Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kondoa Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
3
Ministries
nil
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuchangia mawazo yangu na wananchi wapiga kura wa Jimbo la Kondoa Mjini kama namna wanavyopenda itokee katika Wizara hii ya Nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na niishukuru Wizara kwa kazi kubwa ambayo inafanywa katika maeneo mbalimbali. Mimi ninaomba nichangie specifically kwenye Jimbo langu kwa sababu zipo changamoto ambazo zinawakumba wananchi wa Jimbo wangependa wapate majibu ya Serikali Wizara na mimi kama Mbunge wao nipate majibu hasa ya kuwajibu baada ya kuwa na changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja specifically nakwenda kwenye Kata inaitwa Bolisa kwanza ifahamike naongoza Jimbo la Mjini, Halmashauri ya Mji wa Kondoa kwa hiyo mimi nina mitaa sina vijiji. Ninayo Kata inaitwa Bolisa hii Kata ina mitaa mitatu ilipata mradi wa REA toka mwaka 2019, Mkandarasi aliyepewa kazi ile aliondoka mpaka wiki hii ndiyo niliambiwa amerudi lakini pamoja na kurudi kwenyewe bado kuna viporo ambavyo hakuvimaliza. Lakini ukiacha viporo ambavyo hakuvimaliza nimeambiwa kwamba scope yake imeisha lakini kuna mitaa miwili katika hiyo mitatu haikupata umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wananchi wa Kata ya Bolisa mara zote wanaipigia simu wakitaka kujua kwamba kwenye mradi wa REA ndiyo umeishia pale? Kwa sababu hata nilipohudhuria kwenye maonesho pale nilikutana na meneja wangu na watu ambao tumekuwa tukihangaika namna ya kuona tunaweza tukaukwamua ule mradi. Kwa hiyo, ningependa Mheshimiwa Waziri anisaidie kupata kujua ule mradi umeishia pale? Kama umeishia pale maana yake ni mtaa mmoja tu ambao ni nguzo zimefika pale, wananchi walishafanya wiring toka mwaka 2020 mpaka leo wanasubiria umeme, wana mashaka pia wanataka kujua mradi ule wa REA kama umeishia pale nyumba namba moja imewekewa umeme kwa Shilingi 27,000. Je, ile ya pili mradi ulipokomea wao watawekewa kwa 27,000 au watawekewa kwa hiyo 300,000?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nataka tupate kujua kwa sababu kuna changamoto kuna Kata inaitwa Suruke, Kata hii ina mitaa yake, Kata pamoja na mitaa hakuna nguzo hata moja iliyowahi kwenda. Kwa hiyo, ni Halmashauri ya Mji lakini Kata yote haina hata nguzo iliyosimama kwenye ardhi ya Kata ile. Katika kufuatilia sijaona hasa mpango hasa wa kuona kwamba Kata ile ni lini hasa itapelekewa umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekutafuta Mheshimiwa Waziri sikupata bahati ya kukutana na wewe lakini nilikutana na Mheshimiwa Naibu Waziri, akawa amewasiliana na Mkurugenzi Ndugu yetu Seif lakini nawashukuru yeye Engineer Seif pamoja na Kasomambutu walifanya mawasiliano walikwenda kutembelea hiyo mitaa ninayoisema waliona hali halisi. Sasa nitaka kujua hii Kata hasa ya Suruke na yenyewe itapelekewa umeme kwa maana ya REA au tunategemea kuwapelekea kwa zaidi ya shilingi 300,000 au shilingi 600,000, shilingi 900,000 au shilingi 1,000,000? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni hili la utata wa bei ya kuwaunganishia wananchi umeme, ni kweli ile ni Halmashauri ya Mji ina mitaa badala ya vijiji lakini ndugu yangu kutoka katikati ya mji unakwenda hizo Kata ni kilometa nyingi na kazi pekee inayofanyika kwenye Kata zile ni kilimo na mifugo. Maana yake siyo tu vijiji vinavyokua bado ni vijiji mno, mwananchi anajenga nyumba yake kwa kipindi cha miaka mitatu au minne sana katumia gharama kubwa 200,000 leo ukimwambia mwananchi huyu ukamuunganishie umeme kwa shilingi 300,000 bila nguzo akiongeza mita 60 shilingi 600,000 yule mwananchi hana uwezo wa kulipa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia hata watumishi tu Walimu hivi kweli mtu anaweza kuunganisha umeme kwa hali ilivyo katika vijiji vyetu, hii mitaa yetu ambayo miji tunataka tuikuze kwa gharama hiyo? Kwa hiyo nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri hebu ule mpango mlioutaja kwenye hotuba yenu ya kufanya utafiti kuona kama watu hawa wanaweza wakagharamia hiyo ni vema ukafanyika mapema. Hapa mimi ninashauri Kamati utakayoiunda itakwenda miezi sita lakini wananchi tayari walishajiandaa miaka mitatu iliyopita kuupokea umeme na ninaamini nchi hii ni kubwa mimi nikurahisishie tu kwa Jimbo langu la Kondoa Mjini. Jimbo la Kondoa Mjini ni Mji ambao unakua bado hauna ile hadhi kubwa ya kusema kwamba wananchi wenye kuishi hapa ni watu wenye uwezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mitaa ambayo naomba niitaje sasa hivi ni mitaa ambayo ipo vijijini kabisa ambapo hakuna mwananchi nikiangalia mmoja mmoja wa kulipa zaidi ya hiyo 300,000 au 600,000 kwa sababu asilimia kubwa watu hawa wanahudumiwa na mpango wa TASAF. Sasa najiuliza mtu unamsaidia kula asubuhi, mchana na jioni kwa kutumia TASAF anawezaje kuingiza umeme kwa hiyo pesa? Lakini sote tunakubaliana ukipeleka umeme kijijini maana yake unakwenda kuinua uchumi wa wanavijiji wale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia maeneo mengi ambayo mmepeleka umeme vijiji vile vimebadilika kabisa katika shughuli za kiuchumi, badala ya watu kulima wameweza kufungua viwanda vidogo vidogo, wameweza kufungua saloon na vitu kama hivyo. Kwa hiyo, kwa sababu nchi yetu ipo katika uchumi wa kati ni vema sasa mitaa hii tusiibague kwa kusema tuwafungue umeme kwa gharama kubwa kwa sababu kuwapelekea huduma ya umeme ni kuwasaidia kuwakwamua kiuchumi, kwa sababu nchi yetu ipo katika uchumi wa kati tunaamini sasa tutaendelea kuulinda huo uchumi wa kati kwa kuwapelekea wananchi umeme maeneo yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huwa naona aibu sana ninapofanya ziara kwenye Jimbo la Mjini halafu unakwenda Kata nzima hata nguzo haina kwangu inakuwa ni shida sana. Tunaitaje Mji hali ya kuwa hakuna mwanga kuna giza wakati wote? Naomba niitaje hii mitaa ili Mheshimiwa Waziri ayachukue mambo haya yangu siyo mengi ni matatu tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni huo mradi wa REA Kata ya Bolisa lazima ufike mwisho na wananchi wapelekewe umeme ili kupunguza kero kwa wananchi, jambo la pili ni kuiangalia hiyo Kata ya Suruke ambayo yenyewe Kata yote na mitaa yao hakuna hata nguzo iliyosimama kwenye ardhi ya Kata hiyo, maana yake siyo umeme tu hata nguzo haijasimama. Tuna mtaa wa Damai, tuna mtaa wa Kwantisi, mtaa wa Gubali, mtaa wa Hachwi, mtaa wa Chandimo, mtaa wa Serya, mtaa wa Dumi, mtaa wa Kwamtwara, mtaa wa Chemchem, mtaa wa Tampori, mtaa wa Ausia, mtaa wa Suruke, mtaa wa Guluma, mtaa wa Tungufu pamoja na mitaa ya Unkuku pamoja na Choyi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa fikiria ni Jimbo lenye Kata Nane peke yake mitaa yote hii haina umeme na tunasema hii ni Halmashauri ya Mji. Mimi Mheshimiwa Waziri ninakuomba ndugu yangu hakikisha waelekeze REA wakawasaidie, ule mpango wa TANESCO wa kwenda kusema unakwenda kujaziliza, TANESCO yenyewe bajeti yao ni ndogo wakipata nguzo 20 hazifiki popote. Leo Mji unapanuka maeneo ya karibu ya Mji, TANESCO wanaweza wakamudu kwa hizo nguzo 30, 20, 40 lakini mtaa mzima hauna umeme, Kata nzima na mitaa yake haina umeme hawa wanahitaji wasaidiwe mradi wa REA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaambiwa kuna hii nini Peri-urban, tunaisikia Dodoma tunaisikia Dar es Salaam, tunaisikia Arusha kwenye miji yetu ya Halmashauri huko kwa kweli hatuna matumaini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nina mashaka makubwa sana na kuwa na Halmashauri za Mji, leo mambo ya Halmashauri ya Mji yamekuwa ni ya kusubiri ninaogopa tutasubiri na huu umeme mpaka vijiji vyote vitakamilika. Kwa hiyo tutakuza vijiji tutasahau kuikuza mitaa yetu. Leo ukija kwenye maji Miji 28 tunaendelea kusubiri ukija kwenye tactic masuala ya barabara tunasubiri, ukija kwenye umeme tunaambiwa kuna huo mradi tofauti na REA ambayo tunajua ndiyo wanafanya vizuri sisi tunaendelea kusubiri! Hivi ni dhambi kuwa na Halmashauri ya Mji? Ninaunga mkono hoja na wala sina haja ya kushika Shilingi na nitaitikia ndiyo bajeti yao lakini wafahamu kilio hiki cha Mbunge mwenzao kinanisababishia mimi wakati mwingine nakimbia Jimboni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.