Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Vita Rashid Kawawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa. Kwanza naungana mkono na wenzangu kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na wataalam wote wa Wizara na Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, EWURA na Taasisi zote zilizo chini ya Wizara hii kwa kazi nzuri mnayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Wizara kwa maana ya Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Waziri kwa dhamira ya dhati ya kuongeza nguvu ya umeme na usambazaji wa umeme na utayarishaji, kuanzisha umeme katika maeneo mbalimbali ambayo kwa ujumla wake watakaoweza kuzalisha katika mwaka huu bajeti 2022/2023 megawatts 1,466 lakini zilizopo mbioni kwenye kukamilika ni megawatts karibu 2,380 ambayo ni Nyerere Hydro power, Rusumo megawatts 80 na Kinyerezi 185. Jumla yake zikikamilika na kwa sasa tuna megawatts 1,694 tunazozalisha kwa maji na gesi na biomass megawatts 1,694, jumla yake tutakuwa na megawatts 4,075.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa tulivyo megawatts 1,694 na matumizi ya juu kabisa ya umeme nchini ni megawatts 1,335. Kwa hiyo, hapa tukijumlisha na miradi hii iliyopo na ukaenda kukamilika nadhani mwishoni mwa mwaka huu na mwakani tutakuwa na megawatts 4,075, lakini tutakuwa na surplus ya umeme ya megawatts 2,740. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushauri wangu, sasa hivi tukishakamilisha hii miradi tu-concentrate katika kazi ya kusambaza kwa maana ya kusafirisha na kusambaza umeme na ile kufanya ile kazi ya National Grid Stabilization Project. Tukishamaliza miradi hii ya kuzalisha umeme, tutakuwa na megawatts 4,755, fedha nyingi tuzielekeze huko kwenye kusafirisha, kusambaza na stabilization za grid kwa sababu tutakuwa na surplus ya 2,740. Kwa hiyo, nadhani sasa hivi tukiendelea na concentration ya eneo hili itatusaidia sana kuwafikia wananchi vijijini ili waweze kufikia vitongoji vile tu-concentrate kwenye kukopa kwenye umeme wa kusambaza kwa wananchi vijijini badala ya kuendelea ku-invest kwenye uzalishaji wa umeme kwa sababu tutakuwa na surplus kubwa ya umeme katika kipindi hiki mpaka hapo tukiona hitaji linazidi kuongezeka basi tuendelee pamoja na kwamba policy or electric supply industry reform ile strategic road map inatutaka mpaka 2025 tuwe tunazalisha megawatts 10,000, lakini kwa sasa hivi mimi nadhani tukishafika hapo tu-concentrate na usambazaji na stabilization ya umeme vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, namshukuru Waziri walivyoleta timu yao hapa na nikaenda kuzungumza nao na wakanielewa, tuna proposal ya additional villages ambavyo vilirukwa katika vijiji vyetu na maeneo, tuna maeneo ambayo niliyasema ya maji. Serikali ina-invest fedha nyingi sana kwenye vituo vya maji, kwa maana visima kwenye vyanzo vya maji, lakini hakuna umeme katika vile vyanzo vya maji, tunatumia nishati ya mafuta ambayo ni very expensive. Kwa sasa hivi katika vijiji vya kwangu kule kwa mfano Ligunga, Lusewa wanalalamika na wanagoma kulipia kwa sababu wanashindwa kumudu gharama ya mafuta ili kusukuma maji yaweze kusambazwa. Kwa hiyo, ni vyema Serikali waka-concentrate sasa hivi kupeleka umeme katika maeneo ya vyanzo vya maji, kwenye vitongoji vyenye shule, zahanati na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru sana kwangu na vijiji na maeneo ya Ligunga pale nilishaeleza nilikubaliwa kwamba utashushwa umeme, kuna Sasawala Sekondari ambako kuna water pump pia, kuna eneo la Kijiji Zanzibar, Mchanjira, Likuwi Water pump, Selous Camp, Selous Sekondari, Vitongoji vya Mfuate, Rukimwa na Semu Zahanati, Magazine Sekondari lakini pia tuna Kituo cha Jeshi pale hakina umeme na kuna sehemu wana pump nazo hakuna umeme. Kwa hiyo, tutashukuru sana maombi yangu yale yakienda kutekelezwa ili tuweze kufanya kazi yetu ikiwa njema ya kusambaza maji na wapate huduma iliyo bora ya umeme. Nina imani sana na Waziri na Naibu Waziri kwa ubunifu wao, usimamizi wa kazi zao, tunaamini tutafika mbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, sisi katika East Afrika hapa kwenye suala la mafuta, Uganda mafuta wao kwa bei ya Tanzania ni Sh.3,468, Kenya baada ya ku-subsidize ikashuka mpaka Sh.3,001, sisi Tanzania Sh.3,148 na leo hii bei imeshuka naamini itakuwa imefika 3,000 kwa bei. Kwa hiyo, tupo vizuri na hii crisis iko dunia nzima, tuendelee kuwa wavumilivu, naamini kabisa Waziri na timu yake na EWURA wataendelea kuratibu vizuri suala hili la mafuta kwa nchi yetu. Hata hivyo, lazima tumshukuru Rais wetu kukubali kutoa bilioni 100 ambayo leo hii hapa kwetu bei imeshuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Watanzania tuendelee kuwa wavumilivu na tukiamini kwamba Serikali yetu imara ipo na inawajali wananchi na tutaendelea kuhakikisha kwamba tunasimamia vizuri bei hizi za mafuta. Kwa kushuka kwa bei ya leo naamini katika nchi za Afrika Mashariki tutakuwa chini zaidi. Kwa hiyo, nawaomba sana Wizara, Mheshimiwa Waziri waendelee kusimamia hivyo hivyo, waendelee kusimamia ule mfumo wa bulk procurement ambao unatuhakikishia kuwa na mafuta ya kutosha katika mwezi mzima na kidogo na tunaweza tukawauzia na wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ulikuwa huo, nakushukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)