Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa hii nami niweze kuchangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya. Kiupekee kabisa niipongeze Wizara ya Nishati wakiongozwa na Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa January Makamba na Naibu Waziri, Mheshimiwa Stephen Byabato na Watendaji wote wa Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Simiyu unapata umeme kutoka katika Mikoa ya jirani Mkoa wa Shinyanga, Mwanza na Mara wenye njia za umeme zenye msongo wa Kilovolt 33. Changamoto kubwa tulizonazo katika Mkoa wa Simiyu ni kiujumla njia hizi zimekuwa ni ndefu sana lakini kumekuwa na changamoto ya umeme kukatika mara kwa mara. Lakini ukiangalia Maswa Feeder ambayo ni njia ya umeme inasambaza umeme ukitoka kuanzia Kwimba, Mwanza na una-supply katika Wilaya za Bariadi tano. Sasa changamoto zikitokea katika Wilaya moja zinaathiri Wilaya zingine katika Mkoa huo. Na changamoto ya pili Mkoa huu hauna grid substation, hali hii inasababisha viwanda ambavyo vinaendeshwa katika Mkoa huu kunakuwepo na changamoto ya umeme, umeme haujitoshelezi na viwanda vingi ukiangalia tuna viwanda vikubwa saba vya pamba na vingine nane vimekufa kwa sababu ya kutokuwa na umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ya kutatua changamoto hii. Wizara ilipendekeza kuwepo na grid substation ambayo mradi ulishazinduliwa katika Kijiji cha Imalile Wilaya ya Bariadi na Mradi huu utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 75. Lakini nimeona katika bajeti fedha iliyotengwa ni Milioni 725 fedha hii ni ndogo sana na ukizingatia wananchi tayari wameshalipa fidia lakini mpaka hivi sasa bado mradi haujaanza na changamoto hii imekuwa ni ya muda mrefu sana. Tunamuomba Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha hoja yake atueleze ana mpango gani na Mkoa wa Simiyu ili tuweze kupata umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine tuliyonayo katika Mkoa wa Simiyu kuna baadhi ya maeneo ya migodi ambayo hayajapelekewa umeme hadi mpakahivi sasa kwenye Wilaya ya Busega na Wilaya Bariadi. Na maeneo hayo ni kama ifuatavyo, Dutwa, Halawa, Nyawa, malamata na Bulumbaka bado yote hayajapelekewa umeme, ukizingatia migodi hii inachangia mapato ya Serikali vizuri. Kwa mfano, katika Mgodi wa Gasuma wao wanatumia zaidi ya lita 2,000 ambayo hii inaongeza gharama za uzalishaji na inasababisha wao wasiweze kuzalisha kwa kiwango cha juu. Tunaiomba Serikali iweze kupeleka umeme katika maeneo haya ili hawa wachimbaji waweze kunufaika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwenye bajeti wametenga Bilioni 100 katika mradi wa kupeleka umeme katika maeneo ya wachimbaji. Nikuombe Mheshimiwa Waziri katika hiyo Bilioni 100 nasi Mkoa wa Simiyu uweze kutuona na maeneo haya ya wachimbaji yaweze kupata umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Simiyu tunavyo Vijiji 470 na Vijiji vilivyopata umeme ni Vijiji 269 na Vijiji 201 havijapata umeme. Nikuombe Mheshimiwa Waziri nimekusikia unasema utapeleka umeme kwenye Vitongoji kama huku kwenye Vijiji bado hatujaweza kufanikiwa kumaliza kupeleka umeme, nikuombe uweze kuja na mpango mzuri wa kuweza kuhakikisha kwamba Vijiji vyote vinapelekewa umeme kama tulivyoahidi katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ifikapo mwaka 2025 tutaweza kusambaza umeme katika Vijiji vyote na katika vitongoji vyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)