Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Deodatus Philip Mwanyika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika hoja iliyopo mbele yetu ambayo ni hotuba ya Waziri wa Nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema naunga mkono hoja hii iliyopo mbele yetu. Ninapenda vilevile nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu yake nzima, tunaanza kuona sekta inavyozidi kujipambanua, tunaanza kuona transparency kwenye hii sekta, uwazi, Waziri ametuonesha na ametuunganisha na wataalam wa kila aina katika maonesho ambayo tuliyaona hapa karibuni, kwa hiyo ninampongeza sana, ni jambo ambalo linaonekana ni dogo lakini ni kubwa sana, hiyo ndiyo inaitwa leadership. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kwa kuanza, kuongelea jambo ambalo nimelisikia leo hapa kwamba tayari tumefikia mahali ambapo LNG tutakuwa kwenye hatua ya kwanza ya kusaini. Hii hatua ni kubwa sana na sijui kama Wabunge wanaweza kuelewa vizuri kwa nini nasema ni kubwa sana. Jambo hili ni zito, uchumi sasa tunajua kuliko tulivyojua huko nyuma. Kwamba uchumi wa gesi ni uchumi ambao tutautegemea sana tunakokwenda lakini uchumi wa gesi siyo uchumi tu, gesi ni silaha, gesi ni usalama wa Taifa na Mheshimiwa Mwijage ameweza kuielezea vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema na kusisitiza, tunaomba sana kwamba haya majadiliano ambayo yamefikia mahali ambapo sasa wanakwenda kusaini wayakamilishe kwa haraka, hizo signing zifanyike na tuende kwenye hatua nyingine. Tumepoteza muda mwingi sana kwenye suala la gesi, tumepoteza muda mwingi sana, leo hii tusingekuwa hata na kilio cha haya mafuta ambayo tunayasema kwa sababu gesi hii tumekuwa nayo kwa miongo zaidi ya 40.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo nipende kusema kama alivyosema mdogo wangu Mheshimiwa Sanga, Njombe tunayo potential kubwa sana ya ku-generate power, peke yetu tunaweza tukafika megawati karibu 1,200 hata bila Nyerere Dam, Njombe tunao huo uwezo. Kwa sababu ukiangalia tuna megawati 600 pale Liganga na Mchuchuma, ukienda Ruhuji tunakaribu megawatt 360, ukija Lukamali hapa amepazungumzia kuna megawatt 200, ukienda Makambako tunazo megawati karibu 150 za upepo. Lakini tuna mito mingi midogo midogo na maporomoko ambayo yanaweza kuzalisha umeme kwa wingi. Kwa kiasi kikubwa tumekuwa mbali na tumetoa mchango mkubwa sana katika energy sector. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuongelea tu uzalishaji kutoka katika maporomoko madogo madogo. Nchi nyingine pamoja na yote wakiwa na uwezo wa kujaliwa na Mwenyezi Mungu kupata maporomoko ambayo Njombe tunayo, leo hii tungekuwa tunaongelea uzalishaji mkubwa sana wa umeme kutoka katika maporomoko mbalimbali ya mito midogo midogo katika Mkoa wa Njombe, kwa bahati mbaya sisi katika Jimbo langu bado tuna matatizo makubwa ya umeme. Nimepata faraja leo kusikia kwamba na umekuwa muwazi Mheshimiwa Waziri kusema kwamba kilichokwamisha ni nini na Serikali inakwenda kufanya nini. Nipende kumpongeza sana sana Waziri, lakini nipende kumpongeza Mheshimiwa Rais sana kwa haya makubwa mawili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza hilo la LNG ni jambo kubwa anastahili kupongezwa na kwa kweli, kwa LNG nchi hii inaenda kuwa nchi ya uchumi wa gesi. Tunajua itachukua muda kwa vile tumechelewa, lakini tulipeleke kwa nguvu kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye maporomoko madogo madogo ambayo napenda kuyazungumzia. Pamoja na matatizo niliyonayo katika Jimbo langu ya kutokuwa na umeme kwenye vijiji zaidi ya takribani 20 mpaka leo hii na mitaa kadhaa kama 15, tumeweza kuzalisha umeme kutoka kwenye maporomoko haya madogo madogo. Ninapenda kusema tukienda kwenye kijiji kimoja kule kinaitwa Boimanda na Matola, pale tuna umeme ambao unazalishwa na Masista. Kuna mradi wa Masista ambao wameshaunza ni wa maporomoko. Mradi ule umekwama, na nipende kuishukuru Wizara kupitia REA wameweza kuwasaidia kwa kuwapa baadhi ya fedha. Mradi ule unahitaji 2.6 billion dollars wameweza ku-invest wao wenyewe kwa nguvu zao 1.6 billion dollars. Walikuwa na gap ya karibu one million dollars naongelea million dollars siyo billion. Serikali imewasaidia lakini Mheshimiwa Waziri nipende kusema, ukiangalia Masista wale ni Masista wa Benedict Getrude. Masista wale tayari wameshapeleka transmission line mpaka kwenye maeneo ya vijiji wakitegemea kwamba wangeweza kukamilisha generation. Kwa bahati mbaya hawakuweza kwa ukosefu wa fedha, Serikali imeamua kuwasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TANESCO kwa makubaliano na REA walikubaliana waende kwenye maeneo yale, watumie transmission line ambazo zimeingia kwenye maeneo ya vijijini ili waweze kuchukua umeme ambao unatoka kwenye gridi ambao unapita yale maeneo kwenda maeneo mengine ya Ludewa, wautelemshe kwa transfoma uingie kwenye maeneo ya vijiji vile vya Matola na Boimanda na waweze kuwasha umeme mapema. Tunavyoongea wako gizani lakini wana nyaya za umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ninapenda kukuomba wakati umewaleta wataalam hapa niliweza kuongea nao kidogo lakini naomba utie mkazo ili transformer ile ambayo tayari imeshawekwa kwa gharama za TANESCO lakini haifanyi kazi iko idle, ifanye kazi ili wananchi wale waweze kupata umeme kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye jambo la pili la umeme wa maporomoko vilevile. Ninapenda hapa kuzungumzia mradi mdogo wa umeme unaitwa Mapembasi. Mradi huu ni wa siku nyingi, na ninapenda kusema toka mwanzo ni-declare interest kwamba ni mmoja katika waanzilishi wa mradi ule na mradi ule ni mradi ambao una Watanzania professionals katika Serikali, katika Mashirika ya Umma, vijijini wameungana, wamekusanya fedha zao, wengine wazee wamekusanya fedha ya pension kwa ajili ya kuendeleza mradi wa Mapembasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha ni kwamba mradi huu mpaka leo haujaweza kuendelea na kinachokwamisha ni urasimu ambao umejitokeza kwa muda mrefu ndani ya TANESCO na hasa kabla ya TANESCO haijapata uongozi mpya. Nina matumaini makubwa sana mradi huu utakwenda kufanyika sasa. Pia mradi huu unapata tatizo ambalo tunasema ni la kiufundi, kwa sababu ndani ya vifungu vya sheria ambavyo Mheshimiwa Sanga hakuviongelea kwa undani, nipende kufafanua kidogo na hii ni miradi mingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria ambayo ni ya mwaka 2000 ni regulation inasema kwamba, hakuna mtu ataruhusiwa kuingia kwenye miradi midogo midogo ya SPPA kama uzalishaji wake unazidi demand katika maeneo yale ambayo yeye anazalisha umeme. Kwa hiyo, Njombe tunazalisha, tuna-consume megawatt Tano lakini Mapembasi wanaweza kuzalisha megawati 10. Kwa utaratibu wa regulation hii TANESCO hawawezi kuwapa mkataba Mapembasi kwa sababu wao wanazalisha umeme zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nadhani hata logic inakuwa defeated hapa, kwa sababu hawa wanazalisha umeme siyo kwa ajili yao, hawazalishi umeme kwa ajili ya Njombe, wanazalisha umeme kwa ajili yaku-feed kwenye gridi, uende kwenye maeneo mengine na ikiwezekana uuzwe mpaka nje ya nchi. Kwa hiyo, ni wazi kwamba sheria hii inawezekana iliwekwa kwa maksudi Fulani lakini nadhani imepitwa na wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewasikia hapa Wajumbe wa kamati ya Nishati wakisema ikiwezekana ni vema tutumie kila nafasi yakuweza ku-generate umeme katika nchi yetu kwa kutumia rasilimali tulizonazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuna rasilimali zinachukua megawati 10. Tunawezaje kwa miaka karibu Saba bado tunasema kwamba majadiliano yanaendelea? Nimeona katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ameongelea hapa, na nimshukuru Waziri toka ameingia amelisukuma hili jambo lakini bado linakwamba huko TANESCO. TANESCO wanataka umeme huu uuzwe siyo zaidi ya senti Saba American Dollars. Lakini sheria ya EWURA ya SPPA imeshaweka vigezo kwamba ukizalisha umeme kutoka katika maporomoko madogo madogo yasiyozidi megawati 10 unaweza ukauza umeme huo kwa senti 7.8. Lakini wao hawataki, sifahamu wana-interest gani na ndiyo maana watu wengine huwa wanakuja na mawazo kwamba labda kuna kitu ambacho wanakitaka. Kwa sababu sheria iko wazi, vitu viko wazi, lakini hatufanyi progress kwenye mradi huu mdogo wa Mapembasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Mheshimiwa Waziri uendelee na nguvu ile ile ambayo ulishaonesha kwamba utasukuma miradi midogo midogo na hasa ile ambayo iko ndani ya uwezo wa sheria. Hakuna mtu anavunja sheria hapa, sheria inaruhusu, ukiweza ku-develop na mradi huu siyo mradi mdogo ni mradi utakaotumia karibu Dollar Milioni 30 na watu wame-invest. Katika hao ma-shareholder tunao wazee wengi, Mzee Luhanjo alikuwa Secretary ni moja ya wanahisa kwenye mradi ule. Mzee Profesa Mbilinyi mpaka amekufa hajaona hata megawati moja ikizalishwa na ameweka hela zake pale, na kuna professionals wengi, Madaktari na Maprofesa kutoka Chuo Kikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni moja ya mradi ambao ni mfano wa mkusanyiko wa Watanzania waliojitolea ili kuweza kutengeneza power iingie kwenye gridi. Unawezaje kuanza kusita, unawezaje kuanza kuwa na wasiwasi na mradi ambao Watanzania wameamua ku-invest na wanataka kuuza umeme kwa bei ile ambayo inakubalika kwa minajiri ya sheria ya Tanzania. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Deodatus.

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)