Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Tumaini Bryceson Magessa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii, lakini namshukuru sana Mwenyezi Mungu vilevile kutupa nafasi ya kuweza kujadili hotuba hii ya Nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti hii nilikuwa napitia randama, nikaona wazi kwamba katika malengo makubwa ya Wizara ya Nishati moja ni kuongeza uzalishaji, kuboresha mfumo wa usafirishaji na usambazaji wa umeme. Sasa nikawa najaribu kuangalia Waziri anapozungumza ni mahali gani anagusa kuongeza uzalishaji na ni wapi ripoti hii inaongeza kama anaongeza uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu nifanye marekebisho kwamba katika kuongeza uzalishaji inawezekana hii leaflet haikuonesha Bwawa la Nyerere, lakini kwenye vipaumbele vya Wizara hii kwenye randama kipengele “A” kinaonesha Bwawa la Julius Nyerere kwa hiyo inawezekana katika usomaji kuna mahali watu wamesoma tu haraka haraka lakini imeonyeshwa ndio namba moja kwenye vile vipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu yako nzima ambayo wachangiaji wameonesha namna ulivyo na wataalam wazuri, lakini Mheshimiwa Waziri niseme tu wazi mimi ningeulizwa leo mahali gani kuna shida kule kwa wananchi wetu pamoja na uzalishaji huu unaosemwa, ningezungumza shida tunayoipata kubwa ni kutokana na wananchi wetu kuwa na ahadi ya vijiji kadhaa kumaliziwa kupewa umeme na havijapewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiwa na jirani yako anakula, halafu wewe unalala njaa pembeni, unaweza ukajua malalamiko uliyonayo ndani ya moyo na hata ndani ya kusema, kwa hiyo kuna watu wengi ambao tunao kule kwenye vijiji vyetu wanalalamika kwa sababu umeme haujafika kwao. Lakini nikupongeze kwa sababu kama nilivyosema malengo haya ambayo nimesema umeonesha wazi kwamba kuna uzalishaji unakwenda kufanyika sasa shida ambayo naiona katika vile vipaumbele kuna vipaumbele kutoka “A” mpaka “U”; sasa “A” mpaka “U” vinanionesha kama ni vingi sana na hii pesa ambayo niseme tu kwenye randama inasomeka bado ni shilingi trilioni 2.7 lakini hapa imesemwa shilingi trilioni 2.9 maana yake kuna mahali fulani hapajarekebishwa hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nisema pesa hii nina mashaka sana kwenye utekelezaji kama inaweza kufanya haya mambo ambayo yameandikwa huku, kwa hiyo inawezekana mipango ikawa mizuri sana, lakini mwisho wa siku tutakapoanza kuteleza tukaingia kwenye mahali fulani ambako tunashindwa kuitekeleza. Kwa hiyo, niombe sana nikiona hapa kama nilivyosema “A” mpaka “U” inaonesha tuna sehemu tunakwenda kuongeza umeme uzalishaji JK Nyerere megawati 2115.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna Ruhuji megawati 358; Lumakari megawati 222; Kinyerezi megawati 185; Lusumo megawati 80; Malagalasi megawati 47.5; ukiangalia Somanga kuna megawati 330 na sehemu zingine nyingi ambazo zinaonekana kwamba lengo letu inaonekana ni kubwa na mpango wetu mkubwa kwenye hotuba hii ni kufikia megawati 5,000 ifikapo mwaka 2025/2026. Sasa nikawa na mashaka hapo kwamba je, hii allocation ya fedha ambayo tunaisema hapa, itatupeleka kutengeneza na tufikishe megawati 5000 kama tulivyoandika hapa maana tusife mahali tukawa na mipango mizuri kubwa resources zetu hazitoshi.

Kwa hiyo, niombe sana kwenye hoja hii tuhakikishe resource tunazozizungumzia tuna mahali tunaweza kwenda kuzipata ili tuzipate megawati 5000 kwa sababu wananchi wanahitaji umeme sasa, mwanzo umeme ulikuwa ni hanasa lakini sasa hivi kila mmoja ana uhitaji kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna usafirishaji nimeona hapa kuna Rufiji Chalinze - Dodoma Kv 400; kuna Chalinze - Kinyerezi Kv 400; Singida – Arusha - Namanga Kv 220; kuna Rusumo - Nyakanazi Kv 220; kuna Geita - Nyakanazi Kv 220. Sasa nisimame hapa kwenye Geita - Nyakanazi hapa, ndipo Jimbo la Busanda vijiji kadhaa vinategemea vipate umeme kwenye mradi huu wa Geita - Nyakanazi. Hapa vimeandikwa kwamba kuna allocation ya shilingi bilioni 6.53; mradi huu umekuwepo muda mrefu, unajengwa na hauishi, kwa hiyo mahali fulani kwenye vijiji ambayo tunategemea vipate umeme kutoka kwenye mradi huu imeendelea kuwa ni mazungumzo tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanzo nilisema ni nguzo za umeme, lakini baadaye imezungumzwa kwamba sasa kama hapa inatakiwa kwenda kumaliziwa, sina uhakika kama mradi huu utamaliziwa kwa wakati ili wananchi waweze kupata umeme kutoka mradi huu wa Geita – Nyakanazi; kuna Bulyanhulu - Geita Kv 220; kuna North-West Grid Extension ambayo inaenda Mbeya, Sumbawanga, Mpanda, Kigoma na Nyakanazi iko mingi ambayo imeandikwa hapa, lakini more interesting ni mradi ule ambao mnakwenda kuhakikisha kwamba sasa mnaenda ku-rectify SGR.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme kwenda kwenye SGR ambayo sasa hivi ipo kwenye construction, tunategemea kabisa hapa pawe muhimu sana kwa sababu bila umeme maana yake hatutaweza ku-oparate. Sasa inaonekana katika miradi hii ambayo imeandikwa hapa, hiyo SGR rectification ni sehemu yake. Kwa hiyo, niwaombe sana tuhakikishe kwamba tunakwenda kufanya hivi vitu ili wananchi wetu waweze kuona maendeleo ambayo tumekwisha waambia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna kipengele “C” ambacho ni cha kuendeleza miradi ya nishati vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini, hapa kuna changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimboni Busanda mwaka jana kwenye hotuba hii kwenye bajeti hii tulionesha kuna vijiji 57 havina umeme, REA wakaonekana tumepata mkandarasi, mkandarasi yule akaonekana baadaye alikuwa anaonekana performance bond hana, tumepata mwingine, lakini mpaka leo ninavyozungumza mwaka jana vilikuwa 57 na mwaka huu ni 57. Sasa kama tunapima KPI tunataka kuona utekelezaji umefanyikaje mwaka jana vilikuwa 57 na mwaka huu bado viko 57, niwaombe sana unaweza ukajua ilivyo vigumu kusimama kwenye mkutano wa wananchi ukawaeleza mwaka jana vijiji 57 vilikuwa havina umeme, halafu wanakuambia vingapi umeshaweka umeme mwaka huu unasema bado viko 57, kwa hiyo wewe una nafanya zero performance.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nikuombe sitaki kusema Waziri una zero performance kwenye hili, lakini Mbunge ndiye ana zero performance kwa sababu wananchi wanajua hajafanya kitu chochote. Sasa niwaombe sana kwenye REA hapa kwamba kama tumewaambiwa wananchi kuna vijiji 3,617 basi kazi ianze kuonekana, tuanze kuonekana kama vijiji vinapungua ili kufika mwaka 2025 kuwe na mahali fulani wananchi ambao walikuwa hawana umeme wameshapata umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi juzi nimepewa t-shirt kwenye semina ya hapa t-shirt imeandikwa nyuma sasa tunaingia vitongoji vyote, huku nyuma ya t-shirt yangu nimeogopa kuivaa kwa sababu wananchi wanaweza wakanipiga mawe, kwamba mimi jimbo langu lina vijiji 84, halafu nina vijiji 26 tu vyenye umeme na vijiji 58 havina umeme, halafu nitembee na tisheti nyuma imeandikikwa kwa sababu tunaingia kwenye vitongoji wataniuliza, are you mad? Umekuwaje tena? Yaani mmeingia kwenye vitongoji wakati vijiji havina umeme, mbona mmeruka? (KIcheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana nataka hii t-shirt niivae, lakini naomba sasa nihakikishiwe kwamba nikiivaa tunapata kweli umeme kwenye vijiji na baadaye twende kwenye vitongoji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sehemu “D” kwenye randama kuanzisha maandalizi ya kupeleka umeme katika vitongoji vyote ambayo iko ukurasa wa saba kwenye randama yetu, niwapongeze sana kwa hili kama kuna mahali wananchi wanapata shida ni ile kilometa moja tulio-supply umeme yaani mtu umemuonjesha biriani, lakini biriani yenyewe ilikuwa ni punje 10 sasa anatamani aanze kula biriani imekwisha, hebu tuwapelekee nimefurahi sana kusikia sasa unatuongezea kilometa mbili, sijui zinaanza lini hizi, ili walau hizi kilometa mbili hizo zionyeshe kwamba kuna mahali sasa wananchi wameongezewa hii peripheral ya kilometa moja ilikuwa inatuletea ukipiga zile nguzo span ya mita 50 ni nguzo 20; lakini ukipiga span ya mita 100 maana yake ni habari ya nguzo kumi na ngapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba sana ili wananchi wetu waweze kuona maandalizi haya tunayafanya kwenye vitongoji na nyongeza tulioifanya, lakini wako wananchi wengi wameamasika kuweka umeme kwenye nyumba zao na bahati mbaya hapa katikati tumeambiwa mita hakuna, kwa hiyo wananchi wengi wamekwisha fanya wiring, wamekwisha fanyiwa survey, lakini umeme hauendi kwao kwa sababu mita hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa niliyokuwa nayo mchana wa leo ni kwamba mita kadhaa zimeenda, lakini kuanzia wale waliofanya wiring na kuwa surveyed kuanzia mwezi wa pili kuja mwezi wa tano hapa bado mita zile hazitoshi. Niombe sana wananchi wale wapate umeme, maeneo mengi sitaki kuyataja hapa wako wananchi kila anayekupigia simu anaonesha amemaliza hii kazi wiring, amekuwa surveyed lakini hawezi kupata umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi niwaombe sana wataalam Mheshimiwa Waziri kwa sababu scope ya kazi wanaijua, kama scope ya kazi wanaijua maana yake wanajua ni mita ngapi zinahitajika, ni nguzo ngapi za LV zinahitajika, ni wire kiasi gani za copper au aluminum zinahitajika, insulator kiasi gani zinahitajika kuunganisha huu umeme. (Makofi)

Sasa ni mahali gani ambako tunafika mahali tanafanya mradi utekelezeke, lakini tunavyoenda kutekeleza mita 800 hamna, mita 10000 hakuna, hii inakujaje? Kwa hiyo niombe sana tunapokwenda kwenye mradi ambao tayari tutakaa mezani kuandika kwenye makaratasi, scope ya kazi inajulikana, tutatengeneza chart activities zetu tufike mahali kwamba tuna vijua vile vitu tuviagize vije ili wananchi wetu wasifike mahali ameshalipa amefanya wiring lakini anaonekana umeme anasubiri mita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kuna watu toka mwaka jana mwezi wa 10 walikuwa hawajafungiwa umeme, leo ni mwezi wa tano miezi saba na ameshalipa pesa yake hii pesa angelipia mwanafunzi ada, sasa kwa nini aliingiza huku lazima naye ana vipaumbele vya alifikiri angepata umeme azalishe, halafu alipie mwanafunzi ada, sasa imekaa miezi saba, mtoto hajaenda shule, kwa hiyo, niwaombe sana kwa sababu scope tunayo tuwe tunafanya makadirio ambayo yanaweza yakafanya wananchi wetu waweze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Jimboni Busanda kila siku nimekuwa ninasema sisi ni wachimbaji wa dhahabu, sisi ni wakulima, nilitegemea sana umeme uje kule ili hizo maximum demand hizo KVA tuweze kuwalipa, sasa nashangaa inaonekana umeme unaenda mahali kwenda tu kwenye matumizi ambayo ni domestic wakati matumizi ya viwanda yalitakiwa yazalishiwe kule Busanda umeme haufiki. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri inawezekana jicho lako lilikuwa halijachungulia Busanda kwa ukubwa wake nikuombe sana ulete tuchimbe dhahabu kwa kutumia umeme huu ambao tunausema leo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)