Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Selemani Jumanne Zedi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukene

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Bukene niweze kuchangia hotuba hii muhimu ya Wizara ya Nishati. Nitaanza na Miradi ya Umeme Vijijini (REA).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu la Bukene kabla ya mwaka huu, mwaka uliopita lilikuwa limeunganishiwa umeme vijiji 25 kati ya vijiji 81 vilivyopo katika jimbo langu na vijiji 56 vilikuwa bado havijapata umeme, lakini kuanzia mwaka jana mkandarasi Silo Power yuko site na anaweka umeme kwenye vijiji vyote 56 vilivyokuwa vimebaki. Nafahamu kwamba, speed yake kwa sasa sio nzuri, nilitembelea maonesho ya nishati wiki iliyopita hapa Bungeni nikakutana na mkandarasi na alitoa maelezo kwamba, ana changamoto ya mabadiliko ya bei kulingana na mkataba wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina taarifa kwamba, Wizara ya Nishati imeshakaa na wakandarasi ili kupata ufumbuzi wa tatizo hilo, kwa hiyo, ni matumaini yangu kwamba, tatizo hilo litakwisha na kasi ya mkandarasi sasa kuweka umeme kwenye vijiji hivi 56 itaendelea kama ilivyoanza. Matumaini yangu ni kwamba, mwisho wa mwaka huu vijiji vyote vitakuwa vimeshapata umeme kwa hiyo, kimsingi ni kwamba, kazi hii ikikamilika jimbo langu lenye vijiji 81 vyote vinakwenda kupata umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na vipaumbele ambavyo Mheshimiwa Waziri amevitaja kwenye hotuba yake na kipaumbele kimojawapo ni kwamba, sasa wanakwenda kuanza kazi ya kupeleka umeme kitongoji kwa kitongoji. Ilivyo sasa hivi, tunapeleka umeme kwenye vijiji, lakini kimsingi kijiji kinakuwa na vitongoji kadhaa. Kwa mfano, jimboni kwangu kuna Kijiji kinaitwa Kagongwa, Kijiji ni Kagongwa, lakini Kagongwa ina vitongoji saba na hapa mkandarasi anapeleka umeme kwenye vitongoji viwili. Kwa hiyo, unakuta Kijiji cha Kagongwa vitongoji viwili ndio vina umeme, vitano vitakuwa havina umeme, lakini ukihesabu vijiji vilivyopata umeme Kagongwa utaihesabu, lakini kumbe Kagongwa yenye vitongoji saba ni viwili tu ndio vinakwenda kupata umeme. Kwa hiyo, naunga mkono hicho kipaumbele cha Wizara cha kuhakikisha kwamba, sasa inaondoka kwenye ngazi ya vijiji, inakwenda kupeleka umeme kitongoji kwa kitongoji na hicho ndio kitakuwa kipimo sahihi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la kupandishwa kwa bei ya kuunganishwa umeme. Wote tunafahamu kwamba, maeneo ya vijijini gharama ya kuunganisha umeme ni Sh.27,000, lakini hivi karibuni yalitokea mabadiliko kwa baadhi ya maeneo ya vijijini yakapandishiwa hiyo gharama. Kwa mfano, katika Jimbo langu la Bukene kuna vijii vitatu, Kijiji cha Bukene, Kijiji cha Itobo na Kijiji cha Mambali, vimepandishiwa bei ya kuunganishiwa umeme kutoka Sh.27,000 sasa hivi mtu ambaye yuko ndani ya mita 30 ambaye hahitaji nguzo kutoka Sh.27,000 anatakiwa alipe Sh.320,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwatendei haki kwa sababu, haya ni maeneo ya vijijini. Bukene bado ni kijiji, kina Mwenyekiti wa Kijiji, kina Serikali ya Kijiji, Itobo hivyohivyo, Mambali hivyohivyo, maeneo yote haya ni vijiji, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake nafurahi kwamba, ametambua kwamba hii ni kero na amepata malalamiko mengi na ametuma timu ya wataalam na ametoa time frame ya miezi sita kwamba, hawa wataalam wampe feedback.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba, haya maeneo yote ambayo ni vijiji, kwa mfano Bukene, Mambali, Itobo, pamoja na kwamba, ukiyaona yanafanana na miji, lakini bado ni vijiji. Yana Serikali za Vijiji, yana Wenyeviti wa Vijiji, kwa hiyo, yalipishwe sawa na vijiji vingine gharama ya Sh.27,000 ili kuondoa ubaguzi wa kijiji kwa kijiji kwa sababu, wote wanalingana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nimeliona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati ni kuwa, Wizara imetenga bilioni tano kwa ajili ya kuanza sasa utekelezaji wa mambo kadhaa katika Mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima mpaka Tanga. Kama ambavyo nimekuwa nikisema jimboni kwangu pale ndio kuna kituo kikubwa cha courting yard ambako mabomba yote, vipande vyote vya mabomba elfu 86, vitalazimika kufika pale Sojo, jimboni kwangu kupakwa rangi maalum ili vitakapofukiwa chini visioze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mojawapo ya kazi ambazo Mheshimiwa Waziri amezizungumza kwenye Wizara yake ni kwamba, mwaka huu amepata fedha ambazo zitatumika kutoa elimu kwa jamii inayozunguka mradi ule ili kuwafahamisha kuhusu fursa mbalimbali zinazokuja na mradi ule. Sasa pale jimboni kwangu wananchi wafanyabiashara tuko tayari kuchangamkia hizi fursa. Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba, Wizara ya Nishati ikishirikiana na Wizara nyingine, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara za Uwezeshaji kwamba, sasa hivi shughuli pale imeanza kidogokidogo kuna kampuni imeshaanza pale kufanya shughuli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna haja ya kuwatambua sasa hawa wafanyabiashara wa ndani, wazawa wa maeneo yale, kuwaeleza fursa zilizopo pale na kuangalia wana changamoto gani. Wengine wana changamoto za kimitaji, waweze kusaidiwa wapate mitaji ili waweze kushindana na kupata kazi zitakazokuja na fursa ya hili bomba la mafuta. Pale kutakuwa na kazi za usafirishaji, kutakuwa na kazi za kulipa vyakula, kazi za ulinzi na kazi mbalimbali, kwa hiyo, matumaini yetu ni kwamba, sisi ambao ni wakazi ambao tunazunguka maeneo yale ndio tuwe wa kwanza kunufaika na fursa ambazo zitapatikana pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kunufaika na hizo fursa kama tutaachwa tu tushindane na watu wengine, kwa hiyo, kuna kila haja kama Mheshimiwa Waziri alivyozungumza kwenye hotuba yake kwamba, amepata fedha sasa ambazo wataalam watakuja katika maeneo yale, watatueleza fursa zilizopo, watatambua sasa wafanyabiashara, wazabuni na wazawa mbalimbali ili kutatua changamoto zao na kuwawezesha kuchangamkia hizo fursa. Sisi tuko tayari kabisa kuchangamkia fursa hizo ili tuweze kunufaika na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina hofu na hili, uwezo wa Mheshimiwa Waziri Makamba naufahamu siku nyingi na najua haya mengi ambayo amesema ataya-deliver, lakini chini ya usimamizi makini wa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan, sina hofu, najua changamoto zilizopo zitatatuliwa ili sekta hii ya nishati iweze kupatiwa msukumo unaohitajika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kwetu kule hii nishati maana yake ni uchumi. Maeneo ya vijijini kule, kwa mfano, sasa hivi jimbo langu kutokana na uwepo wa nishati ya umeme sasa hivi shughuli nyingi za uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao zinaongezeka. Kule kwangu miaka mizuri ya fedha sisi ni wakulima wazuri sana wa mpunga, lakini miaka yote kabla hatujapata umeme, mpunga wote tulikuwa tunaupeleka Kagongwa kule, Kahama Mjini kwa ajili ya kuchakatwa kuwa mchele. Kwa hiyo, tulikuwa tunapoteza fursa za kiuchumi, lakini sasa hivi maeneo ya jimbo langu kule baada ya umeme kupatikana, wawekezaji wamekuja, wamewekeza, wana mashine kubwa za kisasa za kuchakata mchele na sasa hivi hatuuzi mpunga tena tunaongeza thamani, tunauza mchele na kupata faida kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante. (Makofi)