Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami leo niweze kuchangia kwenye bajeti hii ya Wizara ya Nishati. Kwanza binafsi nimpongeze Mheshimiwa Rais lakini pia nipongeze Wizara kwa kazi nzuri ambazo zimeendelea kufanyika na pongezi hizi zinaenda hasa kwenye uendelezaji wa Bwawa letu la Mwalimu Nyerere, sisi kama Wajumbe wa Kamati tumeweza kufika kule site na tumeona development kubwa sana ya ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Kwa kweli tunapongeza kwa sababu tumeona kazi zinazoendelea kufanyika pia tumeona fedha ambazo zinatolewa kwa hiyo binafsi tunawapongeza sana na tunaamini kama Kamati tumewaomba Wizara walisimamie na Bwawa hili liweze kukamilika kwa haraka zaidi. Kwa hiyo, tunaomba sana Wizara mlichukulie kwa umakini na kuhakikisha kwamba mwakani 2023 tuweze kupata megawatt 2,115 kutoka kwenye Bwawa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi changamoto ambazo tunazo leo tukipata megawati hivi kutoka kwenye hili Bwawa la Mwalimu Nyerere tutaongeza umeme mwingi sana kwenye Gridi ya Taifa. Lakini pia katika master plan yetu ya Taifa hadi kufikia mwaka 2025 tunatakiwa tuwe na umeme megawati 5000. Kwa hiyo hadi sasa hivi tunazo megawati 1,600 tukichukua na lile la Bwawa la Mwalimu Nyerere 2,100 maana yake tutakuwa na around 3,000 na something, lakini pia kutokana na hivi vyanzo mbalimbali tulivyonavyo tumeona kabisa tunakaribia 4,000 bado tuna upungufu wa megawati karibu 1,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaiomba Wizara ihakikishe kwamba vyanzo vinavyosababisha kuzalisha umeme wa ziada hasa kwenye gesi, lakini pia kwenye vyanzo vingine vya jotoardhi tuwekeze kule kwenye maeneo hayo ili tuweze kupata megawati za kutosha kwa sababu kuwepo kwa umeme mwingi utatusaidia kuhakikisha kwamba kunakuwa na uhakika wa upatikanaji wa umeme, lakini pia tutahakikisha kwamba hata miradi yetu mikubwa kama SGR inaweze ku-operate bila kuwa na kukatikakatika au kutokuwepo kwa umeme wa kutosha, lakini pia hata kusambaza kwa nchi jirani lazima tuwe na umeme wa kutosha kusambaza na kuwauzia nchi jirani ambazo zinatuzunguka kama Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi lakini pia Malawi ni masoko ambayo lazima tuyachukue kama Taifa na hasa ukizingatia mipango ambayo tunayo kama Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kingine Mheshimiwa Waziri nikupongeze tu, tunajua sasa hivi tuna changamoto kubwa ya mafuta katika soko la dunia, lakini pia kumekuwepo na upandaji wa bei ya mafuta duniani kote, tumeona changamoto hizi katika nchi kama Marekani, lakini pia tumeona nchi kama Uingereza, lakini pia tumeona nchi kama Nigeria, pia wameweza kusimamisha ndege zao zisiweze kuruka kwa sababu ya changamoto hizi. Ukiachilia mbali huko lakini hata hapa nchi jirani ya Kenya tumeweza kuona ndugu zetu wakibeba madumu kwenye pikipiki wakipeleka sheli kuweka mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo unaweza kuona kwamba tatizo hili si dogo, ni tatizo kubwa tuwapongeze tu Wizara kwa kuhakikisha kwamba mafuta yameweza kupatikana ndani ya nchi yetu, uhaba ambao tulitarajia kwamba tungeupata, tungekuwa katika vituo vya mafuta hakuna hilo halijatokea. Kwa hiyo binafsi ninawapongeza kwa kazi nzuri, tumepata changamoto ya upandaji wa bei ya mafuta, tunatambua kwamba bidhaa yoyote inapokuwa na mgogoro duniani ni lazima changamoto zitokee katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu haizalishi mafuta na sisi tunaagiza kwa hiyo tunapoagiza ziko hizo changamoto tunawaomba tu PBPA waendelee kusimamia uagizaji wa mafuta na mafuta haya yaendelee kupatikana isitokee nchi yetu ikakosa mafuta, zipo nchi tumezishuhudia zinapata uhaba wa mafuta kama nchi ambayo nimeitolea mfano ya Kenya, nchi inakosa mafuta, nchi inapokosa mafuta maana yake unaangusha uchumi wa nchi, lakini sisi kama Taifa nchi yetu haijakosa mafuta hilo tunakiri na mafuta yanapatikana hadi kwenye maeneo yetu ya vijijini. Changamoto ni bei ambayo tunaishukuru pia Serikali kwa kuweka fedha shilingi 100,000,000 kuhakikisha kwamba ina-control upandaji wa bei hili suala kwa kweli tunawaomba sana liendelee kusimamiwa kwa ukaribu na kwa umakini kwa sababu ikitokea tu tukakosa mafuta kwenye nchi yetu ninaamini uchumi wa Taifa hili utaanguka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hawa PBPA wamefanya kazi ambayo ni nzuri kwa sababu tumeweza kuona nchi kama Zambia, Malawi, Rwanda, Burundi na Uganda wanatutumia sisi kama Tanzania kwa kupitia hii PBPA kuingiza mafuta yao kwenye nchi zao. Kwa hiyo wangeweza kutumia nchi nyingine, lakini wametumia nchi yetu maana yake tuna utaratibu mzuri wa kuagiza mafuta katika Taifa letu. Changamoto zilizopo au zinazojitokea nyinyi kama Wizara mzisimamie kuhakikisha kwamba mnadhibiti changamoto hizo kwa sababu ikitokea tukaacha ikawa holela tunaweza tukapata mafuta mengine machafu, tunaweza tukapata mafuta mengine yakawa sio bora yakaua magari yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hii ndio ambayo imesababisha tulipotoka huko kuwa na magari ambayo yanaharibika, tumetoka huko kulikuwa kuna malalamiko hadi tumefikia hatua tumepandisha mafuta ya taa kufikia bei ambayo ipo sawa au zaidi ya petroli na dizeli ni kwa sababu ya kudhibiti uchakachuaji wa mafuta. Hivyo basi tunawaomba udhibiti uendelee kusimamiwa kwa ukaribu, lakini pia uadilifu uendelee kuwepo kuhakikisha kwamba bidhaa hii adimu katika taifa letu inaingia na wananchi wanapata kile ambacho wanastahili ili kuweza kuhuisha uchumi wa watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimia Waziri katika hilo tunakupongeza, lakini uangalie changamoto zilizopo ili tunapoelekea tuweze kuziboresha na kuwa imara zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kingine ambacho nilitaka nizungumzie Mheshimiwa Waziri gharama za umeme katika maeneo yetu ambazo mlizitangaza hivi karibuni, lakini pia kwenye bajeti yako umeeleza kwamba utaunda Tume, itembelee maeneo yote nchini kuangalia bei za umeme. Nikushauri Mheshimiwa Waziri yapo maeneo ya kupandishwa kwa bei wakati mnapandisha bei mlivyosema tunapandisha basi hata ile bei ya zamani iliyokuwepo ikawa mmefanya double maana yake pale Igunga tulikuwa tunaingiza umeme kwa mita 30 shilingi 170,000; mlivyosema bei turudishe nchi nzima tulitangaziwa shilingi 27,000 ikashuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mlivyosema turudi kama zamani haikurudi ile shilingi 170,000 imeenda shilingi 320,000; kwa hiyo imekuwa tena gharama zaidi. Nikuomba Mheshimiwa Waziri haikuishia hapo, imeenda sasa hii bei hadi kijijini kwetu, kijiji cha Tomachankola na wao walipe shilingi 320,000, kijiji cha Nkinga na wao walipe shilingi 320,000, kijiji cha Simbo hivi kweli Mheshimiwa Waziri kweli vijiji hivi mnaenda kuwawekea shilingi 300,000 eti kisa tu wana kituo cha afya, eti kisa tu wana sekondari ya kata, eti kisa…

Mheshimiwa Waziri kuwa na sera ya kuwa na shule za sekondari za kata ni sera ya nchi nzima ni kwamba kila kata kuwepo na sekondari. Sasa isiwe adhabu kwa watu wetu, lakini pia kuwepo kwa vituo vya afya, tumepata fedha nyingi sana za vituo vya afya kwenye vijiji vyetu, kwenye kata zetu isiwe sababu ya kutuadhibu tukaenda kwenye bei ya shilingi 320,000. Nakuomba sana vijiji vinavyofanana na Chomachankola, Nkinga na Simbo visipelekwe kwenye hiyo bei, tunakuomba Mheshimiwa Waziri uturudishie kwenye shilingi 27,000 fedha hii tumeshaunganisha hii nchi umeme karibu maeneo yote hivi tunavyomalizia tumeshakula ng’ombe mzima tumebakiza mkia, tusiende kwenye lawama ambazo hazina sababu za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri rudisha kwenye vijiji vyetu bei ya shilingi 27,000; peleka kwenye makao makuu ya kata shilingi 170,000; peleka Manispaa paleka majiji lakini kwenye vijiji vinavyotambulika vijiji rudisha bei ya shilingi 27,000 kuhakikisha kwamba wananchi wanaweza kufurahia maisha yao.

Lakini nikuombe Mheshimiwa Waziri sisi pale Igunga umeme unakatika kama ambavyo maeneo mengine wamezungumza, lakini katika bajeti ambayo inatembea hii tuliwekewa kwamba tungejengwa sub-station ya kuweza ku-supply umeme pale Igunga. Lakini sub-station ile haijajengwa, tunaamini kwenye bajeti inayokuja tutapata hiyo sub-station ambayo ilikuwa imeshawekwa ijengwe pale Mbutu katika Wilaya ya Igunga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sub-station hii ijengwe ili kupunguza usafiri na usafirishaji wa umeme kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine umeme wa Igunga tunaupata kutoka Nzega yaani unatembea zaidi ya kilometa 150 kwenda kusambazia kufika Makao Makuu ya Wilaya, lakini pia kusambazia Wilaya nyingine zinakwenda mpaka Wilaya ya Uyui. Mheshimiwa Waziri hili suala kwa kweli kama ndio Igunga inafanyika hivi na maeneo mengine katika nchi ipo hivi maana yake ni changamoto kubwa sana na uhakika wa umeme hauwezi kuwepo kama hatutojenga sub-station kwenye maeneo haya nikuombe sana sub-station ijengwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Mheshimiwa Waziri sisi katika line hiyo kunapita nguzo zinapita kwenye majaruba na mji ya Igunga nguzo zinapita kwenye majaruba sio Igunga peke yake naamini maeneo mbalimbali katika nchi hii ambako nguzo zinapita kwenye majaruba, matokeo yake ni nguzo kuanguka kipindi cha masika, lakini pia kukatika kwa umeme, Mheshimiwa Waziri tuletee nguzo za zege, maeneo yote yenye majaruba weka nguzo za zege ili wananchi wawe na uhakika wa kupata umeme kiangazi pamoja na masika. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Gulamali kengele ilishapigwa.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)