Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Nusrat Shaaban Hanje

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitanukuu maneno ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1962 alipata kusema; “hatuwezi kutatua matatizo yetu kwa kujidanganya kwamba hayapo.” Wizara hii ni Wizara ambayo mimi naweza nikaichukulia kama Wizara ya mfukoni kwenye pochi la mama, kwa sababu mama ameweza kutoa shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kusaidia kushusha bei ya mafuta ambayo imeonekana inaathiri wananchi wengi sana wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa masikitiko makubwa sana leo mpaka tunafunga Bunge saa 7.00 mchana bado Wabunge walikuwa hawajapata taarifa ya Kamati kuona mapendekezo ya Kamati kwa sababu ya unyeti wa information ambazo Wabunge wangeweza kusaidia/kumsaidia mama ili fedha aliyoitoa asione kama imepotea kupeleka kwenye sehemu ya mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo niwapongeze sana Wabunge wenzangu kwa sababu wamejitahidi kutafuta taarifa nyingine sehemu nyingine na wameendelea kusaidia kuchangia kwenye kuona namna gani tunaweza tukasaidia Taifa letu na isionekane kama Serikali imepoteza fedha, kwa sababu tunahitaji fedha mno kuna miradi ya barabara, kuna miradi ya hospitali, kuna miradi ya shule, lakini mama ameona apeleke upande wa mafuta kwa ajili ya kupunguzia Watanzania gharama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tarehe 25 Mei Mkoa wa Singida mzima ulikatika umeme na kwenye mitandao ukaonekana kibonzo kinasambaa kwamba mtu anasema Singida nzima umeme umezima halafu mwenzie anamjibu kwamba unaishi Singida kwani wewe ni alizeti? (Kicheko)

Mimi kama Mbunge wa kutoka Mkoa wa Singida kwa mpango huu ambao nimeona na namna ambavyo Mkoa wangu umetajwa kwenye bajeti ya Nishati, ninasikitika kwamba inawezekana Serikali inafikiri wanaoishi Singida wote ni alizeti. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka mingi tumekuwa tunajadili kuhusiana na umeme wa upepo Mkoa wa Singida na kila Mbunge wa Mkoa wa Singida anayesimama anaongea kwa sababu kuna uwezekano mkubwa sana wa umeme wa upepo Mkoa wa Singida ukasaidia wananchi wa Mkoa wa Singida, lakini pia ukasaidia watanzania wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka tunapozungumza Singida ni miongoni mwa Mikoa ya Tanzania ambayo miundombinu yake na upatikanaji wake wa umeme bado unasuasua. Ukisoma bajeti ya Wizara ya Nishati inaonesha kwamba wana-respond (wanaitikia) ile mipango ya maendeleo endelevu SDGs namba saba ambayo inalenga kutoa upatikanaji wa nishati safi ya uhakika na gharama nafuu. Lakini nasikitika sana mimi nimezaliwa kijijini kwenye giza, kwa taarifa za waliokuwepo wakati nazaliwa wanasema nilizaliwa kijijini kabisa kwenye giza, kwa hiyo, ninasikitika sana kwamba mimi nakaribia kuzeeka bado Watanzania wamama wa Singida wanajifungulia kwenye vibatari na giza kwa sababu bado Singida hospitali hazijaunganishwa kwenye umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana na jambo hili sio geni, Wabunge wengi sana wanaotoka vijijini wanajua kama Watanzania bado wanajifungua kwenye vibatari, bahati mbaya hata bei za mafuta zinazotegemewa kushuka bei ya mafuta ya taa bado haijaguswa kabisa. Mimi natoka mkoa ambao sehemu kubwa ni vijijini, kwa hiyo, watumiaji wa vibatari na taa za chemli bado wapo ni masikitiko yangu makubwa sana. Kwa sababu mimi ni mama wa Mkoa wa Singida, naomba nitaje katika Wilaya ya Ikungi zipo zahanati ambazo hazijaunganishwa na umeme. Bahati mbaya sana katika Wilaya ya Ikungi zahanati 33 hazijaunganishwa na umeme lakini pia bahati mbaya zaidi Jimbo la Singida Magharibi zahanati 20 hazijaunganishwa na umeme mpaka tunapozungumza na umeme umepita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wananchi wanakwenda hospitali, wanatumia tochi, mama anajifungua kwa kutumia tochi anatoka nje anaangalia umeme umepita juu. Zahanati ya Kintandaa, zahanati ya Mtunduru, zahanati ya Ihombwe, zahanati ya Msosa, zahanati ya Mgungira, zahanati ya Yumbu, zahanati ya Mwaru, Ntuntu, Minyuhe, Iglansoni, Muhintiri, Nduru, Mpugizi, Mnang’ana, Kipunda, Songandogo and the list goes on. Inasikitisha mno Ubunge wangu mimi mwanamke kutoka Singida hautakuwa na maana kama tutaendelea kuacha akina mama wajifungue kwa kutumia tochi za simu, haiwezekani. Bajeti ya Wizara ya Nishati imeongezeka asilimia 13; kuongezeka kwa bajeti hii kukatoe tafsiri kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania hawajui miradi mikubwa na tunaipongeza, lakini niseme tu matumaini ambayo ninayo kama mimi kwa sababu mimi pia Mjumbe wa Kamati miongoni mwa miradi ambayo imepewa fedha kubwa sana katika ongezeko la bajeti ambayo imeongezeka ni pamoja na umeme wa REA Vijijini.

Kwa hiyo, Watanzania waelewe na tunategemea huwa nashangaa kwa nini Serikali wakati inaweka mikakati haiangalii maeneo muhimu? Hatuwezi kujadili kupeleka umeme shule, kupeleka umeme kwenye mahakama bila kujadili hospitali? Mimi naweza nikalala nyumbani kwangu na kibatari, lakini nakwenda kujifungua hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma za afya zinategemea umeme, kuna vipimo vingine lazima utumie umeme. Kwa hiyo, wakati unapanga na tunategemea REA kwa ongezeko hili na wao ni sehemu ya kipaumbele watumie ubunifu wao wote kuhakikisha kwamba kipaumbele cha kwanza kinakuwa kuunganisha vituo vya afya na zahanati zetu ili akina mama ule mzigo ambao Mheshimiwa Rais alisema kwamba mzigo wa usawa wa kijinsia kwenye mabega yake ni mzito zaidi, kwa sababu ni aibu tuna Rais mwanamke, halafu kuna watu ambao wanatakiwa wamsaidie ili wanawake wenzake wasijifungulie kwenye giza, lakini wasaidizi wake inaonekana wanashindwa kumsaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana kwa niaba ya akina mama wa Tanzania tunaomba muwasaidie wanawake kuunganisha hospitali umeme ili waweze kupata huduma za afya kwa mazingira ambayo ni rafiki ili waweze kufanya kazi ambazo zitasaidia wao kuchangia Pato la Taifa, tumsaidie Mheshimiwa Rais kufanya kazi, ahsante sana. (Makofi)