Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipatia fursa ya kuhutubia bajeti ya kimataifa, unajua kuna bajeti ile ya wananchi, ilipita ile bajeti ya kitaifa, sasa hii ni ya kimataifa kwa sababu mambo yake ni dola, ni geopolitical, sijui ni migogoro ni Ukraine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilihudhuria maonesho ya nishati, lakini nimesikiliza vizuri hotuba ya Mheshimiwa Waziri na nimeisoma na viambatisho hivi, napenda nikiri kwamba kuna majibu mengi hapa kuliko maswali niliyonayo kutoka kwenye maonesho na kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, lakini kabla sijaanza kuhutubia nizungumze jambo moja; mwezi Januari, 2018 nilipata bahati ya kuhutubia Kabare, Uganda; Mheshimiwa Rais Jenerali Kaguta Museveni aliniomba nihutubie tena nihutubie kwa Kinyankole.

Mheshimiwa Mwenyekiti, alikuwepo Mheshimiwa Dkt. Kalemani, nikahutubia lakini Wizara ya Nishati wakanikaribisha Bunazi walikuwepo watu wengi na watu kutoka Nzega walikuwepo na kutoka Tanga walikuwepo na baadhi ya Wabunge, sikuona mahali popote ambako watu wa Uganda na Tanzania wanalalamika kwamba bomba la mafuta la kutoka Hoima kwenda Chongoleani lina matatizo, wala mimi katika Jimbo langu sijawahi kuona mahali watu wanalalamika kwamba watafukuzwa. Sasa hao wanaokwenda kutusemea huko Ulaya wametumwa na nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafuta ni ya Uganda, bomba ni la Tanzania; sisi na Uganda ni ndugu, mimi Rais wa Uganda Msita Waitabara ni mjomba wangu na alikuwa anaishi Jimboni kwangu kabla hajaenda kuwa Rais wa Uganda ni ndugu, kwa hiyo, watuache watuache. Lakini wale watu wanaosema bomba lisijengwe nimewapenda kitu kimoja, wanasema tupande miti bilioni tano, mimi ninakubali waje tutawapa eneo watupandie michikichi, watupandie mibuni, watupandie majani ya chai; miti bilioni moja sisi tutakwenda kuvuna wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye nishati; kwenye maonesho nashukuru kwa umeme visiwani off grid watu wa Mazinga, Ikuza, Kerebe, Gumbire, Nyaburo na Goziba suala la umeme nimepata majibu, lakini nimepata majibu kwamba REA II iliyokwama vijiji vya Busingo, Ruwanda yote itakuwa haina matatizo na miradi yote ya TANESCO itatengenezwa, nishukuru kwenye hotuba Mheshimiwa Waziri umekumbuka suala la campsite, vituo vidogo vinavyoondoa matatizo ya distribution ya mafuta, nashukuru Mheshimiwa Waziri ulikuwa Mwenyekiti wangu kwenye Kamati zetu tulilijadili sana sasa upele umepata mkunaji, ulishughulike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe jambo lingine umesema magari ya Wizara ya Nishati yatafungiwa gesi, mimi sikubali, magari yote ya Serikali yaanze kutumia gesi, zipo faida za kutumia gesi, gesi is economical, gesi is available, waanze kutumia gesi hiyo nimeisoma kwenye hotuba yako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumze mambo ya kidunia; suala la mafuta na mwenendo wa mafuta duniani; hili tunaomba uelewa Watanzania wote muelewe suala la mafuta halimhusu Mheshimiwa Rais wala halimhusu Waziri, wala halimhusu Mkurugenzi, ni suala la kidunia, sina muda ningezirudia zile sababu tano zinazosababisha hivyo, zipo nje ya uwezo wetu, na ninapozungumzia hiyo suala la uelewa nipende kuishukuru Serikali na hasa hasa Mheshimiwa Rais, kimsingi hoja sio bei ya mafuta imeshuka, bei ya mafuta haijashuka, bei ya mafuta imeshushwa, ukiangalia kwenye soko la dunia na nilikutana na mtaalam mmoja nilikuwa naangalia bei ya dunia inapanda, ila mamlaka imeshusha bei angalau kwa siku mbili hizi tupate afueni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uelewa wa Watanzania muelewe huko bado vumbi linatimka, bei ya mafuta inaendelea kupanda, ila mamlaka imeamua bei ishuke na hiyo ninaiita zawadi namba tatu, zawadi ya mama na hii ni zawadi ya mama namba tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze suala moja muhimu ambalo watu hawalielewi katika somo la mafuta; petroleum business management introduction huwa tunafundishwa availability, reliability na availability of mafuta ndio tunafundishwa. Sasa katika suala la availability kuna kitu Watanzania hatukijui, ni siri iliyo wazi kwamba sisi tunapata umeme asilimia 60 inatokana na gesi ya Songosongo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama isingekuwepo kutokana na vyanzo vya maji kutotosha tunge-import mafuta, kama ingetokea tatizo la supply/ disruption of supply ina maana tungeingia gizani mnasema mafuta yamepanda watu wanapiga kelele nawaambia Mungu apishe mbali ikitokea tatizo la umeme 60 percent kila mtu atatafutana. Kwa hiyo, tuipongeze Serikali, tuishukuru Serikali kwa kuwezesha hii gesi na tunapoishukuru gesi lazima uwakumbuke waasisi akina Sylvester Barongo na vijana wake wakati ule akina Mzee Ntomola, akina Kilagani, akina Khalifani na hapo ndipo ninapoipongeza Serikali ya Mheshimiwa Samia kwa kuwarudisha wakongwe kwenye sekta yaani uwarudishe wakongwe waje wakuoneshe njia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haikuwa rahisi kuchukua gesi ya Songosongo, sasa niwaambie kama sisi leo tungeingiza mafuta kwa bei hii, tungetumia trilioni moja kuagiza mafuta ya miezi minne; trilioni moja kuagiza dizeli ya kuendesha mitambo, sasa hoja sio trilioni moja, hoja ni kwamba foreign currency ungeipata wapi. Kwa hiyo wakati tunashukuru punguzo la bei huku kushuka kwa bei tushukuru kwa kuwepo na mfumo wa gesi asilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze bulk procurement; bulk procurement watu hawaielewi, Tanzania haijawahi kuwa soko la mafuta na nilikuwa nikilisema Tanzania haijawahi kuwa soko la mafuta, huwezi kumwambia international trader kwamba unataka tani 10,000; tani 5,000. Sasa hivi kutokana na bulk procurement consolidation ya maziwa yote makuu, mahitaji kupitia Dar es salaam sasa dunia inatambua kwamba Tanzania kuna soko la mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi tunashika mpini wao wanashika makali, watakuja hapa, watakuja hapa, sasa kwakuwa na wingi wa mafuta kama walivyosema Mbunge wa Manonga ndio maana hata mtikisiko unaompata South Africa, unaompata Nigeria, unaompata Kenya hautupati sisi na hiyo ni siri Waziri anajua na nasema Waziri usiisema kwa sababu tupo live watu wengine watakuja kuiba style yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi hatuwezi kuadimika mafuta kwa sababu ya mfumo wetu, asije mtu akakwambia rahisi, what is rahisi? Hakuna kitu cheap, cheap lazima kiwe pegged, kiwe pegged kwenye international kuna watu wamekwenda kuagiza mafuta cheap fedha zimeliwa, fedha zikiliwa za Serikali utamwambiaje CAG, hili Bunge utaliambiaje, lazima tufuate mfumo unaojulikana kama tunapata ya aghali tupate aghali, tuvumilie kesho tutapata nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengine nataka kuzungumzia ni trading hub, kidogo na hii nazungumza taratibu Mheshimiwa Waziri wasije wakawepo watazamaji kwingine kule, shangazi yangu nikamsalimia akakataa kuniitikia, kuna tofauti kati ya strategic reserve na trading hub.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ningeomba mlete mjadala, mlete semina sijakubaliana nalo. Strategic reserve inaweza ikawa ni trading hub na ninakupongeza umekubali kwamba tuweke bonded warehouse, sasa zitumie zile bonded warehouse ku-re-export kwenye enabling countries, nchi za Kongo kwenye madini kuna watu wanaweza kununua lita 500,000 kwa mpigo, waambie waje Tanga wanunue, waambie waende Dar es Salaam wanunue, nilikuwa nikifanya kazi hiyo unajua, tuna push volume. Kwa hiyo tuigeuze Tanzania soko, wanapokuja vijana wetu watapata kazi, lakini ile amari iliyopo kwenye ghala letu ndiyo hiyo strategic reserve. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemwambia Mheshimiwa Waziri akatikisha kichwa, tunahitaji mjadala tukae Wabunge tujadiliane na utaratibu utazingatiwa kusudi tunyukane hapa, kwa sababu hatuwezi kukubali hili suala lipite lina uzuri na ukali wake. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kenya juzi wamefanya mjadala juu ya hili walitoka bila kuelewana, OTS walikuwa na mjadala juzi walitoka bila kuelewana. Mambo ya aging, mambo ya kukamatwa na mafuta ya bei kubwa yakashuka, kwa jirani yameshuka wewe una mafuta ya bei kubwa utafanya nini, tunapaswa tuelezane kwa nia nzuri inayofanywa tutoke tumeelewana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine Tanzania tunayo storage capacity ya 1.4 billion liters kwa mwaka tunayotumia tuna storage capacity hiyo, 89 percent ni private sector, ninaiomba Serikali msiiache private sector, ndio iliyotufikisha hapa, hamasisha private sector wawekeze, Serikali weka uratibu, weka wadhibiti waweze kuelekeza. (Makofi)

Suala jingine naomba la utafutaji na uchimbaji wa mafuta, nishukuru unao wataalam Mzee Khalifani bosi wangu amerudi, tutafute mafuta mambo ya kuogopa ASPA sijui nini hakuna, usiogope lazima utapoteza na katika kupoteza utapata, hii ni biashara ya stara kubwa, ni biashara ya gharama kubwa, kwa hiyo, tuhamasishe kutafuta mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na sasa siyo siri kwa sababu ya kupanda kwa mafuta nchi za Ulaya wanakimbilia Afrika tumesikia hapa Afrika Magharibi, tungependa kusikia wanakuja Tanzania na wakija wape masharti, tunao vijana wamesoma hapa wamekwenda China wakasoma petroleum, mradi wa gesi haukufanya kazi waajiri watoto wale, waingize kwenye sekta ndio masharti kwamba njoo uwekeze, wekeza vijana wa Kitanzania waweze kufanyakazi, tafuteni mafuta, wakati wanatafuta green energy ni hadi 2050 sasa 2050 na sisi tutumie ndiyo maana na ninamuambia mjomba asikie huko aliko Kampala na Entebe tunataka mafuta ya Uganda yapite Tanga kusudi Tanga wafaidi na njia yote tufaidi, tufaidi na sisi tuchome gesi kama wazungu walivyochoma wakati sisi tumelala. (Makofi)