Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwimba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SHANIF M. JAMAL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza kwenye hotuba hii ambayo ipo mbele yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri yenye matumaini kwa wananchi ambayo ameitoa hapa mbele yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitapenda kuchangia katika maeneo machache matatu. La kwanza, ningependa kuchangia sehemu ya umeme vijijini REA. REA ni changamoto kubwa tuliyonayo sisi wananchi wa Jimbo la Kwimba. Tuna vijiji takribani 32 tunasubiri kupata umeme. Ilani ya Chama cha Mapinduzi inatangaza kwamba umeme utafikishwa mwaka huu mwishoni lakini bado kuna changamoto, ukimfuatilia mkandarasi amemaliza vijiji vinne kupata umeme, lakini hivyo vijiji vinne ambavyo ameshavimaliza bado hajawasha umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli shughuli ya umeme vijijini inaenda taratibu sana, ningeomba sana Mheshimiwa Waziri aweke nguvu ya ziada, umeme vijijini ni siasa. Ni siasa kwetu sisi huko vijijini, hivyo, tunaomba tupate umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kusema kwenye bajeti ya mwaka huu mahitaji ya kupeleka umeme vijijini kwenye bajeti yake Mheshimiwa Waziri amesema mahitaji ni shilingi trilioni 1.24, lakini fedha alizozitenga ni bilioni 164, ni asilimia 15 tu. Nasema hizi fedha ni ndogo sana anatakiwa aongeze bidii kwa sababu maana yake tutapata umeme vijijini asilimia 15 tu kwa mwaka ujao. Ningeomba sana hizi fedha za kupeleka umeme vijijini zingeongezwa kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili pia kuna changamoto wakandarasi wanasema hata Mheshimiwa Waziri alitwambia kwamba kuna changamoto, vifaa vimepanda bei, wanaboresha mikataba na wakandarasi. Naomba tupate mwelekeo wa Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake wakati anatupa majibu, atuambie wakandarasi hawa anafunga nao mkataba lini, watarekebisha lini, ili hawa wakandarasi waweze kuendelea na kazi kwa speed kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kulizungumzia ni suala la subsidy, suala la shilingi bilioni 100 ambayo Serikali imetoa kwenye mafuta. Naomba ku-declare interest mimi ni mdau, nataka nipongeze Serikali kwa kazi nzuri sana ambayo imefanya ya kutoa msaada kupunguza makali ya mafuta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii subsidy ya bilioni 100 iliyotolewa kwenye mwezi Juni ina changamoto nyingi sana ambazo imekuja nazo, wafanyabiashara wa mafuta, kuna mafuta yamekaa kwenye maghala ambayo yalishalipiwa kodi sasa hivi yale mafuta yote yaliyokwishalipiwa kodi sasa inabidi uuze kwa pungufu ya sh.300 ambayo ni subsidy. Kuna hasara kwenye kwa makampuni ya mafuta takribani shilingi bilioni 50 inapatikana hasara kwa makampuni ya mafuta ambayo yamekutwa na stock ya aina hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ni kwamba subsidy nasaidia kupunguza makali lakini kuna utaratibu, sasa maana yake mafuta ni biashara ni shughuli ambayo ni nyeti sana haitaki kuingiliwa sana. Maana yake sasa mwezi wa Sita tumeingilia mwezi wa Saba hatujui kinachoondelea, kutakuwa na utofauti tena, maana yake kuna mafuta utakuwa unalipia mwezi wa Sita utavuka nayo mwezi wa Saba. Sasa mwelekeo wa mwezi wa Saba haijulikani tena itategemea kwamba Makampuni tena yatapata hasara au itatokea nini. Mimi ningeshauri wazo la Serikali kupunguza makali ni mazuri lakini iwe endelevu, maana yake ifanyike kwa miezi mitatu au miezi sita. Kila miezi itakuwa ina changamoto yake. Kwa hiyo mimi ningependa kusema kwamba hii subsidy ni kitu kizuri lakini wakifanye kiwe kama Sera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeshauri kwenye suala la subsidy kama inaendelea basi Mheshimiwa Waziri alivyosema kwenye hotuba yake kwamba ataka aanzishe stabilization fund, maana yake basi wangetangaza ingekuwa ni stabilization fund. Mfano, wangetoa fidia kwa miezi mitatu wakati mafuta yanapanda bei basi baadae wakati mafuta yakianza kushuka mwezi wa Agosti, Septemba, mafuta yakianza kushuka bei wanaanza kurudisha ile stabilization fund kurudisha hii fedha. Kwa hiyo, maana yake kuwe na sera na kuwe na utaratibu mzuri wa kuweka wazi kwamba hili suala litaendaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ningependa kulisema leo ni suala la Bulk Procurement Agency. Mimi niwapongeze, Bulk Procurement Agency wanafanya kazi nzuri sana, wanasimamia kuagiza mafuta kwa niaba ya Makampuni ya mafuta. Leo takribani miaka 11, Bulk Procurement Agency wanafanya kazi ya kuleta mafuta ndani ya nchi. Changamoto zipo lakini pia kazi nzuri wamefanya. Hapo nyuma nilisikia mara nyingi watu wakisema kwamba hii mafuta tungevunja Bulk Procurement tukaanza kufanya watu wafanye mafuta ya kuleta watu binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna nchi duniani ambayo inaweza ikaacha mafuta ikafanywa na wafanyabiashara peke yao, lazima Serikali iwe na mkono wake isimamie, changamoto ipo lakini tunafanya kazi vizuri. Pia lazima tufahamu kwamba Bulk Procurement tender zinazotangazwa ndani ya nchi yetu zinaleta mafuta kwa ajili ya nchi nyingine Sita ambazo zimetuzunguka, nchi ya Rwanda, Burundi, DRC, Zambia, Malawi, Uganda wanategemea mafuta yanayoletwa kwenye Bulk Procurement. Kwa hiyo, mimi ningeshauri Serikali wanapofanya maamuzi waangalie kwamba nchi hizi Sita pia zinategemea mafuta yanayoletwa ndani ya nchi yetu. Kwa hiyo tunavyoboresha tuangalie na nchi hizi Sita ambazo zinatuzunguka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ningependa kulisema pia Tanzania tumetoa subsidy nchi zinazotuzunguka zote Sita hizi hazijatoa subsidy. Itafika sehemu tutaenda tutakuta nchi za jirani mafuta ni bei nafuu kuliko mafuta ya Tanzania. Kwa hiyo, lazima tuangalie tuwe tunaenda pamoja na nchi za jirani kwa sababu mafuta yote yanayoingia ndani ya nchi yetu yanaenda pia kwenye nchi ya jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ningependa kulisema ni kwenye Bulk Procurement tunafanya tendering ya meli takribani Nane au Tisa kwa mwezi. Naipongeza Serikali wamewapa uwezo TPDC toka mwaka jana Desemba, mwaka jana Oktoba wameanza kushiriki, naomba TPDC waongeze speed ya kushiriki, wanashiriki kwenye tender moja moja tu za diesel kwenye petroli TPDC hawashiriki sijui kwa nini. Mimi ningeomba sana na ningeishauri Serikali TPDC pia inatakiwa ishiriki kwa undani zaidi maana yake inatakiwa TPDC inavyoshiriki unakuta na bei zinashuka kidogo. Kwa hiyo, TPDC tungeomba muwape nguvu ya ziada, TPDC ishiriki kwenye tender za kila mwezi. Kuna tender Nane unakuta TPDC ana tender moja tu ndiyo anashiriki au mbili zingine zote anaziachia. Mimi ningeomba sana Mheshimiwa Waziri TPDC washiriki kwenye tender zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mengi ya kusema nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja. Naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)