Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Abeid Ighondo Ramadhani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia na mimi fursa angalau nitoe mchango wangu kwenye Wizara hii muhimu ya nishati katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya, yale maonesho ya nishati waliyotuletea pale kwa kweli yametujibia maswali mengi mbayo pengine tungeyaleta hapa na ingetuchukua muda mrefu kuzungumza, lakini tuliutumia ule muda vizuri kwenye mabanda yale kwa hiyo tumepata majibu sahihi. Ni ombi langu sasa yale ambayo tuliambiwa yakafanyiwe kazi siyo kwamba baada ya bajeti kupita sasa waka-relax waje watuletee mabanda tena mwakani. Tunataka kazi kule field, mambo yaonekane tuwashe umeme vijijini mwetu kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika moja ya mambo ambayo mimi ningeenda kuuliza isingekuwa yale maonesho ilikuwa ni vile vijiji ambavyo vilisahaulika kwenye ile survey ya mwanzo ama list ya mwanzo ambayo iliorodheshwa ya vijiji ambavyo vinaenda kupatiwa umeme. Kwangu nilikuwa na vijiji Tisa ambavyo ni Mdilu, Mwasauya, Mwakincheche, Itamka, Mwigh’anji, Endeshi na Sefonga lakini vijiji hivi tayari vimeingizwa. Ninachoomba sasa na wenyewe survey ikafanyike ili nao wapate matumaini na wao sasa kupata umeme, maana yake mpaka sasa hakuna kilichofanyika pamoja na kwamba tayari vimeshaonekana kwenye orodha kwamba watapatiwa huduma hii ya umeme. Kwa hiyo, ile kufanya survey itaonyesha kwamba kweli sasa kazi inaenda kufanyika na wao wanaenda kuwasha umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ambalo ni la muhimu sana tunalolipata kule kwa wananchi ni ile kilomita moja. Kwamba umeme unakwenda kilomita moja tu kwenye Kijiji sasa ile haikidhi haja, ni eneo dogo sana. Ninashukuru sana Mheshimiwa Waziri katika presentation yake amesema kwamba kuna timu ambayo inaenda kukaa na kufanya utafiti zaidi, kufanya tathmini ili kuongeza angalau iongezeke iende hata kwenye kilomita tatu mimi naona hiyo ni sawa, angalau kilomita tatu itafikia kukidhi vigezo au kukidhi kuwapatia wananchi wengi huduma hii. Ukizingatia vijiji vyetu ni vikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kwangu nina vijiji vikubwa unakuta Kijiji kimoja kina vitongoji mpaka vinafika zaidi ya kumi. Mathalani Kitongoji cha Sokoine kikubwa kina hadhi ya Kijiji, Songa kina hadhi ya Kijiji, Kwaye na Mapinduzi na vina huduma za Taasisi za Umma, vina shule, vinavyo hospitali wakati mwingine na vina shughuli za kijamii zinazoendelea zinazohitaji umeme. Lakini kwa sababu tumesema ni Kijiji basi umeme unapelekwa pale Kijijini tu kwenye center jamii iliyo kubwa inaachwa haijapata huduma. Kwa hiyo, ninashauri na ninapendekeza maeneo haya kiwango kile cha kilomita moja kiongezeke ili wananchi wetu waneemeke na hii huduma. Na ni-appreciate kwamba nchi yetu ni miongoni mwa nchi nadhani ipo kwenye top three za rural electrification kwa hiyo ni hatua muhimu na sisi tunaiunga mkono lakini ifanyike iendane na wakati ili sasa tuonde na hili tuende kwenye programu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine la muhimu ambalo hili nadhani TANESCO walichukue. Kuna wananchi ambao wamepeleka maombi, wameshajaza fomu, wamefanya wiring muda mrefu wengine zaidi ya miezi sita lakini mpaka kesho hawajawahi kuunganishiwa umeme. Wakienda wanaambiwa mara generator sijui limefanyaje, mara waya sijui nguzo zimefanyaje, mwananchi hataki kujua habari za nguzo yeye anataka umeme uwake. Kwa hiyo, niwaombe sana ndugu zetu wa TANESCO kwa kuwa tuliowana hata siku ile tuliwaeleza haya, mlitusikia basi naomba haya malalamiko yaondoke, wananchi waliyofanya wiring waunganishiwe umeme ili waache sasa na wao kulalamika, waneemeke na hii huduma. Mathalani pale Kijiji cha Mughamu na Kinyasatu ni zaidi ya nyumba 40 wamefanya wiring lakini hawajapata huduma, pale Miangae, Kinyeto wamefanya wiring muda mrefu lakini hawajapa huduma. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri ulichukue hili angalau tuwapatie watu hawa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru tena pia katika hii programu inayoendelea kwangu nilikuwa na vijiji 31 ambavyo vilihitaji umeme lakini kwa habari njema ni kwamba katika programu inayoendelea sasa hivi kuna vijiji nane ambavyo vinaenda kuwasha umeme kabla ya Tarehe 15 ya mwezi huu. Mimi nalipongeza sana Shirika letu la TANESCO, naipongeza sana Wizara, hata Mkandarasi wa ile Central Electrical ambae anasimamia mradi huu kule Jimboni kwangu, mpaka Tarehe 15 amenihakikishia kwamba vijiji nane vinakwenda kuwashwa umeme. Ninakuomba Mheshimiwa Waziri siku hiyo uje tuambatane na wewe tukawashe umeme tukaone taa pale zikiwaka, vijana wakifurahi, wakipokea fursa hii kwa mikono miwili na kwenda kuchangamkia sasa fursa za viwanda na mambo mengine yanayohitaji umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji ambavyo vinaenda kuwashwa umeme nawaomba wananchi wangu wajiandae ni Kijiji cha Muhango, Kijiji cha Mvae, Kijiji cha Kinyagigi, Kijiji cha Munkhola, Soghana, Mwanyonye na Kiyunadi hawa ninaomba sana Mheshimiwa Waziri ujiandae ili siku hiyo ikifika tuondoke mimi na wewe mguu kwa mguu tuhakikishe umeme unawaka kama ambavyo nimeahidiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine na la mwisho kabisa ni umeme wa upepo pale Singida. Walizungumza nadhani wasemaji wawili waliotangulia hapa kuhusu huu umeme wa upepo. Nchi yetu ina uhitaji mkubwa sana wa umeme na tunafahamu gharama kubwa tunayotumia kupata umeme. Sasa kuna huu umeme wa upepo ambao unapatikana Singida, investment yake wala siyo kubwa, lakini kuna Kampuni ambayo imejitokeza muda mrefu zaidi ya miaka tisa sasa ya Upepo Energy mpaka leo tunaambiwa majadiliano yanaendelea, mazungumzo yanaendelea ile michakato tunayolalamika kila siku, mara mchakato na maneno matamu matamu kwa nini hili jambo halifiki mwisho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana hili jambo sasa lifike mwisho umeme huu wa upepo utakwenda kutupatia megawati 100; lakini huyu mzabuni yeye anasema ana uwezo wa kuzalisha hata megawati 300, kwanini apewe megawati 100 tu apewe tender hii ya kutosha ya megawati azalishe umeme wa kutosha ili nchi yetu inufaike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, megawati 300 itapunguza tatizo kwa kiwango kikubwa sana, lakini pia kuna ule umeme wa solar pale Kititimo wa megawati 45 kwa nini hizi project hazikamiliki tender zake? Niombe sana Waziri atakaposimama aniambie tatizo hapa ni nini mpaka mchakato wa kazi/project hii isikamilike na mradi huu wa upepo kwa upande wangu kwenye Jimbo langu unakwenda kunufaisha vijiji nane ambavyo ni Msikii, Kinyamwenda, Itaja, Kinyamwambo, Miipilo, Kinyagigi na Mwanyonye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme huu ukikamilika haya maeneo yatapata umeme hata hatutahangaika na REA ambayo tunasema inakwenda kilometa moja, huu utapanua wigo utakwenda hata maeneo mengine.

Kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri kwa kuwa na yeye ni kijana mwenzangu atanisikia na yeye kwanza ni msikivu, ni mtu ambaye ni mzalendo. Kwa hiyo, niombe sana alichukue hili atakaposimama hapa aniambie nini sasa kinakwenda kufanyika kuhusu project hizi mbili; huu upepo energy pamoja na ule wa solar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya niunge mkono hoja na niwasilishe ahsante sana. (Makofi)