Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chumbuni
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nichukue nafasi hii kukupongeza wewe lakini ninamshukuru Mwenyezi Mungu kunijaalia nafasi leo kuwa ni miongoni mwa wachangiaji wa Bajeti yetu hii ya Nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipende kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu na Watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi ambayo wanaifanya na ambayo inaonekana. Pili, ningependa niwapongeze watu wa TANESCO kwa kushughulikia lile suala ambalo mara nyingi nikilisema zaidi ya miaka miwili mitatu la kuhusu bei ya umeme ambayo wanauzia Zanzibar. Kiukweli nataka niwapongeze nichukue nafasi hii, wamefanya kama ambavyo imekuwa tumetarajia na hatua ambazo zimefikia kiukweli imebaki kidogo lakini watu wa Zanzibar wanasema ahsante sana na wanaipongeza TANESCO kwa kuwasikiliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka niliseme ni kuhusu kukatikakatika umeme. Zanzibar kumekuwa umeme ukikatikakatika sana sijui kwa nini, kwa hivyo nafikiria TANESCO kwa sababu wao ndiyo source ya umeme Zanzibar kupatikana walichukue hili halafu waangalie waone kuna nini ambalo linasababisha, kama ni miundombinu basi tuone tunarekebisha vipi ili tatizo la kukatika kwa umeme lisiwepo lakini kwa upande wa mwanzo wa bei tunashukuru na wazanzibar wamenituma kabisa wamesema ukipata nafasi ya kuongea basi jaribu kuwaambia kwa hili tunawapongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mama. Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo anai-support Wizara hii na miradi ambayo iko ndani ya Wizara hii. Katika Wizara hii kuna mradi mkubwa wa Bwawa la Mwalim Nyerere, Bwawa la Mwalim Nyerere ambalo limekuwa mara nyingi ni gumzo kubwa ambalo linazungumziwa hapa, kwa stage ambayo imefikiwa sasa hivi, kwa mtu yoyote ambaye hajawahi kwenda chini ya miezi mitatu au minne akienda sasa hivi na akakuta asilimia ambayo imefikiwa basi hawezi kuamini. Mradi unakwenda vizuri, Mama amepeleka pesa ya kutosha, mradi mpaka sasa hivi umeshafikia zaidi ya asilimia 60. Mama ameshatoa zaidi 3.8 bilioni na mpaka sasa hivi hakuna Mkandarasi ambaye anadai wala deni la fedha lolote kuhusu hili Bwawa la Mwalim Nyerere. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi nawapongeza Wizara na TANESCO kwa kuanza kujenga transmission ya kutoka Rufiji kwenda Chalinze. Vilevile na kujenga substation ya Chalinze. Kwa sababu Bwawa hili pamoja na kuwa tunalihitaji na linaendelea kwa kasi hata lingekuwa limeisha leo bila transmission line maana yake pia tusingeweza kutumia umeme huu. TANESCO tumeaa nao na Wizara katika Kamati tukawashauri kwa nini vitu hivi visiende pamoja na sasa hivi wamevianza kwa hivyo tuna uhakika inapofika mwisho wa mradi wa bwawa basi na substation ambazo zitakuwa zinagawa umeme huu zitaweza kutumika na itakuwa yale malengo ambayo tunasema tuendelee katika kuhakikisha umeme mwingi unapatikana lakini unatumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwa na umeme ni jambo moja lakini je tutautumiaji na hatuwezi kuutumia bila kuwa na transmission kuutoa kule ambako uko kuuleta kwenye substation, kwenye substation ndipo ambako tutakuwa tunaugawa kwa ajili ya matumizi. Niwapongeze sana TANESCO na Wizara mpaka sasa hivi kwa stage hiyo ambayo mmeifikia. Labda mimi nitoe ushauri tu mmoja ambao ningependa niwashauri TANESCO mambo mengine yapo kwenye Kamati nimechangia kama Mjumbe na michango yangu mingine nimeandika kwa maandishi, ningewashauri TANESCO sasa hivi umefika wakati wa kutafuta vyanzo vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikia Mheshimiwa Waziri wakati anawasilisha bajeti yake, amesema Wizara imejipanga katika kuhakikisha inakuwa na vyanzo vingine tusitegemee zaidi maji ambapo ikitokea ukame basi inakuwa hali ya taharuki kama miezi mitano, sita ambayo ilipita tuliona wenyewe ambapo mabwawa yana upungufu wa maji basi ikabidi tuingie kwenye mgao wa umeme pasi na kuwa na sababu ya kuingia kwenye hiyo. Vyanzo vingi tunavyo hapa nchini kwetu lakini Wizara napenda ijielekeze tuhakikishe tuna vyanzo vingine nje ya maji vya kupata umeme ili inapotokeza ukame au mvua kidogo basi tuhakikishe tunayo reserve ambayo tunaweza tukaitumia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine na si kwa umuhimu sana lakini ni umuhimu ni kwa ajili ya miradi hii ya REA ambayo inakwenda kwenye Vijiji. Vijiji vingi REA imefika, lakini watu wengi ambao wako kwenye vitongoji sasa ambavyo Mheshimiwa Waziri amesema kuna mpango kabambe wa kupeleka kwenye vitongoji. Mimi ningependa tungehakikisha sasa kwenye vitongoji tunapeleka umeme kwa kiwango kikubwa kwa sababu watu wengi wanasema umeme upo lakini uko Mjini, walioko ndanindani kule wanashindwa kuupata, kwa hivyo REA ningependa niwapongeze. Jambo jingine na si kwa umuhimu sana, nichukue nafasi hii niipongeze Wizara nzima si Waziri tu, au Naibu, au Katibu ni Wizara nzima pamoja na ma-technician wao, ma-engineer ambao wanaweza kuisaidia sana hili Shirika letu la umeme TANESCO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache niliona na mimi nitoe mchango wangu huu japo mdogo, nawashukuru sana na naunga mkono hoja kwa asilimia 100. Ahsante sana.