Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Catherine Valentine Magige

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nianze kwa kumpongeza Waziri kaka yangu January kwa kazi kubwa unayoifanya pamoja na timu yako nzima pamoja na Naibu Waziri, Mheshimiwa Rais hakukosea kukupa hii Wizara unaimudu na unaiweza chapa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kuanzisha mpango wa kuwa na hifadhi ya kimkakati ya mafuta na kuhakikisha kwamba TPDC inawezeshwa kushiriki katika biashara ya mafuta kupitia kampuni yake tanzu ya TAN OIL ili kuwezesha upatikanaji wa mafuta nchini. Ieleweke kwamba TPDC haifanyi biashara hii yenyewe inafanya usimamizi inayofanya biashara hii ni TAN OIL. Hii ni hatua nzuri sana niwapongeze, tumeona nchi za wenzetu kama Saudi Arabia, Algeria na Falme za Kiarabu wanatumia makampuni katika mataifa yao katika biashara hii. Niwapongeze sana Serikali niipongeze Wizara na Waziri na timu yako yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kwa kutenga Shilingi Bilioni 500 kwa kuboresha grid ya Taifa, pesa hizi zitasaidia upatikanaji wa umeme na kupunguza tatizo la umeme. Tunajua umeme ni uchumi, umeme ni kila kitu tunajua Bilioni hizi 500 zitasaidia sana. Sambamba na kupongeza Serikali naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mtendaji Mkuu wa Tanesco Ndugu Maharage Chande anafanyakazi kubwa sana tunaiona na tupo pamoja naye tunamuomba endelea kufanyakazi kuhakikisha changamoto hii ya umeme kwa wananchi inapungua kama siyo kuisha kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali kwa kutenga Shilingi Bilioni 140 kwa ajili ya kuendelea kusambaza miradi ya umeme vijijini na pia kwa ajili ya kuongeza kusambaza umeme katika vitongoji. Changamoto ya umeme katika vijiji bado ipo kwa baadhi, mimi mwenyewe katika Mkoa wangu wa Arusha katika vijiji vya Wilaya ya Longido, Karatu, Arusha Mjini, Ngorongoro, Arumeru, Meru, kote huko bado kuna changamoto ya baadhi ya vijiji kukosa umeme. Mheshimiwa Waziri nilikuletea list ya vijiji vyangu na uhakika kabisa uliniahidi vijiji vyangu vya katika Mkoa wa Arusha ambavyo havina umeme vyenye changamoto vitapata mpaka vitongoji. Kwa hiyo tunasubiri wananchi wa Arusha umeme huo uweze kutufikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kutenga Shilingi Bilioni Moja katika mradi wa kuhamasisha matumizi endelevu ya nishati safi. TUNAJUA 20% ya wagonjwa wanaosumbuliwa na mfumo wa upumuaji unatokana na matumizi ya kuni, tunaimani kabisa mradi huu utasaidia sana hasa akinamama ambao wengi ndiyo tunahangaika katika kupika kwa kutumia kuni. Tunajua Mheshimiwa Waziri wewe ni mdau mkubwa wa mazingira ulikuwa katika Wizara ya Mazingira, Tanzania tulikuwa tumeshazoea mifuko ya plastic uliacha alama ulihakikisha Tanzania sasa hivi mifuko ya plastic hakuna tumeisahau kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kukutia moyo Mheshimiwa Waziri najua wewe ni kijana mchapakazi, hakuna sehemu ambayo unapita huachi alama, kila sehemu unaacha alama na tunayo imani kabisa utaacha alama kubwa sana katika Wizara hii tuna imani na wewe, Watanzania tuna imani na wewe, chapa kazi tuna imani na Naibu wako pia Makatibu Wakuu na wote katika Wizara yako timu yako nzima tuna imani na ninyi chapeni kazi wananchi wana mategemeo makubwa sana na ninyi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna imani sana na Mheshimiwa Waziri, Rais alimteua January hakufanya makosa kwa sababu tumeanza kuona, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini, tumeona kazi kubwa inayofanywa na Wizara pamoja na Watendaji wote wa Wizara hii, naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)