Napenda niwahakikishie kwamba na tutawashirikisha wana diaspora wenyewe siku hizi wanatuambia msitusemee tulete tuseme wenyewe, kwa hiyo, tutawaleta na tutakuwa na semina. Naomba nisisitize kwamba hili kwa kweli Wizara inalichukulia kwa umuhimu wake na lipo shirikishi na tutakuwa na hiyo semina ukituruhusu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho pengine Sera ya Mambo ya Nje; napenda kurudia kulihakikishia Bunge lako tukufu kwamba Wizara imekamilisha mchakato huu wa Sera ya Mambo ya Nje ambayo inazingatia mabadiliko ya hali ya sasa na tunatarajia katika mwaka ujao wa fedha hii sera itakuwa imepita ianze utekelezaji. Kama nilivyosema sera hii imejumuisha masuala mapya ambayo ni pamoja na uchumi wa kidigitali kama nilivyosema sasa hivi tunajikita kwenye digital diplomacy, lakini pia inazingatia masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi, lakini pia uchumi wa bluu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tumepitisha sera yetu ya mwaka 2001 kulikuwa hakuna dhana ya uchumi wa bluu. Kwa hiyo sasa sera yetu nayo itajikita katika uchumi wa bluu, lakini pia kukuza Kiswahili kama lugha ya kidiplomasia na biashara. Pengine kuhusu kukuza Kiswahili, Waheshimiwa Wabunge nasema kubwa zaidi na naomba mtusaidie Watanzania hawachangamkii fursa, nchi za jirani zinachangamkia. Kwa hiyo, sisi kama Wizara tunawabeba kama juzi nilivyosema nilikuwa na Malabo, Equatorial Guinea tumewabeba kuhakikisha kwamba katika kikao hicho tuna wakalimani, wasije wakapata sababu kwamba hawapo. Lakini tunasema kwa pamoja kwa kweli tuchangamkie fursa, majirani zetu wanaenda mbio na sisi tuende mbio. Balozi zetu zimeanzisha vituo, juzi nimefungua Kituo katika Ubalozi wetu wa Seoul, Jamhuri ya Korea na nimeweza kutoa vyeti kwa wanafunzi 300 wa Korea waliyojifunza Kiswahili. Lakini pia ndiyo nasema kuna mwalimu mmoja, tumekuwa tunatafuta, Balozi wetu anahangaika lakini bado kwa hiyo mimi ninasema tuchangamkie fursa na Afrika ya Kusini kwenye Balozi yetu nao wamefungua kituo cha kuweza kutoa mafundisho ya Kiswahili, kwa hiyo fursa zipo tuzichangamkie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwishoni nimalizie kwa kusema katika masuala ya utawala na maendeleo ya watumishi kuna swali lilitokea kuhusu kulipa mafao yao. Naomba nilihakikishie Bunge hili kwamba mafao yote sasa hivi ambayo yalikuwa yamechelewesha yanalipwa na mengine yanafanyiwa uchakataji kwa hiyo naangalia sasa katika mwaka ujao wa fedha tutakuwa tumemaliza mafao ambayo watumishi walikuwa hawajalipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako naomba nimalizie kwa kusema kuhusu kuridhia mikataba; kuhusiana na Serikali kuridhia mikataba mbalimbali iliyosaini, naomba kulitaarifu Bunge lako kuwa Wizara itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Wizara na Taasisi nyingine za Serikali ili kuhakikisha kwamba Serikali inaridhia mikataba yenye maslahi ya Taifa na kutokana na Mwongozo wa Kamati yetu tayari tulishakuwa na kikao maalum cha kupitia mikataba yote ambayo tulisaini, hatujaridhia au mikataba ambayo hatujasaini na sasa hivi kwa kukaa na wenzetu wa Wizara za Sheria na wengine kwa hiyo mikataba hii ninapenda kukuhakikishia Bunge lako kwamba inafanyiwa kazi kwa manufaa ya Taifa letu.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo napenda kuwashukuru tena kwa kunisikiliza, ahsanteni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tena kutoa hoja, ahsante sana. (Makofi)
(Hoja imetolewa Iamuliwe)
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.