Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Emmanuel Adamson Mwakasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nami nafasi ya kuchangia katika Wizara muhimu hii ya Nishati na mimi nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan hasa kwa hili la leo kwamba hata mafuta sasa yamepungua bei kwa kiasi fulani. Lakini Mheshimiwa January Makamba unafanya kazi nzuri hongera sana. (Makofi)

Mimi nadhani nianze na hili la leo kupungua bei ya mafuta, hili liende na kwenye Wizara zingine. Wakati mafuta yamepanda bei na vitu vingi vilipanda bei kwa kisingizio cha haya mafuta. Kwa mfano, Wizara nyingine litachukua hata hili kwamba kwa mfano kwenye kilimo sasa mazao nayo, yaonekane yanaanza kupungua bei kwa maana ya kwamba vitu tuvione vinaanza kupungua bei. Kama vitu mitaani vitazidi kuwa na hali ile ile wananchi hawawezi kuona unafuu wa kupungua bei ya mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia usalama wa mafuta wapo ndugu zetu Kampuni mbalimbali na mashirika ambayo yanashughulika na usalama wa mafuta. Vituo vingi vya mafuta vina mafuta mazuri, lakini baadhi ya vituo vinaharibu sana magari ya watu. Kuna vituo ambavyo ukishaweka mafuta sijui huwa wanachanganya au namna gani, lakini baada ya hapo unakuta umeweka mafuta gari imekuwa na matatizo, kwa hiyo, wananchi pia wanapata tatizo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye suala la REA; maeneo mengi yalishaahidiwa na Serikali kwamba yatapewa umeme wa REA katika mwaka huu mpaka mwaka kesho kwamba karibu vijiji vyote vitapata umeme, nchi hii ni kubwa na kuna majimbo mengine ni ya mjini kama mimi Tabora Mjini ni mjini, lakini kwa kutamka ni mjini, ila Tabora Mjini ina vijiji 41 na vijiji vile vingine vinakwenda mpaka masaa mawili kufikia hivyo vijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna baadhi ya watendaji wakishaona neno mjini wanasema wote hawa kuunganishiwa REA ni shilingi 27,000 kitu ambacho wanakuwa hawajawatendea haki wananchi. Mheshimiwa Makamba uzuri Tabora umeshafika, umefika Nisha kule na sehemu zingine, lakini kuna Mawaziri wawili akiwemo Mheshimiwa Mgalu kuna siku moja nilikuwa nataka nimpeleke kijiji kimoja Itema, alivyofika njiani wakati ule akiwa Naibu Waziri akasema huku kote pia ni Tabora Mjini, naomba tuishie hapa hapa, hatukuweza kufika kwa sababu ni mbali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna mwongozo mlitoa kwamba hata vijiji vile viweze kupatiwa umeme wa REA. Sasa nina taarifa kwamba kwa sababu neno mjini linasemwa wananchi wa vijijini kule wanataka kupewa umeme kwa gharama ambayo sio ya REA. Kwa hiyo, naomba hili Mheshimiwa Waziri January uliangalie sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna suala hili la uunganishwaji umeme, nimesikia hata kwenye taarifa ya Kamati ya Nishati, hawa wakandarasi ambao wanaunganisha umeme kwenye nyumba mbalimbali gharama zao ni kubwa sana. Nadhani ni vizuri Serikali ikaangalia namna ya kuwa-control hao wakandarasi, hakuna faida Serikali ipunguze namna ya kufanya installments za umeme, halafu hao wakandarasi wawe wanazidisha bei, yale makali ya fedha za uunganishwaji umeme yatabaki pale pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna hawa waratibu ambao watakuwa wanatoa taarifa hizi za uunganishwaji wa umeme hasa katika suala hili la REA. Naomba ndugu yangu January katika hili hao waratibu wenu ambao watakuwa wanatoa hizi taarifa muwafuatilie ili kuona kwamba taarifa zao je, zitakuwa sahihi? Maana yake mara nyingi hamuambiwi taarifa ambazo ni sahihi. Vijiji vingi kweli na vitongoji havijapata umeme na wananchi muda tuliowaahidi kwamba ukifika muda fulani watapata umeme, wanasikiliza tu muda ule ukifika hawakupata huo umeme Mheshimiwa January tutakuwa katika hali mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna suala hili la kubadilisha nyaya za umeme sehemu mbalimbali nchini, Tabora kuna shida sana ya kukatikakatika umeme kama walivyosema wenzangu hapo. Wananchi wanapata shida ya umeme lakini pia kwa wafanyabiashara ambao ni walipakodi wazuri kwa Serikali, mitambo yao muda mrefu inapokuwa haifanyi kazi wanapata wao hasara, lakini pia na Serikali inapata hasara kwa kutopata zile kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ni-declare interest katika eneo hili na mimi ni mhusika. Mimi nina mashine mbalimbali za kusaga, kukoboa na ku-grade, lakini muda mrefu unaweza kukuta kwa wiki mara nne hazijafanya kazi kabisa umeme haupo. (Makofi)

Kwa hiyo, unapata hasara mfanyabiashara, lakini pia Serikali inapata hasara, lakini umeme ule unaporudi mara nyingine unaunguza vyombo mbalimbali, kwa sababu unarudi ukiwa hauja-stabilize na gharama hiyo TANESCO kulipa sio rahisi huwa hawalipi, kwa hiyo wananchi na wafanyabiashara wanapata hasara sana, kwa hiyo naomba muangalie katika hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mheshimiwa January aliongelea hapa suala kuhusu mkataba ule wa gesi ambao umesema mazungumzo yameendelea vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hii gesi watakapokuwa wamefanikiwa ionekane kweli ina faida kwa wananchi kwa sababu inaweza ikaletwa gesi lakini gharama zake ni kubwa na huku tunasema tuondoe utumiaji wa nishati hizi halisia kama miti na nini kwa sababu ya uharibifu wa mazingira, lakini kama hii gesi ambayo wanaendelea kufanya mchakato wake itaendelea kuwa ghali itakuwa hakuna faida, wananchi wataendelea kukata miti na vitu kama hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya machache, naunga mkono hii hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)