Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Ahmed Mabukhut Shabiby

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Gairo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuwa mmoja wa wachangiaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitaanza kwa upande wa TANESCO na ninataka niseme kwamba Mheshimiwa Waziri kwa upande huu pamoja na Naibu wako Bunge lililopita mliongea vitu vizuri sana kuhusu mipango yenu ya kusambaza umeme kwenye nchi hii na sehemu mojawapo uliyoigusa ilikuwa ni katika eneo la Jimbo la Gairo na maeneo ya Mpwapwa, Kongwa na sehemu nyingine ambayo tunatumia line moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mheshimiwa Waziri anakumbuka nilishakwenda kumlalamikia mara nyingi maeneo ya Gairo umeme unakuwa unakatikakatika sana na mojawapo ya sababu ni nguzo kuanguka hizi za miti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa bahati nzuri sasa hivi tunaona mnabadilisha mnaweka nguzo za zege, lakini hizi nguzo nazo naomba kwa ushauri wangu mjaribu kuziangalia. Hizi nguzo za zege ni fupi kuliko nguzo za umeme zile za miti hata mkiziangalia barabarani unaona ni vifupi vifupi na katika maeneo haya ya kuja Dodoma maeneo haya mpaka kule Gairo watu wengi wanajenga. Kwa hiyo, sasa mtawapa watu usumbufu wenye vile viwanja, otherwise mtaanza tena kuwaambia nunua nguzo ndefu ili labda kama kuna magari yanapita au nini kwa ajili yasiguse. Kwa hiyo, tunaomba muwe makini kwenye nguzo mzidishe kidogo urefu wa nguzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba uharakishaji wa kile kituo cha kupooza umeme, kwa ajili ya kupata umeme wa kuanzisha viwanda katika maeneo hayo niliyoyataja kwa sababu sasa hivi huwezi ukaanzisha pale kiwanda cha mafuta wala kiwanda cha sembe kwa ajili umeme ni mdogo na bahati nzuri Gairo tuna bahati moja, katika Wilaya ya Gairo tunatumia umeme wa aina mbili; tunatumia umeme wa Bwawa la Kidatu na tunatumia umeme wa Bwawa la Mtera. Kwa hiyo, tunatumia umeme pote, pale pana switch kwa hiyo umeme wa Dodoma ukikatika tunawasha wa Morogoro lakini uwezo nao wa umeme ni shida.

Kwa hiyo, tunaomba na kile kituo cha Morogoro-Msamvu toka ile transfoma kubwa iungue hamjaweza kuweka tena transfoma kubwa. Tunajua mna mipango, lakini tunaomba ile mipango mharakishe kwa sababu mipango ya transfoma ile ndio itaweza kuweka umeme mkubwa Morogoro Mjini, Mvomero, Kilosa, Morogoro Vijijini pamoja na Gairo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna matatizo yanajitokeza bahati nzuri nawashukuru REA pamoja na TANESCO kwamba vijiji vyote vya Gairo vimo kwenye programu ya umeme na vimeshapata umeme, kasoro vijiji vya Tarafa ya Nungwe ambayo kuna milima mikubwa sana kama ya Lushoto. Sasa pale wakandarasi wa REA wameweka umeme karibu vijiji vyote, lakini kuna kisehemu ambako wako TFS, kuna misitu kama mita 400 au mita 300. Sasa wale hawataki kuachia ule msitu ili zile nyaya zipite wanadai shilingi milioni 400. Sasa mimi nashangaa Serikali kwa Serikali mnadaiana fedha ili wananchi wapate huduma, wakati wananchi wangu wamekubali kutoa mashamba yao na maeneo yao bure kupeleka huo umeme na hata hao wenyewe watu wa TFS watafaidika na huo umeme kwa sababu mashamba yao ya miti yale yatapata mashine sasa za kutumia umeme badala ya majenereta na dizeli kwa hiyo tunaomba hilo ulishughulikie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ahadi ya Waziri aliyepita Mheshimiwa Kalemani ya gari pale Gairo baada ya kuona yale maeneo ya mlimani na alisema pale pale na aliongea na Mkurugenzi aliyepita kwamba iende pale gari, zilikuwa gari mbili TANESCO moja iende Gairo lakini sasa sijajua je, haya matamshi ya Mawaziri akiondoka linakuwa la kwake binafsi au linakuwa la Kiserikali na Wizara? Naomba ile gari ya Gairo ya TANESCO ifike, tuliongea na wewe, tulimtafuta Mkurugenzi wa TANESCO lakini hatukumpata, naomba ile gari iliyoahidiwa kwa sababu ilikuwepo, tunaiomba ile gari yetu iwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni masuala ya bili za umeme. Bili za umeme ni shida sana, yaani kwa mfano nianze na watumiaji wadogo, yaani mtumiaji mdogo akiwa anaweka umeme wa shilingi 20,000 siku akijiroga tu labda awe na LUKU tu lakini kwa mfano kama ana mita siku akirogwa akiweka umeme wa shilingi 50,000 hata akifunga nyumba wale watakuja na umeme wa shilingi 50,000. Kwa hiyo, nikuambie Mheshimiwa Waziri TANESCO na Wizara yako usione watu wengi sana wamechomoka chomoka humu kwenye Uwaziri hata Mheshimiwa Muhongo, akina Mheshimiwa Kalemani, akina nani na nani sio kwamba walikuwa hawafai, walikuwa wanafaa, lakini watendaji wengi kwenye TANESCO ni matatizo. Kwa hiyo, unaliendesha halmashauri maana yake TANESCO na Wizara yako ni kama halmashauri fulani ya Wilaya hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mazingira mabovu mabovu ni mengi sana humo ndani, kwa hiyo wanafanya timing/kupanga na mimi nimekurushia bili mbili, wewe pamoja na Naibu wako. Kuna sehemu unatumia umeme kuna kitu kinaitwa KVA ile KVA ni nini? Mbona haieleweki maana yake unakuja mtu unaambiwa hapa umeme per unit, labda kwenye wale wanaotumia umeme mkubwa sasa wa viwanda na nini kama alivyosema Mheshimiwa Muhongo kwamba hamuwezi kuendelea bila kuwa na umeme mkubwa na wa bei rahisi. Lakini unapewa unit unaambiwa unit zako ulizotumia ni hizi bei yake ni shilingi milioni sita, halafu unaambiwa kuwa KVA shilingi milioni tatu halafu plus VAT. Sasa ukiangalia hii KVA hujui unaipata wapi, wala haisomeki mahali popote KVA ni kitu gani haijulikani ukiwauliza unaambiwa, unajua umeme ukizima ukiwaka unavyokuja kuwasha mitambo yako pale ndio hii KVA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa huo unawaka kila siku unawaka tu, kwa hiyo kila mwezi na nilikurushia kwa mfano moja kwa jengo moja la Morogoro na lingine la Dodoma; la Dodoma matumizi makubwa KVA shilingi milioni mbili katika shilingi milioni 10 KVA shilingi milioni mbili, jengo lingine la Morogoro matumizi shilingi milioni sita KVA shilingi milioni tatu. Sasa hii yaani tunaonekana kama ni aina fulani ya ujanja ujanja ambao hauna sababu yoyote ya msingi.

Kwa hiyo, hili neno KVA kama mnataka KVA iwepo basi bora muongeze tu bei kwenye unit na mtu anasoma, halafu hamumletei mtu zile mita zenu mnayofunga kubwa mtu hana access ya kusoma. Kwa hiyo, mpaka wewe umletee bili unavyotaka wewe, kwa hiyo unaweka unavyoandika wewe, sasa mteja anapata wapi mahali pa kuangalia pale? Kwa hiyo, hapo tunaomba sana mshughulike na hili suala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nimeshazungumza sana masuala ya mafuta kuna sehemu umeyatekeleza tunakuunga mkono kwa hilo na tunajua wewe hujui chochote kwenye hii Wizara mgeni, lakini nataka nikuambie wewe ni mgeni, Katibu Mkuu ni mgeni Naibu Katibu Mkuu ni mgeni na Naibu wako Waziri ni mgeni. Nilishawahi kujaribu kuongea na wewe siku moja na ulishuhudia kitu nilichokuambia ukakishuhudia mwenyewe na ukakiamini.

Sasa nataka nikuambie haya mambo ya mafuta tunavyochangia najua mnahangaika sana watu wako kutujibu jibu hata kwenye ma-tv na nini, kama yule mmoja Kamishna wa Mafuta anahangaika anasema waliongea Wabunge na sisi mkitujibu na sisi tunajibia hapa, umeona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema hawa Wabunge mafuta yakija na mmehangaika sana, wameita hata semina juzi za Kamati tatu tu kuja kuwaweka sawa pale Hazina, lakini nataka nikuambieni sisi hatuchangii wala hatuchukii mtu, sisi tunachangia kwa sababu tunapenda nchi yetu na tunavyovichangia tunajua, unaweza ukawa profesa wa biashara lakini hujawahi kufanya biashara, unaongea kwa maneno. Unaweza ukawa profesa wa kilimo, lakini huna hata heka moja, kwa hiyo hujui hiyo biashara. Mtu anakuambia nikiagiza mafuta kwa kila mtu nchi italeta mafuta machafu, nchi itapata sijui upungufu wa mafuta toka enzi ya Nyerere, kaja Mwinyi, kaja Mkapa, kaja Kikwete mpaka mwishoni, tuonesheni nchi hii ilipata upungufu lini na ilikuwa inatumia system hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilikuwa inatumia system hiyo lini ilipata upungufu? Hakuna kitu kama hicho na mimi najua kabisa Mheshimiwa Waziri, wewe hujui lolote na ndio maana nilikuambia ukitaka ufanye vizuri hata hawa EWURA safisha kitengo cha…

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Shabiby.

T A A R I F A

MHE: TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa taarifa msemaji Mheshimiwa Shabiby kwamba TPDC toka mwaka 1970 inafanya biashara ya mafuta mpaka mwaka 2002, nchi hii ilikuwa haijapata kukosekana kwa mafuta na ilifanya kazi ya kutafuta petroli na TPDC ikafanya kazi ya kuuza mafuta na bei zikawa nzuri katika nchi hii ahsante endelea. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Shabiby, unaipokea taarifa?

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa yoyote inayokuja mimi napokea. (Kicheko)

Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wangu na Katibu, hebu jaribuni kuangalia juzi nilikuonesha kitu kimoja tu na nikakuambia twende tukapige simu huko uangalie bei za mafuta ni hizi? Kwa hiyo, sisi hatujasema hatutaki bulk procurement, tumesema iwepo lakini ipate ushindani na wawepo na watu binafsi, hakuna mtu amekataa bulk procurement isiwepo iwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hebu ingieni basi hata angalau angalieni kwenye gesi mlitaka muweke bulk procurement wale watu wa gesi wamekataa, leo gesi katika Afrika, Tanzania ni nchi ya kwanza yenye bei rahisi kuliko nchi yoyote ya Afrika, hamjiulizi swali na iko chini ya Nishati? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hao wataalam wanaokupakupa utaalam wewe ni utaalam wa maneno na wa masilahi, mimi narudia kusema hayo maneno. Kuwa mwenyewe na msiweke mtu wa kati. Mnaposema kwamba haya makampuni 28 yameomba kuomba kuleta mafuta, lakini tumechagua sita sasa sisi tunakuwa na uhakika gani si sita yale yale mnayoyapenda? Ninyi mruhusuni kila mtu alete na ile bulk procurement iwepo hiyo ndio ukweli, halafu nilitaka ujiulize swali moja tu na Wabunge wote mjiulize, angalieni toka wakati wa bulk procurement ilipoanza petrol station sasa hivi zinaota kuliko shule za kata. Sasa hapo mjiulize na kuna vitu vingine mimi nataka nikuambie ukweli mimi nitakupa kwa maandishi, sitaki nikupe ushahidi wa maneno maneno ninayoongea hapa, nitakupa kwa maandishi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua wako wengine wamepata shilingi 2,000/shilingi 3,000 hapa hao tuachane nao, kuna watu duniani hawapo na mbinguni hawajafika wanaelea katikati tu umeona bwana. (Kicheko)

Mimi nataka nikupe kwa document, sitaki kuongea kwa mdomo nitakupa kwa document na ninashukuru kwamba umekubali ukaniambia kwamba nikuletee utafanyia kazi. Mimi naomba uliangalie, je, kweli kuna ukweli na hata Mbunge anayetaka naye aje nimueleweshe halafu aone tunavyotandikwa, ahsante sana. (Makofi/Kicheko)