Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Nishati. Kwanza nipende kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Mama yetu mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambayo ameifanya hadi leo mafuta yamepungua bei. Watanzania wafahamu mafuta si kama yamepungua bei, yameshushwa bei na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. Pia niwapongeze wataalam wa Wizara na nampongeza Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa smart kwa sababu hata kutuletea REA na TANESCO ndani ya Bunge ni kuonyesha jinsi gani ambavyo anatamani matatizo ya Wabunge yaweze kutatuliwa papo kwa papo, tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo ya kuchangia kwenye vipaumbele vyako 12 ambavyo tunavyo hapa, ninaweza nikaanza na kipaumbele Namba Moja, Namba Mbili na Namba 12 ndivyo nitakavyovizungumzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipengele Namba Mbili, Mheshimiwa Waziri umezungumzia kuhusu kutekeleza miradi ya nishati vijijini pamoja na kuanza utaratibu wa kupeleka umeme katika vitongoji vyote nchini. Mheshimiwa Waziri nizungumze wazi, utekelezaji wa REA kwenye sehemu kubwa ya Majimbo kipindi cha nyuma haukuwa mzuri sana. At least Makandarasi wa sasa japokuwa nao wapo wanaosuasua ila kwa Jimbo la Makete Mkandarasi wa sasa anaunafuu, lakini wale waliopita wana changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunalitekeleza hili, kabla hatujaenda kwenye kuangalia vitongoji, tufanye sensa ni Watanzania wangapi wamesuka nyumba kwenye Taifa hili na hawajaingiziwa umeme hadi sasa. Kwa sababu gani, umeme huu umeishia sehemu kubwa kwenye vituo vya afya na maeneo mengine. Watanzania wengi wamejitoa kwa moyo kusuka umeme toka mwaka 2019, 2018, 2020 lakini hadi sasa hawajaingiziwa umeme. Hao wangepewa special task kuangalia jinsi gani tunaweza tukawasaidia, wakaweza kupata umeme kwenye Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa ni maswali tukienda Wabunge kwenye mikutano wanauliza, mimi nimesuka Mheshimiwa Mbunge umeme utafika lini? Mimi nimesuka umeme utafika lini? Tunaomba sana mfanye sensa kwa Mameneja wetu wa Mikoa watuambie. Kwa mimi Makete tu nina kijiji cha Mago, na kijiji kama cha kule Matamba na vijiji kama vya Lupalilo, hivi vyote vinawakazi takribani zaidi ya 2,000 hadi 3,000 wamesuka umeme lakini hawajaingiziwa. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri kwenye jambo kama hilo uweze kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Makete tunalo Bwawa la Umeme la Mto Lumakalya. Ninyi mnaita Lumakalya lakini sisi ni Mto Luvanyila. Hili Bwawa la Mto Lumakalya ni bwawa ambalo linaenda kuzalisha zaidi ya megawati 222. Lakini pili tuna bwawa la Mto Luhuji, zaidi ya megawati 300, kwa maana kwamba megawati karibu nusu zinazotumika kwenye Taifa hili zinaweza zikaenda kuzalishwa ndani ya Mkoa wa Njombe. Ninakuomba Mheshimiwa Waziri, nimeona kwenye bajeti umenitengea Bilioni Nane, imani yangu ni kwamba hii Bilioni Nane ni kishika uchumba tu kwa sababu mradi una zaidi ya Bilioni 787 thamani yake. Kwa hiyo, ninaamini hii Bilioni Nane ni ya kuanzia tu. Nikuombe, wananchi wetu wamekuwa stranded kwa muda mrefu hawajui mradi unaanza lini. Pili tathmini ya gharama ambazo wananchi wanazunguka bwawa lile la Mto Lumakalya inafanyika lini ili wananchi wetu waweze kupewa fidia na waweze kupata fedha ambazo zitatokana na fidia za maeneo yale. Ninaomba sana huu mradi uweze kuanza, utakuwa umeandika Mheshimiwa January Makamba. Ninakuomba sana sana sana. Hii miradi miwili ikisimama inaweza kutusaidia sana katika kuondoa gap la umeme kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ninalotaka kulizungumzia Mheshimiwa Waziri ni kwenye Mikoa na maeneo kadhaa ambayo Serikali inatumia fedha nyingi kununua umeme na kuwapa umeme na wengine hawatumii umeme. Tunatumia fedha nyingi za Serikali kuhakikisha kwamba wanapata umeme. Kwa mfano, nizungumzie, tuna Mkoa kama wa Kigoma Mheshimiwa Waziri. Mkoa wa Kigoma wanatumia kwa mwezi 1.4 Bilioni kununua mafuta kwa ajili ya kuendeshea Mkoa ule umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuomba gridi ya Taifa iweze kwenda Kigoma. Wakati Serikali inatumia Bilioni 1.4 kununua mafuta, return yake ni chini ya Milioni 800. Kwa hiyo, tunatengeneza hasara zaidi ya Milioni 700 kila mwezi kwenye Taifa hili kwa ajili ya Mkoa wa Kigoma. Ni lazima uangaliwe kwa jicho la karibu Mkoa wa Kigoma ili tuondokane na hii debt ambayo tunaitengeneza kila siku ya kupoteza Milioni 800. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nenda Mkoa wa Kagera mimi nilikuwa Kagera juzi. Mkoa wa Kagera tunanunua umeme kutoka Uganda, megawati 10 tunanunua kutoka Uganda. Lakini megawati tano zinatumika na kiwanda cha Kagera Sugar. Megawati tano ndiyo zinatumika na Mkoa wa Kagera. Tunatumia zaidi ya Bilioni Moja na Milioni Mia Mbili kwa mwezi kununua umeme kutoka Uganda. Miundombinu ile siyo ya kwetu, ni miundombinu ya kutoka Uganda. Wakati huo huo pale tuna uwezo wa kutoa umeme Nyakanazi na tukapeleka Kagera na watu wa Kagera wakawa wameondokana na tatizo la umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, Kiwanda cha Kagera Sugar wanao uwezo wa kuzalisha zaidi ya megawati 25 na waka-supply kwenye Mkoa wa Kagera. Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri zungumza na watu wa Kagera Sugar waweze kukusaidia jinsi gani ya kutatua na uzuri mitambo wanayo, wanachokwama ni sheria za nchi zinawazuia kuwauzia umeme watu wa gridi ya Taifa, lakini hapo anao uwezo wa kukupa megawati 20 na ukatatua tatizo la kununua umeme Uganda ambapo tunapoteza over 1.4 billion, 1.2 billion kununua umeme. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Mkoa wa Katavi tunanunua umeme kutoka Zambia. Tunatumia over 1.5 billion kununua umeme kutoka Zambia, lakini watu wa Katavi na Sumbawanga wanao uwezo wa kupata gridi ya Taifa ili tukaondokana na fedha hizi nyingi ambazo tunatumia kununua umeme kutoka nje. Ninakuomba Mheshimiwa January Makamba, imekuwa ni muda mrefu Mikoa hii wanahangaika na umeme, tunaomba utusaidie, Watanzania hawa wapate umeme wa ndani na hizi fedha ambazo tunapeleka kwenye Mataifa mengine tuweze kutatua changamoto za Watanzania ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha Mheshimiwa Waziri, nenda pale kwenye mgodi wa Geita Gold Mining. Geita Gold Mining wanatumia mafuta, hawatumii gridi ya Taifa na sijajua ni mchezo gani unaendelea. Kwa sababu wanapata exemption kwenye mafuta, wanaingiza mafuta hawataki kuingiza gridi ya Taifa kwenye mgodi wao. Ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri…. (Makofi)

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa!

MWENYEKITI: Taarifa.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, aah ananikata upepo huyo…

T A A R I F A

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza natambua mchango mzuri wa Mheshimiwa Sanga, lakini Geita tayari kuna substation ambayo imekamilika ina megawati 98 ina mwaka mzima na laini ya umeme ilishaingia mpaka mgodini lakini hawajaanza kutumia umeme kwa kisingizio kwamba umeme ule hauko stable. Kwa hiyo, ni muda muafaka Mheshimiwa Waziri kuwasimamia wa-stabilize umeme kuokoa gharama ambazo wanazitumia kwenye mafuta ya diesel.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Festo Sanga unapokea hiyo taarifa?

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napokea taarifa yake na ndiko nilikokuwa naelekea, kwamba Mheshimiwa Waziri watu wa Geita Gold Mining ule mgodi unatumia mafuta. Mafuta ambayo wanayatumia ndani ya mwezi wanatumia mafuta ya Bilioni 3.3 ambayo yana exemption ambayo kodi hiyo ingeweza kuingia Tanzania na ingetusaidia Serikali yetu, kwa siku wanatumia zaidi ya megawati tano hadi 10 kwenye mgodi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale tumetengeneza substation. Substation tuliyoitengeneza ipo kwenye Kijiji cha Mpumbwi kama sikosei, Kijiji cha Mpumbwi ni kilomita sita tu kuelekea mgodini, umeme uingie ili hawa Geita Gold walipe fedha hizi. Megawati tano kwa siku ni fedha nyingi, lakini inaonekana kuna mchezo hapo unaendelea wa uchelewashi wa wale kuingiziwa umeme, na Shirika letu la TANESCO linazidi kukosa mapato kutoka kwenye mgodi wa Geita Gold kwa sababu hawataki kutumia, wameona mlango na dirisha kwenye mafuta, kwenye exemption hawataki kuja kuingia kwenye gridi ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ninakuomba Kaka yangu January Makamba, tuna imani na wewe vijana, wana CCM tuna imani na wewe, Bunge lina imani na wewe, unaenda kuwa ni game changer, issue ni moja kwamba una long strategic plan ambazo wengi hawawezi kukuelewa, lakini ninakusihi kwenye haya maeneo ambayo nimeyazungumza, nenda katatue matatizo ya Watanzania. Suala la umeme kwenye Geita Gold lianze kufanya kazi. Hii exemption ya mafuta tupate fedha hii, hii ni fedha Gold Mining hapa kuna kitu wanakicheza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nishukuru na niunge mkono hoja na nikutakie kila la kheri, ninaamini hii ni moja kati ya bajeti super na Kaka yangu nakutakia kila la kheri. Ahsante sana. (Makofi)