Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Dr. Christina Christopher Mnzava

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nimshukuru Mwenyezi Mungu kupata fursa ya kusimama kwenye Bunge lako Tukufu kuchangia Wizara ya Nishati. Ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya katika Taifa letu. Tulikumbwa na tatizo kubwa sana la mfumuko wa bei ya mafuta lakini Mheshimiwa Rais kwa jinsi anavyotuthamini Watanzania aliweza kutoa ruzuku ya Bilioni Mia Moja, kwa kweli tunampongeza sana kwa kazi kubwa ambayo anaifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwashukuru Wizara ya Nishati Mheshimiwa Kaka yangu Makamba, Watendaji wote na Wasaidizi wako wote kwa kweli mnafanya kazi kubwa sana. Tunajua dunia nzima ina changamoto nyingi na imepelekea mafuta kupanda bei, hili ni janga la dunia siyo janga la Tanzania peke yake. Baada ya Mheshimiwa Rais kutoa fedha kama ruzuku Shilingi Bilioni 100 leo Dodoma nimeenda kununua mafuta angalau yameweza kushuka bei kidogo kama Shilingi 120 hivi, kwa kweli ni juhudi kubwa ambayo inafanywa na Serikali yetu tunajua katika kila mafanikio changamoto hazikosekani tuwaombe sasa kwa bajeti hii ambayo iko mbele yetu ile mipango ambayo mmepanga, nimeona katika jarida hili ambalo mmetupatia mmeweka vipaumbele, ukivisoma hivi vipaumbele unapata matumaini kabisa kwamba Wizara hii inakwenda kufanyakazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijielekeza tu kwenye kipaumbele Namba Mbili cha bajeti hii ambacho kinasema kutekeleza miradi ya nishati vijijini pamoja na kuanzisha utaratibu wa kupeleka umeme katika vitongoji ndani ya nchi. Kwa kweli, suala la umeme hasa huu umeme wa REA vijijini imekuwa ni changamoto kubwa sana. Unakuta kuna Kata ambazo ziko kwenye Manispaa mfano kule Shinyanga, kuna Kata ambayo iko karibu kabisa na grid ya Taifa, pale Ibadakuli ambapo umeme uko pale grid ya Taifa iko pal,e lakini vijiji na vitongoji vya pembeni havina umeme. Hili suala kwa kweli linaumiza sana wananchi wakati mwingine anakuuliza swali unashangaa, anakwambia grid ya Taifa hii hapa ambayo inasambaza umeme kwenda Mwanza, ambayo inapeleka umeme Kahama, ambayo inapeleka umeme Mikoa mingine sisi hapa tunaotoka katika kata ya Ibadakuli hakuna umeme! Kwa kweli huwa inaumiza sana kuona kwamba wananchi wanapata shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu kubwa nyingine ni nini? Ni kwa sababu wale wako ndani ya Manispaa wanahesabika kama wako Mjini lakini kiukweli ni kwamba wako kijijini. Vijiji vile ambavyo viko ndani ya Manispaa ningeomba huo utaratibu wa Peri-urban ambao tunausikia mnausema kila wakati lakini utekelezaji wake bado unasuasua. Tunaomba vijiji vyote ambavyo viko ndani ya Halmashauri za Miji au Halmashauri za Manispaa ziweze kupatiwa umeme ili hawa wananchi na wenyewe waweze kufaidika na suala zima la kukuza uchumi. Kwa sababu tunajua umeme ndiyo chanzo kikubwa cha kuhakikisha kwamba vijana wetu wanajiajiri, wengi wamefungua viwanda vidogo vidogo kwa ajili ya kutengeneza mageti, wengine wanachomelea magari, wengine wanatengeneza majiko bila kuwa na nishati ya uhakika ya umeme hawawezi kufanya kitu chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho nataka kukizungumzia ni suala zima la kukatika umeme. Kwa kweli inasikitisha, Wizara mnatufanya tunapata hasara, kwa sababu kama una kiwanda na una shift unalipa wafanyakazi, unategemea wafanyakazi wengine waingie Saa 12 mpaka saa Nane, wengine waingie Saa Nane mpaka usiku, wengine waingie usiku Saa Nne mpaka asubuhi, umeme unapokatika ina maana uzalishaji unadorora, lakini mwenye kiwanda hataacha kuwalipa wale wafanyakazi, matokeo yake nishati inazorota umeme unakatika wanaamua kuwapumzisha vijana ili kubana matumizi. Wenye viwanda wakishabana matumizi tayari wale vijana wanarudi mtaani wanakuwa hawana ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka tujue Mheshimiwa Waziri unapokuja kuhitimisha, tunataka tujue utaratibu wa kudumu mpango mkakati wa kudumu ambao utawezesha huu umeme ukawa stable, kwanza mnatutia hasara unawasha TV, umewasha friji baada ya muda umeme umekatika unarudi unakatika unaweza ukakatika hata mara nane kwa siku, kwa kweli hii haikubaliki ninaomba kabisa Wizara ya Nishati ije na majibu mazuri na mpango mkakati mzuri, umeme wa uhakika mwanzoni tulikuwa tunajua labda wakati mwingine maji sijui katika Bwawa la Mtera yamepungua, mara sijui vitu gani! tunataka mtuambie gesi asili inatusaidiaje kuhakikisha umeme unakuwa stable, mabwawa yanatusaidiaje kuhakikisha umeme unakuwa stable, hizi grid zetu za Taifa zinatusaidiaje kuhakikisha kwamba umeme unakuwa stable? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mengi wameyafanya katika hii Wizara, kwa kweli hata maneno mengi ya kuongea ninakosa kwa sababu hapa wametu-pre-empty wametupa mpango mzuri, wametupa vipaumbele, wametupa way forward, sasa tunaomba haya mliyoyaandika yatekelezeke, mwaka kesho tukiwa hai kipindi cha bajeti hii ya Wizara ya Nishati, hii itakuwa reference na mkishindwa kuitekeleza hii itabidi tuwaulize tushikiane Shilingi hapa, tuminyane tushikane mashati ili kuhakikisha kwamba wananchi wa Tanzania wananufaika na nishati ambayo Mwenyezi Mungu ametujaalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, ninahitaji kusikia majibu ya uhakika, ahsante sana. (Makofi)