Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Jesca David Kishoa

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza kabisa niuelekeze mchango wangu katika Shirika letu la TPDC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna msemo unasema hivi, to realize the value of what you have imagine you have lost it. Ili tuweze kujua mchango wa TPDC kwenye sekta ya nishati tufikirie kuipoteza TPDC kwenye sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vyovyote vile tusitegemee TPDC inaweza kufanya vitu vikubwa na vizuri kama haijawezeshwa vya kutosha. TPDC leo hii inadai TANESCO zaidi ya bilioni 500, hizi ni fedha nyingi sana. Wakati inadai TANESCO deni la bilioni karibu 600 wanamchukua TPDC kupitia kampuni tanzu ya TANOIL wanamwingiza kwenye market sharing kwenye biashara ya mafuta. Tafsiri yake ni kwamba, ni kama unamchukua mtoto wako unamfunga miguu na mikono, halafu unampeleka kwenye ulingo akapambane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, TPDC kupitia kampuni tanzu ya TANOIL inaagiza only 2% ya mafuta yote yanayoletwa nchini kila mwezi, yaani katika tani laki tatu zinazokuja kwenye nchi kila mwezi TPDC wanaingiza tani elfu ishirini peke yake. Huyu TPDC kupitia kampuni tanzu ya TANOIL anawezaje kupata muscles kwenye negotiation ya price kama asilimia ya kuingiza mafuta ni only 2%? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri mambo kadhaa; kwanza ni muhimu sana Serikali ikaingilia kati deni hili la TPDC kudai TANESCO. Wanaweza wakatenga kiasi kidogo cha ruzuku wakaweza kupunguza ukubwa wa deni hili. Pia kuna haja ya kubadili sheria zetu kwenye Petroleum Act tukaona kwamba, badala ya fedha yote inayopatikana TPDC kupelekwa Hazina, basi ikishafika Hazina irudi kwa ajili ya kusaidia shughuli za TPDC. Ni muhimu sana kwa sababu TPDC ikiwezeshwa ndio muarobaini wa kudumu wa changamoto ya mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa mwisho kwa upande wa TPDC, ni muhimu sasa ule ujenzi wa vituo vya uhifadhi wa mafuta ukamilishwe kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kwa ufupi ucheleweshwaji wa Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere. Taarifa ya Kamati iko very clear, sababu zinazotolewa na Serikali ambazo zinaonesha ucheleweshwaji wa Mradi wa Julius Nyerere, sababu hizi hazitoshi. Sababu hizi hazitoshi kwa sababu leo tunaambiwa Mradi wa Julius Nyerere umechelewa kukamilika eti kwa sababu za kimazingira. Ninavyofahamu hakuna mradi wowote ambao unaweza ukatekelezeka bila kufanyika feasibility study, lakini pia najua hakuna mradi wowote ambao unaweza ukakamilika bila kufanya environment impact assessment. Haiwezekani mradi wa over six trillion uwe na kikwazo cha kimazingira, kwanza ni aibu hata taarifa hii kuwepo kwenye documents za Serikali kwa sababu, inaonesha namna ambavyo hatuko smart. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaambiwa sababu nyingine ni Covid-19. Leo naomba niseme Covid-19 imekuwa ikitumika mara nyingi kama kichaka cha kuficha uovu ambao unaendelea kushindwa kutekeleza miradi mbalimbali ya Serikali. Kama kweli sababu ni Covid-19 basi tuambiwe, ile scope time kwa sababu, inaonekana ule muda ambao wanasema umesababishwa na Covid-19 hauendani kabisa na uchelewaji, tumechelewa zaidi ya mwaka mzima. Tunahitaji tuambiwe very specifically, hiyo mitambo wanayosema kwamba, imeagizwa na ikachelewa kuja kwa sababu ya Covid-19 kwanza ni mitambo gani na evidence tupewe kwa sababu, inasikitisha sana miradi mikubwa kama hii ambayo ina nia ya kutaka kututoa kwenye changamoto ya umeme kushindwa kutekelezeka kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa haraka haraka nijielekeze sasa kuchangia eneo la global agenda kubwa ya duniani kwa sasa inayohusiana na masuala ya energy transition. Wote tunajua katika hii dunia tumekuwa tukiishi na kunakuwa na vipindi vinapita; kulikuwepo mwanzoni kuna kipindi cha renaissance, wanaojua historia karne ya 14, kikaja kipindi cha enlightment karne ya 17, kikaja kipindi cha industrial revolution, kikaja kipindi cha globalization, kimekuja kipindi sasa cha fourth industrialization ambapo hapa tunazungumzia masuala ya artificial intelligence, tunazungumzia masuala ya internet na tunazungumzia masuala ya energy transition. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika kipindi hiki unapozungumza energy transition haya ni makubaliano ambayo yamefanywa na Wakuu wa Nchi mbalimbali duniani kutaka kuangalia njia mbadala ya kuweza kuokoa dunia na athari hasi za tabianchi na mazingira na ndio maana kumekuwa kukifanyika mikutano mikubwa duniani. Umefanyika mkutano wa Paris Agreement mwaka 2016, lakini pia kuna Mkutano wa Scotland Cop26 wa mwaka 2021 ambao lengo kubwa la mikutano hii na huu Mkutano wa Scotland Cop wa 26 alihudhuria Mheshimiwa Rais mwaka jana, lengo kubwa la makubaliano haya wamesema kwamba, wanataka sasa dunia iwe na joto lisilozidi 1.5 centigrade. Njia wanayoitumia wanasema wanataka kutumia njia ya kusitisha matumizi ya nishati chafu ambayo ni fossil.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nina vitu nataka nishauri hapa. Kama kuna kipindi tunatakiwa kuipa kipaumbele kwa nguvu zote taasisi ya Serikali ya GST ni sasa. Nasema hivyo kwa sababu gani; sisi tuna critical minerals, hizi critical minerals ndio zinazohitajika sana kwenye soko la dunia sasa hivi kwenye madini, kwa sababu moja, ndio madini yanayotakiwa kutumika kutengeneza miundombinu ya nishati safi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia umeme wa upepo unatengenezwa kwa kutumia turbines. Turbines inatumia madini ya copper, ukiangalia mabetri ya magari yanatengenezwa kwa kutumia madini ambayo yanaitwa graphite, kwa hiyo, haya madini yote na mengi sana yapo nchini Tanzania, lakini tuna changamoto kubwa moja, GST ambao ndio watafiti wakubwa wa madini katika nchi yetu hawawezeshwi. Ndio kwanza bajeti yao wametengewa bilioni 3.5 na hii ni OC peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri, ile helicopter iliyokuwa inazurura majuzi hapa kwenye mikoa mbalimbali ipelekeni GST ikafanye kazi kwa ajili ya kuchunguza madini haya yanapatikana wapi. Itakuwa sio mara ya kwanza, tuliwahi kuwa na helicopter sisi 1990 huko miaka ya nyuma na ilifanya kazi kubwa. Ni vizuri sasa hivi tunapotaka kutafuta madini haya ambayo yanaweza kutunufaisha kwenye nchi yetu, vitu kama hivi vitumike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Tanzania ni watano duniani kwa madini ya graphite ambayo ndio yanahitajika sana kwa sasa, lakini yako wapi? Ni jitihada gani Serikali imefanya kuyatafuta? Tunategemea taarifa kutoka kwenye kampuni za madini, haiwezekani. Tutafute madini haya ili yaweze kutusaidia kwenye kutengeneza miundombinu ya nishati safi ambayo ndio agenda kubwa duniani kwa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna changamoto GST hakuna watumishi. Ni vema idadi ya watumishi ikaongezeka ili wafanye kazi kwa uhakika zaidi. Itakuwa ni aibu sana pamoja na rasilimali kubwa hii ambayo Mwenyezi Mungu ametupa ya kuwa na madini ambayo ndio yanahitajika kwa sasa, critical minerals, halafu bado tukaendelea kuyakalia, tukaendelea kuyafunika na tusijue namna ya kutumia na wakati kufikia mwaka 2025 kama tutakuwa vizuri kwenye kuyatafuta, nchi ya Tanzania ndio inakwenda kuongoza dunia nzima kwa kutoa madini ya graphite, hizi ni tafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, naomba nigusie umeme wa upepo Mkoa wa Singida. Tumekuwa tukiimba wimbo huu kwa muda mrefu sana. Naomba tu ku-declare, pamoja na kwamba, duniani kwa sasa agenda ya matumizi ya nishati safi ni pamoja na nishati ya umeme wa upepo, lakini nashindwa kuelewa ni kwa nini Serikali imekuwa na kigugumizi kwenye utekelezaji wa Mradi huu wa Umeme wa Upepo Singida? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka nenda miaka rudi tumezungumza, toka miaka ya 2011/2012 mpaka leo hakuna kitu kilichofanyika hata nguzo moja hakuna. Tunaahidiwa miaka yote umeme wa upepo, umeme wa upepo, hakuna kilichofanyika. Watafiti wametafiti wakaona kwamba, umeme wa upepo wa uhakika katika ukanda wa East Africa unapatikana Singida na Makambako na una uwezo wa kuzalisha nishati ya kutosha, kwa nini kunakuwa na kigugumizi kwenye utekelezaji wa nishati ya umeme wa upepo Mkoa wa Singida? Wananchi wa Singida tumewakosea nini Serikali hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inazungumza vyanzo vingine vya umeme wa upepo inaacha kutaja Singida kwenye umeme wa upepo na wakati inajua kuna umuhimu wa kuwa na energy mixing kwenye uzalishaji wa umeme. Naomba Serikali kwa dhati kabisa na Mheshimiwa Januari Makamba aji-commit kwenye hili, wenzake wengi waliji-commit kwenye hili, lakini hakuna utekelezaji wowote. Do your part Mheshimiwa Waziri kwenye hili, afanye hili ili wananchi wa Singida wamkumbuke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.