Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Aeshi Khalfan Hilaly

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumbawanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi; awali ya yote naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, lakini vilevile kuipongeza Wizara yote ya Ujenzi.
Mimi ndani ya Jimbo langu la Sumbawanga Mjini kwa kweli, wananchi kupitia mimi, nitoe shukrani zangu nyingi sana za dhati, tumepata barabara zote kwa kiwango cha lami, zimejengwa na zimekamilika ndani ya Jimbo la Sumbawanga Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama hapa kwa hoja moja tu ya uwanja wa ndege. Kwenye bajeti ya mwaka huu uwanja wa ndege ndani ya Jimbo la Sumbwanga Mjini unajengwa. Sasa wako baadhi ya Wabunge wametaka kupinga wakisema uwanja wa ndege ndani ya Jimbo la Sumbawanga Mjini usijengwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme ukweli, uwanja wa ndege wa Sumbawanga ukijengwa utarahisisha mambo mengi; na uwanja wa ndege unapojengwa eneo lolote lile ni maendeleo makubwa. Sasa nataka niseme, mimi nimuombe Mheshimiwa Waziri bajeti hii iende kama ambavyo imepangwa na wananchi wa Sumbawanga walikusikia na wamefurahi sana na mimi kama Mbunge nasema hivi, ninaunga mkono kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine nilitaka niwashauri Wabunge, kila Mbunge amechaguliwa jimboni kwake na wananchi wake. Mimi nimehangaika miaka mitano kuhakikisha tunapata bajeti ya kujenga uwanja wa ndege na hatimaye tumefanikiwa, ninaomba kila Mbunge akalilie jimbo lake. Na Waheshimiwa wengine waliokuwa wanasema tusijenge uwanja wa ndege, basi kwao wakajenge reli hiyo siyo kwangu, mimi kwangu sihitaji reli, nahitaji uwanja wa ndege. Barabara ya lami ninayo, nataka sasa uwanja wa ndege ujengwe ndani ya Jimbo la Sumbawanga Mjini. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kusema hivi kwa sababu Wabunge hawa wanaopinga uwanja wa ndege ndiyo wanaosafiri kutoka Wilayani kwao wanapita Wilaya ya Jimbo la Sumbawanga Mjini wanakwenda Mbeya kufuata uwanja wa ndege. Sasa tunataka tuwarahisishie, uwanja ukijengwa Sumbawanga hawatasafiri kwa muda mrefu. Kwa hiyo, nataka niseme tu kuwa Mheshimiwa Waziri nakuunga mkono na nitatetea hoja hii, ilimradi kuanzia mwaka huu uwanja huo utajengwa na wananchi wa Sumbawanga watapanda ndege kwa bei nafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kutoka Sumbawanga kwenda Dar es Salaam tunapanda kwa shilingi 900,000, lakini uwanja utakapokuwa umekamilika tutapanda kwa shilingi 200,000, mtakuwa mmetusaidia mno.
Kwa hiyo, nasema kwa haya machache kwa dakika tano ulizonipa, nilitaka kumuunga mkono Mheshimiwa Waziri kwamba, tunaomba sasa uwanja huu wa ndege ujengwe kama tulivyokuwa tumekusudia kwenye bajeti yako. Ahsante sana kwa kunipa nafasi.